Mwandishi nikiwa na mtunzi mashuhuri hayati Gil Scott Heron (kushoto), baada ya onesho lake Jazz Cafe, London. Scott- Heron alifariki akiwa na umri wa 63, mwaka 2011. Picha ya A. Macha , 1999.
Nilikuwa naongea na rafiki
yangu mhadhiri; Dk Ikaweba Bunting, anafundisha Marekani...
Tulisononeka kifo cha mshairi maarufu wa
mahadhi ya Jazz, marehemu Gil Scott Heron. Bw Scott Heron alikuwa na ujumbe
mzito uliotetea maslahi ya wananchi weusi wa Marekani na kuzungumzia matatizo
kadhaa ya jamii hiyo ukiwemo utumiaji dawa za kulevya. Alipiga piano na
kuandika riwaya na mashairi matamu na makali sana. Ukitaka mfano mzuri hebu
tafuta “Pieces of a Man” katika You Tube. Sikiliza sauti yake mshairi
anayesemwa kuwa ni baba wa watenzi wa
Rapu na Ushairi wenye ujumbe. Fuatilia piano iliyotulia na mdundo wa Blues na Jazz. Kama unahusudu lugha, zingatia namna Kiingereza kinavyotumiwa
kumchora na kumhakiki mhusika anayeimbwa.
Hayati Gil Scott Heron aliandika riwaya na kufundisha fasihi. Anaomboleza maisha ya mtu huyu aliyeanza na
bangi huishia jehanam. Baadaye jamaa
anateketea kabisa.
“I saw him go to pieces.
He was always such a good, good man.”
(Nilimtazama akivunjika
vipande vipande
Alikuwa mtu mzuri sana...)
Niliwahi kumhoji marehemu
Gil Scott Heron mara mbili. Kila
nilipokuwa naye nilijifunza mengi kuhusu utunzi, fasihi, wajibu wa raia kwa
jamii zao na mapenzi ya maisha. Kama mwanamuziki nilikumbushwa uzuri wa kutumia
ala na vyombo kuelezea kadhia. Sasa tuliposikia Bw Heron kafariki akiwa na umri
mbichi wa miaka 62, mwaka 2011, tuliduwaa.
“Kwanini watu weusi , hasa
wanaume tunafariki umri huu?”
Hukwe Zawose , nguli wa
muziki wa jadi toka Tanzania alifariki na miaka 63, Desemba 2003. Hadi leo ukilitaja jina la
Zawose huku Majuu waliomjua, wakiwemo wasanii wa Kiafrika, wasanii na wananchi
wa Kizungu hutingisha vichwa.
Mara yangu ya mwisho kukutana na Zawose
ilikuwa hapa London alipokuja na mpwa wake, (pia marehemu), Charles Zawose
mwaka 1996. Hukwe alitumbuiza na Salif Kaita , albino na mwanamuziki maarufu wa
Mali ukumbi wa Barbican Centre.
Ukumbi bab kubwa.
Peke yake, Zawose ( na Ilimba na zana nyingine Kigogo)
alitingisha dimba, utadhani kapandwa na radi, kageuka tsunami, sauti nyororo
inayobadilika badilika kuwa kisu, rungu, upinde na mawimbi. Akafa na miaka
hiyo, 63.
Mwandishi nikiwa na hayati Hukwe Zawose, alipokuja kutumbuiza ukumbi maarufu wa Barbican Centre. Picha ya Les Rickford, 1996
Mwanamuziki mashuhuri wa
Kimarekani aliyefariki mwaka 1991 na miaka 65 alikuwa mpiga tarumbeta wa Jazz,
Miles Davis. Miles Davis hakuwa tu mwanamuziki shupavu aliyechora picha wakati
wake wa mapumziko. Miles alileta mapinduzi katika fani hii ya Jazz kwa
kuibadili mara nne. Kwa vipi?
