Leo tuzungumzie watoto. Tuangalie afya,
mapenzi na usalama wao. Hakuna kipindi cha historia yetu wanadamu ambapo watoto
wanafanyiwa unyama duniani kama sasa.
Mwezi Machi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya
Watoto (UNICEF) lilisema tangu vita vianze Syria, watoto 10,000, wameuawa makusudi. Wengine milioni tano hawana makazi
maalum. Mauaji haya yanafanywa majumbani,
mashuleni, mitaani na kambi za wakimbizi.
Watoto wanapigwa risasi makusudi na magaidi wa Boko Haram, Nigeria. Miezi
miwili sasa wasichana 200 waliotekwa
mkuku na wanaharam hawa (wanaotumia dini kama ngao ya uyahawani wao)
hawajapatikana. Kila kukicha watoto vijijini na mashuleni Nigeria wanauliwa
bila hatia yeyote.
Wiki iliyopita mtoto wa Kipalestina, Tarik Abu
Khdeir, mwenye miaka 15 alipigwa na askari wa Kiyahudi jimbo la West Bank
nusura afe. Alipokuwa akiongea na wanahabari uso mzima ulikuwa umemvimba
utadhani kaota vichuguu vya mchwa. Kipigo kilifuatilia mgogoro kati ya
Wapalestina na Wayahudi. Watoto watatu wa Kiyahudi walikokotwa njiani wakakutwa
wamefariki kitongoji cha Wapalestina. Serikali ya Israel ilidai Hamas iliwaua.
Ili kulipiza kisasi mtoto wa miaka 16 wa Kipalestina, Mohammed Abu Khdeir, naye
aliburutwa barabarani , akapigwa kikatili na kutupwa msituni kama fuko.
Ingawa waliohusika wameshakamatwa na askari
wa Israel, haisaidii kurudisha maisha ya watoto.
Barani Afrika, nchi zenye vita mathalan,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan na Kongo, unyanyasaji wa watoto ni jambo la
kawaida. Umoja wa Mataifa umekadiria asilimia 65 ya ubakaji uliofanywa Kongo kipindi
cha miaka 15 iliyopita uliwaathiri watoto. Asilimia kumi ya watoto waliobakwa
Kongo wana umri chini ya miaka kumi! Mbali ya kubakwa, kupigwa au kulawitiwa
watoto hulazimishwa kubeba mizigo na kuwa askari.
Kwetu Tanzania mateso ya watoto- kwa njia
mbalimbali- yamefikia daraja la kishetani kwa taifa hili lenye utamaduni mahsusi wa amani. Juma lililopita msichana wa
kazi za nyumbani, ambaye jina lake halikutajwa (aliitwa tu “Hausigeli”utadhani
kijiti au kifuu cha nazi) aliteswa miaka miwili na tajiri wake, Boko,
Kinondoni. Picha za mwajiri huyo, Yasinta Rwechengura, akisindikizwa na askari
mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Ulaya ya Kinondoni, ziko sambamba na msichana
anayebubujikwa damu kichwani na kifuani; bado kigoli. Mateso ya watoto wanaofanya kazi
majumbani hayasemeki. Kwa kuwa hawana midomo,
haki au cha kuwatetea, hali zao hazifahamiki.
Baadhi ya maoni ya wasomaji wa “Global Publishers” la Bw Eric Shigongo,
yanadhihirisha huruma na mshangao wa wananchi kuhusu mtoto huyo wa kazi.
“Huwezi
kumtesa binadamu mwenzio kiasi hiki hata kama amefanya nini, unampiga
kama mwizi, lahaulaa. Ilhali yeye ndiye anayeangalia nyumba yako?”
Au
“Yaani ukatili mwanamke unamfanyia mtoto wa mwenzio hivyo au
hujawahi kuzaa hujui uchungu? Huyu ni sawa na muuaji hukumu yake ni kifo tu. Je
kama ni mtoto wake alifanyiwa hivyo
angejisikiaje?”
Hali inadhirisha ukosefu wa utu na ubinafsi
ulioenea leo.
Labda tutasema unyanyasaji huu ni wa waovu
wachache tu. Lakini je, watu wazima wenye nafasi zao wanaolala na kuwalawiti watoto kisirisiri?
Hapa Uingereza mwaka mzima sasa tetemeko la
ardhi la habari linaendelea kufichua visa vya watu mashuhuri waliowalawiti au
kuwabaka watoto.
