Vitendo viwili
vichafu “vinavyofichwa” na watawala
duniani ni biashara ya dawa za kulevya na unyanyasaji wa watoto. Ingawa vya aibu na ufidhuli vina faida sana kwa
wahusika. Dawa za kulevya ni biashara inayotajirisha haraka kuliko zote.
Ripoti
iliyotolewa na Idara ya Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa
(UNIDOP) mwaka 2011, inasisitiza asilimia
20 ya kipato cha dunia hutokana na
biashara hii ya ki-Ibilis. Ndiyo maana mtu yeyote anapopambana na ujambazi huu
lazima atauawa. Haya yanaonekana Mexico - kilele cha ujambazi wa dawa za
kulevya. Video za mauaji – wakiwepo wanawake na vigoli- wakikatwa katwa kwa mapanga, visu na mashoka zimeselelea
mitandaoni.
Habari za Watanzania waliokamatwa wakibeba
unga au “heroin” ughaibuni sasa zimekuwa nongwa.
Unyanyasaji wa
watoto hauna faida ya kiuchumi ila ni “jaha” kwa wahusika. Hali kadhalika ni rahisi kuwatumia watoto kubeba silaha, mizigo, kuwalawiti nk.
Wiki hizi
mbili zilizopita Uingereza imeshuhudia sokomoko
la wakuu wa nchi walivyofanya kila njia
kuzuia habari za ngono na watoto kutofichuliwa.
Madai yalifanywa na mmoja wa vizito ndani ya serikali ya chama cha Conservative
kati ya 1979 na 1990. Inadaiwa mafaili yaliyotayarishwa na marehemu Geoffrey Dickens mwaka 1983 yaliharibiwa baada ya kufikishwa polisi. Uongozi wa sasa wa Waziri Mkuu, David
Cameroon umethibitisha kuwepo kwa mafaili 746,000, ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani kati ya1979
na 1999. Miongoni ya hayo 114
yaliyoharibiwa, 13 yanahusu uchunguzi wa unyanyasaji wa watoto. Neno
linalosikika ni “paedophilia”- yaani tabia ya mtu mzima kuhusudu mapenzi au
ngono na watoto.
Bado madai
yanaendelea kujadiliwa serikalini. Dai
muhimu lasema viongozi wa ngazi za juu, wakiwepo wanadini na familia ya malkia
walihusika. Aliyekuwa madarakani wakati huo ambaye sasa hivi ni mstahiwa mwenye
hadhi ya “Lord” ...anadaiwa alimbaka mwanafunzi wa miaka 19 mwaka 1967.
Kidesturi
wadhifa wa “Lord” unatokana na umwinyi Uingereza na familia ya wafalme. Leo mtu
yeyote aliyefanya mazito jamiini anaweza kuteuliwa kuwa Lodi. Wanawake huitwa Baroness. Mfano ni Mjamaika,
Baroness Doreen Lawrence ambaye mwanae, Stephen, aliuliwa na wabaguzi wa
Kizungu, London, mwaka 1993. Baroness Lawrence amepigania haki ya mwanae kirefu
hadi kuwapeleka baadhi ya wahusika jela.
Moja ya manufaa ya “Malodi” (neno lililoshaingia
ndani ya msamiati wa Kiswanglish) huruhusiwa kuingia kikao maalum cha Wabunge.
Kikao kina nguvu za kupitisha miswaada na sheria za serikali.
Tuendelee.
Dai la pili la kashfa hii inayoitetemesha
Uingereza- linasema uongozi wa enzi za
marehemu Margaret Thatcher ulijaribu vile vile kubatilisha sheria za kuruhusu
watoto chini ya umri wa miaka 16 kufanya ngono. Wiki jana kamati ya uchunguzi ilitahadharishwa
kutoficha baadhi ya madai ikiwepo jina la askofu maarufu aliyelawiti watoto.
Haya mambo yapo
kila mahali.
Lakini hayasemwi. Kwetu Tanzania- miaka mingi-
tabia ya watu wazima au wenye nafasi
kubwa kulala na watoto imeenea. Chawa ameanza kuonekana karibuni kutokana na mjadala
kuhusu ushoga.
