Wiki hii, Mheshimiwa Rais J Kikwete, alikuwa Marekani
kufanyiwa matibabu ya tezi ya uume, hospitali ya John Hopkins, Baltimore. Kitakwimu maradhi haya huwafika
asilimia 45 ya wanaume walioshapitisha miaka 60. Ingawa
lengo la makala haya si kuzungumzia hali ya Rais, ni vizuri tukitathimini
tatizo hili linalowasakama wanaume wengi. Miongoni mwa walioshafikwa ni marehem
Nelson Mandela, kiongozi wa Waislamu Marekani, Louis Farahkan, mwanamuziki
maarufu hayati James Brown, mwigizaji mashuhuri wa Hollywood, Robert De Niro, nk.
Miaka michache iliyopita
niliwahi kuandika juu ya afya ya uume ( na uke vile vile) na kuhimiza haja ya
kuelewa namna ya kutunza na kufanya mazoezi kutunza viungo hivi. Kwa wanaume
viungo viwili muhimu husika ni mfuko wa mbegu (korodani) na tezi kibofu. Visipoangaliwa
vyema husababisha saratani ambayo kihisabati, inaua mwanaume mmoja kati ya saba, duniani. Moja ya suluhisho kuu ni kuzifahamu
dalili kabla hazijaota kutu.
Lakini tezi ya uume au
tezi kibofu, ni nini hasa?
Tezi hii ni kidude cha
mviringo, kiwastani, ukubwa wa jicho la mwanadamu. Hukaa chini ya kibofu cha
mkojo. Kazi ya tezi hii ni kutengeneza maji yanayolinda na kurutubisha mbegu
nyeupe za uume. Tezi huanza kuvimba tunapofikisha miaka 50. Mwanaume mwenye
bahati kufikisha miaka 90, anategemewa kufikisha uvimbe uliovuka asilimia 90, kiumbo.
Ni nadra sana kwa kijana chini ya miaka 40 kusakamwa na adha hii. Hata hivyo
leo maradhi ambayo zamani yalikuwa ya watu makamo na wazee yameanza kuwatoboa vijana.
Kwa vipi?
Chukua mfano tezi kibofu. Harufu mbaya toka
mbegu za uume au kuumwa mbegu zikitoka wakati wa ngono, ni dalili. Hapo hapo
tuzingatie kuwa tatizo kubwa zaidi yaani saratani ya tezi kibofu ni nadra sana
kwa wanaume chini ya miaka 60.
Je, huanzaje? Au tuseme matatizo ni yapi?
Yana matawi
mawili. Tezi kuvimba na hatimaye kupungua likitibiwa au kuangaliwa vyema
na mapema au hugeuka saratani. Saratani
ya tezi ya uume, ni tatizo kubwa zaidi
ambalo humbidi mgonjwa kupasuliwa . Upasuaji unapofanywa kuondoa tezi hii mtu
hufikwa na tatizo la kushindwa kuzuia haja ndogo au kubwa (“incontinence”), kupungukiwa kabisa
nguvu za uume, nk. Watu mashuhuri waliozungumzia kwa uwazi ni pamoja na marehemu mwanamuziki
nguli, James Brown na Nelson Mandela.
Dalili za kuvimba zinazoanza
kuonekana ni njia ya mkojo kuwa nyembamba na kuzuia mtiririko wa haja ndogo.
Mtiririko huwa mdogo au wa kubabia babia, wa matone matone. Pili, huhisi mkojo,
haukutoka wote. Matokeo yabidi kwenda
chooni mara kwa mara hasa usiku. Yabidi kukimbia shauri musuli ya uume imelegea
na huwezi kujizuia. Tatizo hili lipo pia kwa wanawake. Miaka michache
nilizungumzia haja yetu sote kufanya mazoezi kukomaza musuli yake. Subiri.
Je, mganga atathibishaje
tatizo?
Ni muhimu sana kuwahi
kujua dalili. Lakini wanaume wengi (hasa sisi weusi) hatupendi kutazamwa. Huona
aibu kuhisi tumedhalilishwa kama madume. Kwanini? Kuna njia mbili, za uchunguzi.
Ya kwanza (inayotubughudhi zaidi) ni mganga kuingiza kidole (chenye glovu)
kwenye tundu la makalio kupima ukubwa wa tezi. Njia hii ina ugunduzi wa haraka
na hakika zaidi. Ya pili, ni kupimwa damu na mkojo kutathmini figo zikoje.