Mosi alikuwa Jimmy Saville. Mstahiwa
alikuwa mtangazaji mashuhuri wa BBC aliyependwa na mamilioni kiasi ambacho
hakuna hata mtu mmoja aliyemkisia mabaya. Jimmy Saville na sigara lake kubwa,
nywele nyeupe zilizofanana na katani, miwani mekundu juu ya pua nene iliyompa sura ya majigambo na vichekesho
alifariki mwaka 2011 akiwa na miaka 84. Baada tu ya mazishi malalamishi na
mashtaka zaidi ya 200 yalifanywa na wanawake na wanaume waliodai aliwafanyia
uanaharamu wakiwa watoto lakini enzi hizo sheria iliziba masikio.
Hawakusadikiwa.
Wengine wanne walidai aliwachezea wakiwa na
miaka kumi. Kutokana na umaarufu wake alipewa ufunguo akaruhusiwa kuingia
mahospitalini kutumbuiza wagonjwa ambao aliwanajisi na kuwafanyia uchafu.
Aliingia vyumba vya vilema na maiti. Karibuni madai yameongeza kusema Bwana
Saville alihusudu kulala pia na maiti. Alifanya vituko hivi toka mwaka 1964 !
Baada ya habari za Jimmy Saville kuzagaa,
watu wengine maarufu wanaendelea kushtakiwa. Wiki jana mwanamuziki na mchoraji aliyetunukiwa taji la heshima na Malkia na
kuitwa Sir Rolf Harris, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano baada ya
kupatikana na hatia 12 za kulala na watoto. Madai yanasema Bwana Harris mwenye
umri wa miaka 84 alianza ufuska wake miaka 40 iliyopita. Tarakilishi au
kompyuta zake zilikutwa na picha zaidi ya 200 za watoto wadogo wakiwa uchi.
Wakati mashtaka yakiendelea serikali
imetangaza mabomu mawili. La kwanza lahusu viongozi serikalini. Mwaka 1983 enzi za uongozi wa marehemu
Margaret Thatcher uchunguzi uliofichua ulawiti na ubakaji wa watoto ndani ya
mashirika makubwa ya hospitali, BBC na serikalini ulizimwa. Aliyepewa mafaili ya uchunguzi Bwana Leon Brittan,
tajiri- mbunge na Waziri enzi hizo- inadaiwa aliyaharibu mafaili ya mashtaka.
Wiki jana serikali iliamuru uchuguzi ufanywe na maofisa saba wa polisi
wameteuliwa kuusimamia.
Bomu la pili ni ukeketaji. Alhamisi Julai 3, Serikali ya Uingereza
iliwaamuru waganga, waalimu na
wafanyakazi wa taasisi za umma
kutotetereka kuzuia ukeketaji eti kwa sababu za kitamaduni. Toka sheria
ilipopitishwa kutokomeza desturi hii
mwaka 1985 hakuna aliyeshtakiwa hadi mwaka huu.
“Ukeketaji ni uhalifu. Si suala la
kikabila bali utesaji. Si jando unyago
bali unyanyasaji.” Kamati husika ya Wizara ya Uhamiaji ilitamka. Baraza la
Waislamu Uingereza nalo lilitoa taarifa iliyopinga vikali ukeketaji na kusema
Uislamu hauafiki kitendo hicho.
Wenzetu wameamua vita kutetea watoto.
Je, sisi Afrika?
Ukeketaji, ubakaji na kulawiti watoto vinaendelea
kisirisiri (na wazi) mijini na vijijini Tanzania.
Sababu kuu ni umaskini na watoto wengi kutokwenda shule. Watoto kulazimika
kulala nje au kuishi maisha ya dhiki. Pili, woga umeenea. Wahusika hawasemwi. Vyombo
husika - vya kidini, kijadi au kiutawala- huficha au kutumia mabavu kuuzima
moto.
Karibuni nimeelezwa kisa kilichotokea
Tanzania. Mzee aliyekuwa na tabia ya kulala na watoto wadogo- wasichana kwa
wavulana- akiwapa peremende na vijisenti alishikwa (kama mwizi) lakini akawahonga
wahusika. Hawakumpeleka polisi. Walimwachia. Swali ni je, wale watoto
aliowadhuru wataendeleaje na vidonda kimwili na kisaikolojia? Tuendelee na mada juma lijalo.
No comments:
Post a Comment