Mwandishi nikiwa na mtunzi mashuhuri hayati Gil Scott Heron (kushoto), baada ya onesho lake Jazz Cafe, London. Scott- Heron alifariki akiwa na umri wa 63, mwaka 2011. Picha ya A. Macha , 1999.
Nilikuwa naongea na rafiki
yangu mhadhiri; Dk Ikaweba Bunting, anafundisha Marekani...
Tulisononeka kifo cha mshairi maarufu wa
mahadhi ya Jazz, marehemu Gil Scott Heron. Bw Scott Heron alikuwa na ujumbe
mzito uliotetea maslahi ya wananchi weusi wa Marekani na kuzungumzia matatizo
kadhaa ya jamii hiyo ukiwemo utumiaji dawa za kulevya. Alipiga piano na
kuandika riwaya na mashairi matamu na makali sana. Ukitaka mfano mzuri hebu
tafuta “Pieces of a Man” katika You Tube. Sikiliza sauti yake mshairi
anayesemwa kuwa ni baba wa watenzi wa
Rapu na Ushairi wenye ujumbe. Fuatilia piano iliyotulia na mdundo wa Blues na Jazz. Kama unahusudu lugha, zingatia namna Kiingereza kinavyotumiwa
kumchora na kumhakiki mhusika anayeimbwa.
Hayati Gil Scott Heron aliandika riwaya na kufundisha fasihi. Anaomboleza maisha ya mtu huyu aliyeanza na
bangi huishia jehanam. Baadaye jamaa
anateketea kabisa.
“I saw him go to pieces.
He was always such a good, good man.”
(Nilimtazama akivunjika
vipande vipande
Alikuwa mtu mzuri sana...)
