Kwanza kabla ya kuendelea na (kumalizia) mada tuliyoianza
wiki jana, tuwape pole ndugu wa familia
yake Albert Mangwea. Tuwape pia pole marafiki zake na wote waliomjua kwa
karibu. Tuwaombe radhi kwa kuendelea kuzungumzia jambo ambalo linawakumbusha
uchungu wa mtu aliyekwisha zikwa.
Pamoja na hayo tujikumbushe madhumuni ya kuandika na
kuzungumzia suala hili.
Kwanza kabisa kupoteza vijana wanaoanza maisha katika
hali hizi mbaya si jambo zuri. Wapo wengi wanaondelea kuzungumzia kwamba ni
Mungu kaamua na kwamba kifo ni asili maisha. Hatukatai hilo. Ila kwetu Tanzania
imekua sasa desturi kukubali vifo na utamaduni wa kufa mapema. Wanapoendelea kufariki vijana tunakubali ni
maajaliwa. Zikitokea ajali za magari (zinazouzilika) zilizotokana na
uzembe wa madereva pia tunalitaja jina
la Mungu. Mungu amekuwa sasa ndiye mwamba wa kila baya. Kageuka kisingizio.
Kwanini sisi tu ndiyo kitakwimu tuna vifo vingi zaidi tena vya watu wenye umri
mdogo?
Lakini kabla ya kuendelea zaidi, tukubaliane ...
Kitakwimu duniani, kila dakika hufa watu mia moja. Ina
maana baada ya wewe msomaji kumaliza kusoma makala hii(ikiwa utachukua dakika
kumi kufikia mwisho) wanadamu 1,000 watakua wamemaliza maisha yao. Takwimu za
sensa duniani zinatujuza vile vile, kila mwaka tunapoteza watu 56 milioni. Hii
ni takribani idadi ya Watanzania wote. Kila mwaka! Hapo hapo ni vyema
kujikumbusha kila sekunde huzaliwa watoto saba duniani. Kila sekunde dunia
inatema na kumeza. Siri ya maisha ni mzunguko mzima wa sayari na muda.
Wanadamu lakini tuna wajibu na majukumu. Ulimwengu tuliokuta
umetengenezwa na kuchangiwa na kila
aliyepita , aliyekuwepo na atakayekuja. Ndiyo maana unapoanza kuwa mtu mzima shurti ujue la kufanya kuchangia. Siri yake ni
nidhamu na kujituma.
Lawama tunazozitupa kwa Mwenyezi Mungu kila siku
zinachangia kujidunisha. Miaka mia moja
iliyopita, magari, simu na tarakilishi (au kompyuta) vilikua ndoto za Abunawasi.
Nakumbuka mwaka 1990 nilisoma gazeti la Kimarekani
(Newsweek) likasema baada ya miaka ishirini itakua kawaida kwa watu kutembea na
simu mkononi. Sikuweza kubashiri. Leo simu za mkononi ni jambo la kawaida kama
yalivyo magari na runinga. Miaka mia
moja ijayo vitakuwepo vitu vipya zaidi.Yote yamefanywa na wanadamu wenye mikono
miwili na miguu miwili kama wewe na mimi. Swali.
Je, mchango wako utakua nini?
Vijana wanaofariki mapema baada ya kuonja maisha mazuri
ya kazi waliyoipigania wanajisahau.
Unapopambana na
maisha magumu (katika fani yeyote) kisha ukafanikiwa, lazima ujikumbushe
unakotoka. Sisi Waafrika tuna mengi ya kujenga.
Mwaka 1965 mwimbaji Salum Abdallah aliyekuwa mfanya
biashara wa kujitegema alifariki kabla hajavuna matunda ya kazi zake. Salum
Abdallah kama alivyokuja kuwa mwanamuziki mwenzake Mbarakah Mwinshehe
walitafuta studio za kurekodi nyimbo zao Kenya. Kifo cha Mwinshehe kilikua
kibaya zaidi shauri baada ya ajali ya gari (mwaka 1978) alikosa damu shauri damu
huuzwa Kenya, na hakua na fedha. Alikua Kenya akitafuta pia studio.
