Babu wa fasihi ya Kiswahili, Shaaban Robert alifariki
mwezi huu mwaka 1962. Ingetakiwa sikukuu
ya kifo chake yaani Juni 20 ifanyiwe maadhimisho kila mwaka. Sisi na
wenzangu wa bendi ya Sayari tuliwahi kusheherekea kwa maonyesho ya 1983. Hazina
hii tukufu ya taifa inatakiwa zaidi ya hilo.
Moja ya vitabu
vyake babu ni “Kielezo cha Fasili” (kilitolewa
upya na mwongozi wa wachapishaji Tanzania; “Mkuki na Nyota” ,2004) kinafafanua mashairi
yake kwa wasomaji mintaarafu ya kujenga
mapafu kilugha.
Ananyambua Shairi
la “Jina”: “Mwanadamu mwenye fikra njema huacha fahari au sifa kwa watu ambayo
vizazi vyake vya nyuma yake hupenda kuiona, na ambayo itakuwa kama hazina kwa
watu wote katika dunia.”
Albert Mangwea hakua Shaaban Robert; kafa akiwa na miaka 31 tu. Lakini Mangwea au Mangair alitumia fani ya ushairi
kuchangia kuiendeleza fasihi ya Kiswahili na kipaji chake alichomegewa na Muumba.
Kifo hiki
kilichokua Usauzi (Afrika Kusini) kimeongelewa na kinaendelea kuongelewa. Mwaka
jana wakati huu Tanzania ilimpoteza Steve Kanumba. Vifo vya chipukizi hawa vimeacha
utata na mijadala marefu.
Mangwea alifia
ughaibuni. Maisha ugenini ni magumu
maana habari huwa hazitangazwi sana. Mbali na taratibu za kisheria na itikeli,
kinachongojewa kutufariji huwa viongozi wa dini na serikali.