Wakati n’naishi Brazili miaka 20 iliyopita moja ya woga
mkubwa ulioenea ni hatari ya watoto wadogo mijini. Hatari gani?
Sikiliza ...
Siku moja Jumapili n’natembea ufukwe maarufu wa Copacabana jijini Rio De Janeiro. Hapa pana eneo kubwa
sana la kuogelea, wanawake warembo, majumba ya starehe, migahawa, magari,
minazi na starehe za kuotea tu paukwa pakawa. Jaribu kulinganisha ufukwe huu na
Coco Beach , Dar es Salaam. Anzia pale kilima kinachoelekea barabara ya Chake
Chake ongoza hadi Kivukoni penye wauza samaki na boti linalovusha watu. Sema
badala ya hospitali ya Ocean Road na Ikulu sasa weka majumba hayo
niliyozungumzia ya starehe na sehemu ndefu sana maridadi za kufanya mazoezi na kuogelea.
Watalii walipahusudu. Na hii si yote- ufukwe wa Copacabana umeunganika na Ipanema na Leblon, bichi nyingine mashuhuri za
jiji. Wabrazili husema Mwenyezi Mungu aliuumba ulimwengu mzima kwa siku sita,
ile ya saba akakaa kitako akikamilisha Rio De Janeiro peke yake. Nilikua na
tabia ya kwenda kuogelea na kufanya
mazoezi pale mara mbili tatu kwa juma.
Jumapili hii
nilipomaliza mazoezi na mwanangu tukaelekea
kibanda cha madafu. Muuza madafu akatutengenezea mawili- tukasimama pembeni na mrija
tunafaidi maji ya bahari Atlantic.
Ghafla kundi la
watoto kama sita saba hivi, hilo. Kisa nini ? Wamemwona mtoto mwenzao. Wastani
wao miaka sita, saba, minane. Hawa watoto lakini hawakua wa kawaida. Ni watoto yatima
wanalala na kuishi mitaroni na vijiweni; wametupwa au hawana wazazi, wametoroka
majumbani, hawana pa kwenda.
Kwa kuwa nilishakaa kipindi jijini nilijua lengo la wale vifaranga nini.
Haraka haraka kabla mambo hayajageuka kokoto- maana mwanangu alikua akianza
kuwayowayoka- nikawanunulia madafu. Wakanywa.
Sasa umefika wakati wa kuondoa kile wala madafu
tunachokiita “nyama” yaani nazi changa ambayo huwa tamu na madini tosha.
Mchonga madafu keshatutayarishia, sasa tunayala na kijiti kile kile kilicho
sehemu ya mnazi. Kwa mla madafu ada na desturi.
Punde, hilooo... kundi la watalii. Watalii wabichi-
ukiwachunguza wanavyotembea, bwede bwede
bwe, hawajakaa sana mjini. Mosi hawaijui lugha- maana ikiwa huongei Kireno
hapa Brazili- umejichongea, ni sawa na kutojua Kiswahili kwetu Afrika Mashariki.
Watoto walipowasikia wale “Gringos” (wageni wanavyoitwa) wakiongea Kispanyola
cha kubabaisha na Kiingereza, wakawaparamia.
Mtoto wa kwanza - miaka saba hivi- mtemi, ndiyo kiongozi.
Kaanza kwa Kireno: “Tunaomba madafu ba’ mkubwa!”
Mtalii kamwangalia mtoto, kisha wenzake, inavyoelekea neno lililotambulika
moja tu: “agua de coco”( madafu).
Mtalii akamjuza mwenzie Kiingereza : “Hawa si wale watoto wa
siku ile?”
“Ndiyo hawa hawa ...” akahakikishiwa.
“Pesa imekwisha.” Akasema mtalii kiongozi.
“Pesa imekwisha?” mtoto kiongozi miaka saba akajibu; midomo imefyodolewa, anawakagua
wageni utosini hadi miguu iliyovalia kandambili za bichi; kinda wa mitaroni,
hata panya hamthubutu. Sasa nimeshajua nini kitafuata; nikampa ishara mwanangu.
Tukaondoka tukasimama kama mita hamsini
pembeni, tukimalizia “nyama.”
Mungu akikupa kilema hukupa na mwendo.
