Babu wa fasihi ya Kiswahili, Shaaban Robert alifariki
mwezi huu mwaka 1962. Ingetakiwa sikukuu
ya kifo chake yaani Juni 20 ifanyiwe maadhimisho kila mwaka. Sisi na
wenzangu wa bendi ya Sayari tuliwahi kusheherekea kwa maonyesho ya 1983. Hazina
hii tukufu ya taifa inatakiwa zaidi ya hilo.
Moja ya vitabu
vyake babu ni “Kielezo cha Fasili” (kilitolewa
upya na mwongozi wa wachapishaji Tanzania; “Mkuki na Nyota” ,2004) kinafafanua mashairi
yake kwa wasomaji mintaarafu ya kujenga
mapafu kilugha.
Ananyambua Shairi
la “Jina”: “Mwanadamu mwenye fikra njema huacha fahari au sifa kwa watu ambayo
vizazi vyake vya nyuma yake hupenda kuiona, na ambayo itakuwa kama hazina kwa
watu wote katika dunia.”
Albert Mangwea hakua Shaaban Robert; kafa akiwa na miaka 31 tu. Lakini Mangwea au Mangair alitumia fani ya ushairi
kuchangia kuiendeleza fasihi ya Kiswahili na kipaji chake alichomegewa na Muumba.
Kifo hiki
kilichokua Usauzi (Afrika Kusini) kimeongelewa na kinaendelea kuongelewa. Mwaka
jana wakati huu Tanzania ilimpoteza Steve Kanumba. Vifo vya chipukizi hawa vimeacha
utata na mijadala marefu.
Mangwea alifia
ughaibuni. Maisha ugenini ni magumu
maana habari huwa hazitangazwi sana. Mbali na taratibu za kisheria na itikeli,
kinachongojewa kutufariji huwa viongozi wa dini na serikali.
Vipo vifo vya aina nyingi. Ila vifo vinapokua na utata husubiri mkono wa
sheria utubembeleze. Kanumba alifuatiliwa na mashtaka ya bibi aliyekua naye;
Mangwea, hatuyajui bado kiuhakika...
Miaka iliyopita habari za vifo vya Waafrika hasa zile
zilizohusiana na UKIMWI au dawa za kulevya hazikuwekwa wazi, shauri ya aibu,
miiko na staha. Nakumbuka wanamuziki wawili maarufu Hukwe Zawose na mpwake,
Charles Zawose walipofariki, wanahabari hatukueleza chanzo ili kuheshimu hisia
za familia zao.
Magazeti ya
ughaibuni , walakin, hayakupepesa.
Mwanamuziki
Charles Zawose alifariki ghafla akijitayarisha kupanda ndege Sweden alikokua
akifanya maonesho ya muziki wa kijadi, 2004. Kwa kuwa Charles na babake mkubwa
walishajenga sana majina ugenini habari
zilichambuliwa katika magazeti viongozi. Mwandishi John Lusk wa “Independent”
( linaloheshimika sana Uingereza) :
“Kifo
kimenyamazisha moja ya himaya kubwa sana ya familia ya wanamuziki wa
Tanzania... Walikuwa mabalozi viongozi wa muziki wa Kigogo.” Akaongeza kuwa
Zawose kafariki kutokana na “maradhi
yaliyosababishwa na UKIMWI.”
Nyumbani, lakini, ugonjwa
haukutajwa.
Inasemekana Mangwea alikua mtumiaji mkubwa wa dawa za
kulevya. Majadiliano yaliyoendelea juma lililopita ni iwapo aliwekewa sumu,
dawa feki zilizokwisha muda wake, nk. Baya lolote lililofuatia matumizi hayo
basi haliwezi kuacha kuleta utata na hatimaye malumbano mazito. Muhimu sana ni
mafunzo tunayobakiwa nayo.
Si ajabu kwa
wasanii kufariki kutokana na dawa hizi. Huku ughaibuni ni mkasa uliozoeleka tangu
zamani. Miaka miwili iliyopita mwimbaji Amy Winehouse alinyauka –akiwa na umri
mdogo wa miaka 27-baada ya muda mrefu kujiharibu na ulevi huu wa Kishetani na Kiza.
Alikutwa peke yake nyumbani ameshakauka
kutokana na pombe nyingi kuzidi; lakini ni karibuni tu ndipo maelezo rasmi ya
sababu za kifo, yametolewa rasmi.
