Monday, 16 June 2014

USIKU KUCHANGIA JENGO LA WASICHANA WANAOKWEPA UKEKETAJI TANZANIA


Niko hoteli kubwa la The Russet, katikati ya maskani ya wafanyakazi wa kawaida, kaskazini ya  London. Nimealikwa kutumbuiza ngoma za Kiafrika. Mauzo ya sherehe hizo yatasaidia kijiji kimoja Tanzania. Watayarishaji ni shirika la urafiki baina ya Uingereza na Tanzania, BTS yaani British Tanzania Society. Janet Chapman na mwenzake Jonathan Pace, ni wale wazungu wachache wanaofikiria mazuri tu kuhusu Waafrika, hususan Watanzania.
  Watu wa makamo.
Miaka 30 iliyopita  Janet alifanya kazi ya ualimu Sudan,  vijijini; akichanganyika na wakulima na wafugaji maskini. Kati ya jambo ambalo hakulipenda ni mila ya kuwatahiri wasichana wadogo au kwa Kiswahili cha kileo, ukeketaji.  Janet anasema kwa kuwa mwenyewe alikuwa na mabinti wadogo wawili- ambao leo wameshakuwa watu wazima- yalimgusa sana. Baadaye aligundua adha hii imeenea nchi nyingi   bara Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

 Takwimu za shirika la Afya duniani (WHO) zinakadiria wasichana na wanawake milioni 91 na nusu barani wamekeketwa. Kati ya hawa milioni 12 na robo wana umri mdogo wa miaka 10 hadi 14.  Tovuti la habari za ukeketaji (FGM) linadai nchi 26 za Kiafrika, ikiwemo Tanzania zinabeba bendera ya ukeketaji. WHO inafahamisha kati ya wanaotetea adha hii ni mama wazazi waliokeketwa na  baadhi ya wanaume.


 Kufuatana na taarifa za madaktari wa Kitanzania,  maisha ya asilimia 50 ya wasichana wetu vijijini yamo hatarini. Hatari zipi? Waganga wanaeleza wasichana (na wanawake kijumla) wanaokeketwa hutokwa damu mara kwa mara, huwa na maumivu wakati wa haja ndogo na kubwa, maumivu siku za hedhi na uja uzito, na hali ngumu wakati wa kujifungua. Mwanamke wa aina hii, taarifa hii iliyoko mtandao wa Tanzania Trust Development Fund, ( kitengo kinachosaidiana na BTS) inaendelea kufahamisha, ni mtu mwenye maumivu maisha yake yote, na si tu maumivu bali pia urahisi wa kifo. Takwimu za mashirika yanayopinga ukeketaji duniani yanasema mathalan, uchunguzi uliofanywa karibuni, Sudan umethibitisha utasa na kutozaa kutokana na madhara ya ukeketaji katika asilimia 25 ya wanawake kule.
Baadhi ya waliohudhuria toka Bara Hindi wakishangilia kwa makofi na vigele gele. Picha ya See Li...

 Hapa Uingereza, kama ilivyo Tanzania, ukeketaji umewekwa fungu la uhalifu na waganga wanaohusika na upasuaji au shughuli hii wanaendelea kufikishwa mahamakani na kufukuzwa kazi, kila kukicha.
Sherehe ya leo basi, imetayarishwa na Tanzania Development Trust shirika mtoto wa British Tanzania Society (BTS). Lengo lake ni kutafuta fedha kuchangia ujenzi wa nyumba ya wasichana wanaokimbia au kukwepa ukeketaji, Mugumu, mkoani Mara wajisalimishe. Pale watapewa mafunzo mbalimbali ya kuwaendeleza mathalan useremala, kushona na matumizi ya tarakilishi (kompyuta).  Ingawa robo tatu ya wanamuziki tunaoshiriki  ni wanawake,  wanaume pia tumo..
 Leo ukeketaji ni adui mosi wa afya na maendeleo ya wanawake. Harakati dhidi ya adha hii zinamakusudi ya kuhusisha wote: wavulana, wasichana, wanawake, wanaume!
Kwanini  kila mtu?
Wahudhuriaji wa Kizungu...picha na See Li...

