Bangi.
Neno lenye maana na majina
mengi. Marijuana. Cannabis. Sigara kali. Spliff. Kaya. Na kadhalika. Kwa Kiswahili
asili ya neno “bhang” ni Kihindi. Sina hakika kama zamani kabla ya ujio wa
wageni tulilienzi jani hili. Jani lililo mkebe mmoja na “kunguni” wa dawa za
kulevya. Heroin. Unga wa Cocaine. Na mengineyo.
Dawa zinazomgeuza mwanadamu dude, afriti, mahoka, jambazi. Dawa zenye uwezo wa kuharibu jamii kama ilivyo Mexico sasa hivi. Unabisha? Ingia,
You Tube.
Uuone uhayawani wa dawa za
kulevya ulivyoshawabadili wanadamu mafisi. Kuwapeleka wake, mabinti na dada za
majambazi wenzao mwituni kuwafyeka shingo na mashoka. Tunaambiwa magaidi wa
ISIS huko Syria na Iraq, hukata shingo. Mexico hukatakata mwili vipande vipande
kisha wakaviacha viozee vichakani
mithili ya vinyesi.
Hebu tafakari ufisi kama huu ujipenyeze Tanzania. Ndiyo
mwisho. Hatuna tena nchi ya amani wala kuingia mitaani wikiendi kula nyama
choma; kuzamia misikitini, jamatini au makanisani. Ni harufu ya damu kila
mahali. Ulaghai kwisha kazi. Hamnazo.
Sasa bangi...
Katika miaka arobaini iliyopita wanamuziki
dunia iliyoendelea wameiremba bangi kama asusa, starehe, ubabe, nk. Miaka ya Sitini bendi za Kizungu
zilisisimka na utamaduni mzima ukaitwa Flower Power- nguvu ya maua. Matamasha
mashuhuri mathalan, Woodstock (1969), Marekani yaliitukuza. Kuanzia hapo vifo
vya wanamuziki maarufu vikawa “kawaida”.... Miongoni mwao- mpiga gitaa mkali kuzidi wote - Jimi Hendrix
(27), mwimbaji Janis Joplin (27) na Jim Morisson (27) aliyeongoza bendi ya The
Doors. Vijana hawa wenye vipaji tosha, walifariki kipindi
cha 1970 na 1971. Karibuni, 2011 mwimbaji wa Kiingereza Amy Winehouse, naye
alititigwa kwa ukunguni huu akiwa na miaka 27! Astafurlah.
Awal kabla ya haya, miaka ya 1940
na 1950, wanamuziki waliobobea humo walikuwa wapigaji wa Jazz. Mfano, Charlie Parker (mpiga
Saxafoni babu kubwa anayeigwa hadi leo) alikufa ghafla 1955. Alikuwa na miaka 35 tu, lakini mganga
aliyetathmini maiti yake alishangaa alivyochakaa akaonekana ajuza
wa miaka 70.
Muziki wa Reggae toka Jamaica
uliovuma miaka ya Sabini, NDIYO ulioiweka bangi mbele ya taswira. Wanamuziki wa
The Wailers, Peter Tosh , Bunny Livingstone Wailer na Bob Marley, walidai bangi ni sehemu ya
dini ya Rastafari yenye mizizi Ethiopia. Kutokana na maudhui ya muziki wao
uliozungumzia jamii na unyanyasaji, bangi sasa ilipewa hadhi mpya. Mwaka 1978 Bob Marley alitoa Albam nzima
(Kaya) iliyoghani mapenzi, mashairi, siasa na kutukuza bangi.
“Bangi,” aliwahi kusema marehemu
Marley, “ni jani linalookoa taifa; ilhali pombe ni uharibifu.”
Basi uvutaji bangi kama kitu kinachoua, ukageuzwa kheri.
Hususan kwa maudhui ya Reggae yenye siasa za kimaendeleo na dini ya Rastafari.
Kwamba ukiivuta utauona ukweli wa harakati.
Mwaka 1976, Peter Tosh,
alichapuka na Albam kuchangia kampeni ya kuihalalisha bangi kisheria. Jalada la
“Legalize It” lina picha ya mwanamuziki huyu -aliyekuwa pandikizi la mtu-
akivuta kiko kinafoka moshi wa bangi. Marehem Tosh aliuawa na majambazi nyumbani
kwake (1987). Na alifafanua sababu za
msimamo huu ndani ya mahojiano na gazeti
la London, New Music Express, 1978.