Mpiga gitaa stadi kuzidi
wote katika historia, Mmarekani mweusi, Jimi
Hendrix vile vile, aliaga dunia jijini London akiwa na miaka 27 mwaka 1970. Hendrix
alitumia sana dawa hizi za ki-fisi, hususan unga wa “cocaine “ na vidonge vya
kusisimsha. Usiku wa kuamkia asubuhi aliyofariki alikunywa vidonge tisa vya Vesperax- badala ya kimoja
(ilivyotakiwa ) kusudi eti apate usingizi. Tisa!
Bibi wa Kijerumani aliyekuwa naye, Monica Dannemann(
aliyekuja akuandika kitabu kuhusu maisha yake na Hendrix) alijiua 1996 akiwa na
miaka 50. Moja ya sababu za kujiua ni wanahabari na wanawake wengine kumghasi
muda mrefu kwa kutoamini maneno aliyosema. Monika (kama dada aliyekutwa na marehem
Kanumba) ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na kamanda huyu wa magitaa.
Vifo hivi viwili vi mfano wa namna wasanii wanaotumia
vilevi kuzidi- hata nchi zilizoendelea -wanavyosababisha
utata wakishafariki.
Somo kwetu nini?
Kutangaza habari za vifo kama hivi ni fundisho kwa jamii nzima. Fikra iliyoenea kwamba msanii
lazima ule dawa, bangi au pombe sana
ndiyo utunge ni potofu, maana kuna wasanii kibao (tena wakali) wanaotunga bila “madude”
hayo- na wangali hai.
Jambo la pili ni kujua unapokwenda na unachokifanya.
Kama kweli marehemu Ngwea alipewa dawa “feki” au zenye sumu je alichanganyikana na watu
gani?
Ughaibuni ni msitu wenye miiba na chemchemi safi pamoja. Vijana wengi wanapokuja huku,
huwa hawajafanya utafiti tosha, na hata
wakiufanya huwa wa juu juu. Leo
makampuni yanatakiwa na serikali mbalimbali kueleza wazi wazi bidhaa zimetengenezwa
lini na wakati wake utaisha lini. Niliwahi kuwa na wageni wenzangu wa Kibongo
na nilipowakatia mkate nikagundua tarehe yake ilishapita kwa siku tatu. Ingawa
ule mkate haukua na dosari ukiutazama, nilikua tayari kuutupa jaani.
“Hapana hapana ; tutaula tu” wakasema.
Nikasisitiza usiliwe.
“Ah wacha tu tutakula. Kutupa chakula vibaya.”
Kweli, kutupa chakula si vizuri. Lakini desturi za nchi
zilizoendelea ni kutokula vyakula vilivyopita wakati. Hii ni sababu bidhaa
huwekewa dawa zinazozifanya zisioze; hivyo ukizila zaweza kukudhuru. Kwa
Kiingereza neno linalotumika ni “preservatives.” Preservatives hutumikwa katika
vyakula ( au vinywaji) ndani ya mikebe,
vyupa , plastiki, nk. Kutokana na Waafrika
wengi kutoelewa hilo, wafanyabiashara mafisadi wa nchi tajiri (leo) wana tabia
ya kutuma bidhaa hizi kwetu maana wanafahamu hatujali au hatujui. Tunapodhurika
au kufa tunasema Ah kazi ya Mungu.
Kazi ya Mungu haiendi hivyo.
Na serikali zetu, je?
Mwaka 1994 kijana wa Kitanzania aliuawa Italia. Huyu kaka alijihusisha na
biashara ya dawa za ki-Ibilis. Mambo
yalikaa kimya kimya, hadi leo habari zake hazisemwi. Uongo hapana; makosa
yalikua yake. Utamaduni wa biashara hii ni kwamba mkiudhiana, usipolipa au
ukiwasaliti wale unaojihusha nao – ambao huwa majambazi katili- wanakutosa.
Lakini la ajabu serikali zetu ughaibuni huchelea
kujihusisha na watu hawa. Ndugu za mhusika hupewa mwili, mambo (kimya kimya)
yakaishia chini ya mkeka. Wenzetu waliondelea hutuma maofisa serikali na kutangaza habari runingani kusudi liwe funzo
kwa jamii na taifa.
Tumalizie mada hii muhimu juma lijalo.
No comments:
Post a Comment