Miaka mitatu
sasa serikali za Kizungu –zikiongozwa na Wamarekani zimetutaka Waafrika
kulegeza sheria za mapenzi ya jinsia moja. Kinyume na namna mahusiano haya
yanavyokuwa nchi zilizoendelea, ushoga, kwetu si utamaduni na wale wanaofanya huwa
wamelazimika.
Mtafiti na
mchunguzi aliyetuma makala ya kurasa
tatu ndani ya moja ya mitandao jamii inayosomwa
na Waswahili. Anadai:
“Sidhani
Marekani inatutaka tukubali ushoga. Ni kunyanyasa na kuonea ndiyo inataka
tuache maana...hawa tunawatengeneza wenyewe kwa kulawiti vitoto... watu wenye
mahitaji tunatumia ngono kama chombo.”
Nakubaliana na
mwandishi. Zamani nikisoma shule za kulala za sekondari ilikuwa kawaida baadhi ya wavulana kufanywa
wanawake kwa nguvu na vijana wakubwa zaidi. Wapo waliopigana na walioshindwa. Walioshindwa waligeuka mashoga.
Mmoja niliyesoma naye Mzumbe mathalan ( vitendo viliitwa “umbuzi”), alikuja
kuwa shoga maarufu.
Si mashuleni
tu. Mtafiti anaendelea kusema “Malezi ya nyumbani –kulaza watoto wadogo wa
kiume na wakubwa wanaonea wadogo kisha wanazoea – kwa asilimia 80. Mlinzi,
dereva wa watoto, mtoto wa kazi za nyumbani analawiti wanao- wewe mwajiri
hujui, dereva humfungi maisha unamfukuza kazi; unapokuja kufahamu mwanao
keshazoea. Humsaki aliyemfanya hivyo. Hausigeli anasaga vitoto au wadogo zake.”
Ni mambo
yanayotokea majumbani, kisirisiri, tunayafahamu; hatuyapingi.
Mwandishi
anaelezea utafiti aliofanya Dar es
Salaam kuhusu ulawiti. Anadai siku hizi
ili kupata ajira, kinachotakiwa si fedha bali ngono: “ Kwa changu doa kipato ni
kikubwa zaidi asipotumia Kondom au akikubali Tigo.Wafanyao haya ni waume za
watu, waheshimiwa, watu wa dini, wenye hela, makampuni, hoteli – wenye vipato.
Wasichana wanahadaiwa, hatimaye
wanaharibika.”
Mbali na ulawiti unaoendelea mitaani,
mashuleni na katika taasisi za kidini (mathalan madrassa) mtafiti anagusia tatizo
la homoni. Homoni au “hormones” kwa Kiingereza ni viini vinavyoendesha mizunguko
na tabia za maumbile. Watu wanaogeuka jinsia zao kutokana na kulawitiwa wakiwa
wadogo au ujanani kihomoni ni wengi Tanzania anadai mchunguzi.
“Zamani wazee
wa mila walikuwa wakiwavunja lakini siku hizi tunawaficha hatuna mila za
kikabila tunazozifuata na kuwasaidia. Hospitali ni gharama. Aibu. Mbona wapo
wanaume wenye viuongo vya kike na kiume na wameoa?”
Madai mazito.
Suluhisho nini?
Vyombo vyetu
vya habari bado havithubutu kujadili. Bado tunajificha katika shuka za mila na
desturi. Wanaoumia ni watoto na watu wazima walioharibiwa vijijini na mijini.
Misaada ijayo
kupitia taasisi na vyama mafichoni haiwafikii, inaliwa na wachache bila kuwapa
huduma ya hospitali na ajira.
Halafu vipi mtu
aliyelawiti au kuharibu watoto anapokamatwa mbona ndugu zake humtolea dhamana
na kumnyanyasa mtoto au kijana aliyebakwa?
Kwanini tunaruhusu hawa watesaji kutembea
majiani huku tukiwanyanyasa walioharibiwa na kugeuzwa mashoga?Viongozi wetu
hasa Wabunge wanapashwa kupitisha sheria
kali kuwatia nguvuni wanaoharibu watoto.
Lakini je serikali yetu iko tayari kufukua handaki na shimo hili la kiza?
Ilichapishwa Mwananchi Jumapili 20 Julai, 2014
No comments:
Post a Comment