Akasema aliamua kutunga nyimbo za kutetea kuvuta bangi na kuihalalisha
kutokana na kile alichokiita kuonewa na kunyanyaswa na polisi wa Jamaica.
Baadhi ya maneno ya wimbo “Legalize
it” hudai:
“Ihalalishe.
Waimbaji wanaivuta,
Wapigaji vyombo pia,
Madaktari wanaivuta; wauguzi; mahakimu .
... Usiikosoe. Ihalalishe
Ni nzuri kwa mafua, pumu,
kifua kikuu
Ndege wanaila, mchwa na sisimizi wanaipenda
Mbuzi hupenda kucheza nayo...”
Marehemu Peter Tosh akiwasha bangi. Picha ya mtandaoni...
Kitaaluma, ziko aina tatu za
jani la bangi : Cannabis Sativa, Cannabis Indica na Cannabis Ruderalis.
Cannabis Sativa na Indica ndizo huvutwa zaidi; ilhali Cannabis Ruderalis (yenye
miti mifupi, na inayolimwa nchi za
baridi kama Urusi) hutengenezea dawa. Katika
miaka 30 iliyopita watetezi wa bangi wamepigania kuhalalishwa kwa bangi kijumla.
Baadhi ya jamii zimeiruhusu.
Kiongozi ni Uholanzi ambapo bangi huuzwa katika mikahawa na vitafunio vingine.
Mji wa Amsterdam hutembelewa na watalii
wengi kutokana na “uzuri” huu. Baadhi ya majimbo ya Marekani mfano Colorado
yamepata kibali cha kulima na kuuza bangi kama dawa kwa wagonjwa wenye maumivu
makali na wavutaji holela.
Nchini Uingereza kampeni imepingwa
sana. Hapo hapo imetetewa na baadhi ya wanasiasa
na matajiri mathalan mwanamuziki Sting, mchekeshaji Russell Brand, mwandishi
Wil Self -ambaye vitabu vyake vimetafsiriwa lugha 22 -na mfanyabiashara milionea, Richard
Branson anayemiliki ndege za Virgin.
Dhana imepingwa lakini si kwa ushahidi
kama juma hili.
Mtafiti na mtaalamu wa chuo
kikuu cha King’s College London, Profesa
Wayne Hall alisema madhara ya bangi ni makubwa kuliko faida. Profesa Hall ambaye ni mshauri wa shirika la
Afya Duniani (WHO) kasimamia utafiti
yakinifu wa miaka 20 na kufikia hatima ifuatayo.
Kwamba kiasi kikubwa cha
vijana chini ya miaka 20 wanaovuta bangi
huanguka darasani, hupungikiwa uwezo wao
wa kufikiri na hatimaye kuitegemea kwa kila kitu. Ni kama ulemavu.
Kwamba ukishakuwa sugu wa
bangi utataka vikali zaidi!
Kwamba bangi inaongeza hatari za
kuwa mwenda wazimu kwa maradhi kama “psychosis” (kupoteza hisia za hali halisi)
na “schizophrenia”. Maradhi ya “schizo”
humfanya mhusika kusikia kelele au sauti kichwani. Kelele hizo humtoa mhusika
katika ukweli wa mambo na kumjengea njozi za kila aina. Baadhi za kuua.
Kwamba kina mama waja wazito
wanahatarisha maisha ya watoto, tumboni.
Kwamba ni rahisi kwa madereva
waliovuta bangi kusababisha ajali hasa wakiongezea pombe juu.
Fikra za Profesa Hall zilizotangazwa
na magazeti makubwa Uingereza zimesabisha zogo kali. Wavutaji wengi Majuu ni
watu wanaojiweza.
Je, kwetu ambapo wavutaji ni
maskini, vijana wasio na elimu au ajira maalum? Uzunguni maradhi ya akili hutafutiwa tiba na
serikali ina idara na mifuko maalum ya kuhudumia wasiojiweza. Je, kwetu kusikokuwa
na “starehe” hii ya kusaidiwa? Je, serikali zetu nchi changa zitapata wapi muda
wa kuhudumia walevi wa dawa za kulevya badala ya kuelemisha kiasi kikubwa cha
wananchi wanaohitaji mabadiliko ya maisha yao?
Ushauri mmoja tu. Kwako Mwafrika. Achana na bangi.
Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili Oktoba 12, 2014
No comments:
Post a Comment