Sote tunao dada, mama, bibi, mabinti, shangazi, sahiba wa kike, mama wadogo, nk.
Pili, wanawake ndiyo waendelezaji wa familia na wazaaji wa watoto. Vizazi vijavyo.
Tatu, chakula na uchumi wetu unategemea sana  maisha ya wakulima, wanawake na wanavijiji.
Katika makala yake “Wanawake na Maendeleo ya Riziki” mwanataaluma Ruth Meena anasema wanawake huchangia asilimia 80 ya kazi mashambani. Bi Meena anamnukuu Mwalimu Nyerere aliyewahi kuandika:
 “Itakuwa vizuri kuwauliza wakulima wetu hasa wanaume, je hufanya kazi saa ngapi kwa juma? Ukweli wanawake vijijini humenyeka sana, saa 12 hadi 15 kwa siku. Hufanya kazi  Jumapili hata sikukuu. Wanawake wa vijijini hufanya kazi kuliko mtu yeyote mwingine Tanzania. Lakini wanaume wanaoishi vijijini huwa mapumzikoni katika nusu ya maisha yao.”
Mikoa 19 ya Tanzania inaendesha ukeketaji. Je, ni mtu gani huyu anayemenyeka akiwa katika maumivu maisha yake yote?
Mtanzania Malkia Kassu, akiwa mbele ya meza ya kutangaza Watanzania na shughuli zao. Picha na See Li...

Basi ,  tuko klabu ya The Russet,  London.
Kiingilio ni paundi 6 ambazo ni kama dola kumi au shilingi 15,000. Kila senti itapelekwa kusaidia ujenzi huo wa Mugumu. Jumba litaendeshwa na kanisa la Anglican na watu wa madhehebu yote watakaribishwa kujihifadhi hapa. 
Ninapoingia hotelini na ngoma yangu, napokewa na Janet na Jonathan. Wakati tukisalimiana, Mtanzania mmoja mkazi  Uingereza, Peter Mwita anajitambulisha. Kasafiri mbali sana  (toka Cardiff, Wales) na binti yake kuunga mkono shughuli hii. Wapo Watanzania wawili wengine. Chris mzawa wa Meru, Arusha na mkewe Mwingereza. Wanao watoto watatu. Na Malkia Kassu, mshindi wa taji la Miss Commonwealth Afrika 2013, kasimama akitabasamu na mavazi ya kupendeza. Yeye ndiye atakayeongoza mchezo wa bahati nasibu yenye zawadi ya vitu kutoka Tanzania. Malkia Kassu mwenye umri wa miaka 23  katulia kando ya meza ya BTS na majarida mbalimbali ya habari za Tanzania. Lakini pamoja na haya yote, asilimia 99 ya waliofika kuchangia fedha hizi si Watanzania. Takriban wote ni Wazungu, Wahindi na makabila mengine ya Ulaya. Wamechangamkia shughuli hii inayoitwa “Songs For Our Sisters” (Nyimbo kwa dada zetu).
 Wanamuziki tumechanganyika pia.

 “Sokoshimba” (pichani juu) ni Wazimbabwe wawili, mmoja maarufu Uingereza, anaitwa Anna Mudeka. Wanapiga marimba na kuimba Kishona na Kindebele. Wamevalia mavazi mazuri ya vitenge na kofia za mapambo ya Kiafrika. Yupo mwanamke wa Kituruki, Lora Linhares Max, anapiga gitaa la Kizungu linaloshikwa chini ya bega na kutumia kijiti chenye mshipi. Fidla. Na wanamuziki wengine wengi.
Mimi ninatwanga manyanga na bibi wa Kiarabu toka Libya, mwanamuziki na mpiga ngoma maridhawa, Nadia Al Faghih Hassan. Jukwaani tunatumbuiza mseto wa ngoma za Kitanzania (mathalan Mawindi ya Kinyiramba) na mashuhuri ya Kiarabu iitwayo Fellahi.
Nadia Al Faghih Hassan akitumbuiza. Picha na See Li

Ngoma hii ya “Fellahi” kidesturi ni ya  wakulima wa Misri.  Wanawake katika kadamnasi wanapiga vigelegele wakitamkiwa magoma moto. Mmoja toka Uajemi (Iran) hajivungi. Anaaamka akisuka suka na kutikisa mabega, akizungusha kiuno na kunyapua nyapua miguu.
Mwandishi na ngoma yangu. Picha ya See Li...

 Uhondo wa mabibi na mababu umempanda. Tunatandika ngozi ya mnyama na miti. Ngoma!
Julian Marcus wa British Tanzania Society (BTS) akijivunia shati la Kiafrika. Aliendesha meza iliyotangaza shughuli za Watanzania...Picha ya See Li...

Ni usiku  wa raha ya muziki, vinywaji na chakula. Ijumaa tarehe 30 Mei. Hakuna hotuba ndefu wala maongezi mengi. Kila mtu anafahamu kwanini kahudhuria. Kesho yake watayarishaji wanatufahamisha, zimepatikana paundi 1,000 na zaidi (shilingi milioni tatu na nusu).  Kijumla fedha inayotakiwa  ni paundi 60,000 – takriban shilingi laki mbili milioni. Bado sana. Onyesho jingine kuendelea kutafuta fedha linatazamiwa  Oktoba. Inshallah
Mwanamuziki Lora Linhares Max na gitaa lake...Picha na See Li...



 Ilichapishwa na marekebisho machache,  Mwananchi Jumapili- Juni 15, 2014.

No comments:

Post a Comment