Maana tatizo la tezi kibofu huathiri figo na mtiririko mzima wa maji mwilini.
Waganga wanasisitiza
ikiwa umeshaathirika usinywe maji saa mbili au tatu kabla ya kutoka nje au
kwenda kulala. Ukienda kujisaidia jaribu kurudi tena punde kuhakikisha mkojo
wote umekwisha.
Jaribu kutulia kwa
kufanya mazoezi ya pumzi wakati wa kujisaidia. Epuka sigara na vinywaji vyenye
“cafeine” katika kahawa, chai na
Cocacola. Juu kabisa fanya mazoezi kukomaza musuli iliyo kati ya mlango wa haja
kubwa na uume (uke). Musuli unaitwa PC (“pubococcygeus”
) , kitaalamu. Mazoezi haya ni muhimu
kujenga ustahimilivu kwa wanawake na wanaume. Unakaza na kukamua kamua musuli
mara kadhaa kila siku.
Tukiendelea zaidi katika
suala la ulaji. Tafiti za karibuni zimeelemisha kuwa ulaji wa nyama choma au vyakula vyenye
masizi huchangia saratani ya tezi.
Tuangalie zaidi tatizo la
kuchoma nyama.
Utafiti uliofanywa
Marekani mwaka 2013, ulifikia hitimisho la ngazi tatu. Mosi kwamba ulaji wa
nyama nyekundu iliyookwa sana katika moto wa mkaa au moto mkali huchangia viini
vya saratani (“carcinogens”). Pili, mvuke, joto na masizi yaliyoko katika moto
unaozichoma nyama huwa na vimule mule vinavyoingia mwilini , kuathiri maendeleo ya maumbile takikana (DNA)
na kuchangia kuanza kwa saratani.
Tatu, kuna viini vinavyoitwa “heterocyclic
amines” (HCA) ambavyo hutokana na nyama kupashwa moto kwa nguvu. HCA hupenya
mwilini kupitia utumbo mkubwa na kusababisha saratani mbalimbali kama ya utumbo mkubwa, matiti ya wanawake nk.
Utafiti umethibitisha HCA zipo zaidi katika nyama nyekundu za ng’ombe, nguruwe
na kondoo zilizochomwa. Hapa utafiti unasisitiza kula nyama choma hakusababishi
saratani. Ila nyama zinazochomwa katika mahoteli au haraka haraka nje kwa moto
mkali hadi zikaungua , hadi kuwa na masizi masizi, ndizo hatari. Jaribu kuzingatia hilo ewe
msomaji mpenda nyama choma.
Tatizo jingine la ulaji
ni vyakula vyenye mafuta mafuta,pombe kuzidi kiasi na kutofanya mazoezi ya
viungo.
Kuna dawa na vyakula
vinavyosaidia afya ya tezi kibofu.
Dawa za waganga
hospitalini zinaitwa “blocker”
(mzuiaji). Huzuia ukubwa na kuupunguza. Kisayansi ni “Alpha-blocker”....alpha
ni neno lenye asili ya Kigiriki linaloimanisha mwanzo. Alpha na Omega. Mwanzo
na mwisho. Kazi ya Alpha Blocker ni kuzuia homoni ya kiume (“testestorone”)
inayobadili hali mwilini kuwa “dyhrotestorone”...yaani athari mbaya.
Pili ni miti shamba na
vyakula. Wamerakani wanayo “Saw Palmeto” mathalan. Inauzwa maduka yote ya afya
nchi zilizoendelea. Vyakula kama nyanya, upupu, maparachichi, mboga ya kitimiri
(“Parsley”) na mboga nyingine za majani (saladi mbichi). Karibuni, nyanya
imesifiwa sana kwa afya ya tezi ya uume.
Matunda, vile vile, kwa
wingi na kulala muda unaotakiwa (saa 8 kwa watu wazima) ni baadhi ya mambo asilia yanayoweza kuhudumu
afya. La mwisho.
Muhimu kwenda kukaguliwa na mganga kila mwaka
ukishafikisha miaka 50.
-London, 11 Novemba
, 2014
-Bpepe: gmacha52@gmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com
No comments:
Post a Comment