Kiongozi yule wa miaka saba kaingiza mkono tumboni chini
ya fulana yake chafu (tumboni!), akachomoa bastola. Akawaelekeza watalii. Madafu yamesahauliwa; vifaranga wamewazunguka, wanadai dhahabu. Muuza madafu
tu ndiye kabaki akitafadhalisha kwa Kireno:
“Tulizeni mambo vijana” (hakusema watoto, ila vijana!
Mguu wa kuku ni Ustaadh).
Watalii wamenywea utadhani mbunge maarufu aliyefumaniwa.
Mifuko imefunguliwa, fedha zimetolewa, watoto haoooo... wakatoweka na chao.
Haukupita muda lakini wakatiwa mbaroni.
Enzi nikiishi Brazili
ilikuwa kawaida kusikia watoto wa aina ile wameuawa na polisi.
Julai 1993, watoto
wanane waliuawa na watu ambao baada ya uchunguzi kufanywa – walikisiwa kuwa maaskari, mjini Rio. Moja ya
utetezi walioufanya ni kusema eti wanasaidia kufagia (kusafisha) mji kutokana
na adha ya watoto wanaohalifu na kuchafua jiji. Wastani wa watoto waliofyekwa ulikua miaka 11
na 14. Katika taarifa ya polisi na mahakama baadaye, baadhi ya walionusurika walisema asubuhi hiyo (ya
mauaji) walikuwa nje ya kanisa la kikatoliki liitwalo Candelaria. Gari la polisi liliwapita na mmoja wao akawapigia
kelele: “Msijali tutawakomoa siku moja!”
Kati ya walionusurika-
Sandro do Nascimento- alikuja kuwa maarufu sana alipoteka nyara basi
kitongoji cha Rio kiitwacho Jardim
Botanico mwaka 2000. Tukio lilisababisha
kiwewe na kutangazwa runingani siku nzima. Leo unaweza kulitazama katika
sinema: Bus 174, ambayo toka itolewe 2002 imeshinda tuzo 23 duniani. Sinema hii
muhimu inatathmini hali halisi ya watoto
wa maskini, yatima na hatima zao.
Kwanini nimeeleza kisa?
Wakati nikiwa Brazil,
watoto waliua na kuuliwa; waliogopwa na kuchukiwa – kielelezo cha jamii iliyochechemea.
Madhila ya Brazil
yametokana na ukosefu wa elimu hasa kwa hohehahe na yameenea nchi zinazoendelea.
Sinema nyingi karibuni zimeonyesha namna
watoto hugeuzwa askari jeshi Uganda, Sierra Leone na Liberia. Ingawa
bado hatujafikia kiwango hicho taratibu hali ina dalili za kidonda, Tanzania.
Karibuni matukio mawili muafaka yameongelewa sana
mtandaoni. La kwanza ni mabanda ya kuonyesha video mijini. Malalamishi yaliyoenea ni kwamba
ingawa vimepigwa marufuku na serikali-
bado utawakuta watoto wa shule wakiingia vibandani usiku kutazama filamu za ngono, ambazo si za
umri wao. Matokeo, anaandika mwananchi mmoja, kuna kesi nyingi za watoto
wadogo kuwaingilia ( kuwabaka) wenzao kimwili.
Mwananchi anacholalamika ni serikali na chama tawala kutotekeleza tamko
la kupiga marufuku vibanda husika. Kaiita mada na ombi lake : “Udhaifu wa
serikali na mmomonyoko wa maadili mitaani.”
N’nakumbuka mwaka mmoja uliopita nilipotembelea nyumbani
nilikua katika basi Dodoma kuelekea Arusha nikashuhudia sinema ambazo zilikuwa
na mwelekeo wa watu wazima zikionyeshwa ilhali ndani ya basi walijazana watoto.
Tukio la pili ni watoto wetu wanaoishi mpakani Kenya na
Tanzania kutoroka mashuleni kufanya kazi za kuajiriwa na kuuza bidhaa Kenya.
Hii ni kutokana na kile mwandishi alichokiita “kufanya vizuri kwa thamani ya
fedha ya Kenya kuliko ya Tanzania.”
Iko mifano mingi; lakini hii miwili ni inadhihirisha maadili na maisha ya wanafunzi wetu kudhoofika. Hatujaongelea kutofaulu mitihani.
Dalili za mvua ni mawingu. Kwa sasa haya ni madogo , lakini tusipozima moto unaoanza
kuunguza maadili, watoto wetu kushika bunduki halitakua jambo la ajabu siku
za usoni.
Ilitoka pia Mwananchi Jumapili
No comments:
Post a Comment