Wengine walioishia ughaibuni bila mafanikio ni Patrick
Balisidja na Kassim Magati (aliyefariki Botswana 1994). Hii ni mifano michache
ya wanamuziki waliohangaika maisha yao yote bila kheri. Leo vijana wengi wa
Bongo Flava wana maisha mazuri kuliko wajomba na babu zao hao waliopita. Baadhi
ni milionea, wapo waliojenga hoteli. Maisha haya “mazuri” kiwastani ni kipimo
kizuri cha maendeleo ya msanii na mfanyakazi wa sanaa za maonyesho Tanzania.
Lakini mwisho wake uweje? Msanii na mfanyakazi yeyote aliyefanikiwa anatakiwa
asisahau alikotoka na ajikumbushe wajibu kwake na jamii yake.
Wajibu kwa jamii maana yako ni nini?
Zamani enzi za TANU tuliambiwa maadui makubwa ni ujinga,
umaskini na maradhi. Ukiwa maskini elimu inaweza kukukomboa. Ndiyo maana wazazi
wengi huwakazania watoto wasome.
Zaidi ya asilimia
80 ya Watanzania hawajasoma zaidi ya shule ya msingi. Kwa Mwafrika leo elimu ni
chombo cha ukombozi. Mtu unapofaulu kupitia njia nyingine zisizo za elimu
(mathalan usanii au biashara) unaweza kutumia ahueni hiyo kuwasaidia wenzako.
Ndiyo maana nidhamu na kuitambua faida ya mafanikio yako ni jambo muafaka.
Utumiaji wa dawa za kulevya, pombe nk kwa wingi ni moja ya mifano michache ya
ukosefu wa nidhamu. Ndiyo dawa hizi ni sehemu za maisha ya wasanii hasa
wanamuziki. Lakini hatima yake ni nini?
Je, kwanini sasa hivi pameanza kuenea tabia, utamaduni na
desturi ya kutojituma na ubinafsi wa kifuska kuzidi ?
Je tabia hizi zinatokea wapi?
Mbali na kujituma, je asasi za serikali zetu hufanya nini
yanapotokea mauaji ya wananchi?
Wiki iliyopita tulitazama kidogo mauaji ya kijana
aliyeuawa nchini Italia kutokana na biashara Ibilis ya uuzaji wa dawa
zakulevya. Mfano huu unaweza kuwekwa kando kwa vile kijana huyo alijihusisha na
biashara mbovu na haram. Tunaweza kusema mwanadamu huvuna ulichopanda. Mungu
amrehemu.
Lakini je, mwanamke aliyefanya kazi ya kuuza mwili wake
(ukahaba) akapigwa hadi alipofariki?
Mwaka 2004 askari
wawili wa Kiingereza waliokua
matembezini Tanzania baada ya kuwa vitani Iraki, Nigel David (miaka 23) na
Brett Richard (20) walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka na kumuua mwanamke wa
Kitanzania , Conjesta Ulikaye Novemba 2004. Kufuatana na habari za magazeti
mauaji yalitokea hoteli ya Silver Sands,
Dar es Salaam na kesi ikashughulikiwa kwa siku 36 tu baadaye askari
wakaachiliwa huru “kutokana na kukosa ushahidi.”
Linganisha kesi na habari zinazotokea kuhusu wahalifu wa
Kitanzania. Ingekuwa Mtanzania asingenyongwa? Au linganisha kesi kama hii
ughaibuni. Ukiua Uarabuni au nchi nyingine za Mashariki za Mbali, huwezi
kuachiwa tu hivi hivi. Linganisha na kesi zinazohusu Wazungu. Mara nyingi sana
wenzetu wanaposhtakiwa kwa makosa mbalimbali serikali zao hazikai kimya. Miezi
miwili iliyopita mama wa Kizungu (miaka
56) alishikwa na dawa za kulevya (thamani yake Dola milioni 2.4), Indonesia.
Alipohukumiwa kunyongwa, serikali ya Uingereza ilipiga sana kelele. Hadi sasa hajanyongwa.
Serikali za wenzetu hujaribu hutetea wananchi wao. Lakini familia ya
marehemu Conjesta Ulikaye ina zuri gani
la kusema kuhusu binti yao aliyeuawa kinyama vile na waliomtosa kuachiwa? Je,
tunawatendea haki wananchi wetu kweli?
Ikiwa wananchi wanahisi hawatendewi haki je, wataiga wapi nidhamu?
Ilichapwa pia Mwananchi Jumapili
unajua Freddy,Roma haikujengwa kwa siku moja. Mafanikio hayaji kwa "over night". Watanzania hatujui hili na itatusa sana
ReplyDelete