Wakati Jazz ilipoanza karne
ya 20 ilikwenda haraka na “wababe wake” walikuwa Louis “Satchmo” Amstrong
(tarumbeta na kuimba), Duke Ellington (Piano), Dizzie Gillepsie (Tarumbeta) na Charlie Parker (Saxafoni). Hadi leo hakuna
mpiga Saxafoni anayemfikia Charlie Parker kwa kwenda haraka. Baada ya kupiga na
bendi ya Parker kwa kipindi (akiwa bado anasoma) Miles Davis aliamua kubadili
mwendo.
Miles na tarumbeta yake. Picha ya jalada la kitabu cha maisha yake na F Macha, 2015.
Miles na tarumbeta yake. Picha ya jalada la kitabu cha maisha yake na F Macha, 2015.
Alituliza muziki wa Jazz kuwa wa taratibu
zaidi.
Huo ndiyo mwanzo wa “Cool Jazz” unayoisikia sana katika mahoteli makubwa na sehemu za
tafrija za mapenzi na familia, duniani.
Miles alichagua wanamuziki wazuri kuzidi wote akawaingiza katika bendi
zake. Chini yake aliwapa moyo na mafunzo. Wote wamekuwa wanamuziki wakubwa. Mfano
ni Herbie Hancock na mpiga besi mashuhuri
Marcus Miller.
Tatu, Miles alichanganya
Jazz na miziki ya kisasa enzi alizoishi na kuunda mseto unaoitwa Fusion
Music. Alikuwa mvumbuzi na hakupenda
kujirudia rudia aliloshalifanya. Vyuo mbalimbali duniani hutumia miziki yake
kunoa nadharia ...Mathalan kusisitiza “ukimya” katika muziki. Kwamba “ukimya” ni muhimu kama ilivyo “kelele.” Mpiga gitaa
mashuhuri Carlos Santana kakiri hadharani kafunzwa sana na nadharia hii.
Mwanamuziki Remmy Ongala aliyefariki mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 63. Picha ya Jack Vartoogian, New York, 1989...
Mwingine ni Fela Kuti, mwanamuziki
mwa Nigeria.
Fela Kuti alisomea Jazz hapa
London. Aliporudi kwao alitumia ujuzi alioupata kufufua jadi la kabila lake la
Kiyoruba; akaunda mapigo ya “Afro Beat.” Leo Afro Beat imekuwa mtindo mashuhuri.
Wanawe wawili, Seun Kuti na Femi Kuti
wanaendeleza sanaa ya baba yao aliyeingia jukwaani na wake zake 30. Aliwaita “malkia
zangu”...
Fela aliwahi kusema katika
mahojiano kuwa wanaume wengi huwa na wanawake pembeni -yaani nyumba ndogo.
Wanaficha. Yeye huwaweka wote hadharani ili kila mtu ajue. Ukosefu wake huo wa unafiki, ulimponza. Mbali ya muziki wa
Afro Beat alishika ujumbe mzito uliowaudhi mafisadi serikalini.
Mwaka 1977 wanajeshi waliingia eneo lake aliloliita “Jamhuri ya Kalikuta”
wakampiga yeye, wake zake na kumtupa mama yake mzazi toka ghorofa ya pili. Mama
Fela alifariki baadaye kutokana na majeraha ya tukio.
Msanii Kuti alifariki mwaka 1997 akiwa na miaka 58.
Wanahabari waliotutoka
karibuni Tanzania ni pamoja na Mike Sikawa ( miaka 55, mwaka 2008), Adam
Lusekelo (miaka 56, mwaka 2011)...Mhadhiri mpendwa Profesa Chachage S Chachage
alifariki 2006 akiwa miaka 51. Chachage ni wa rika langu. Tulisoma wote na
tulifanya michezo na mazoezi tukiwa
Mzumbe. Baadaye bahati mbaya Chachage aliacha kufanya mazoezi...
Chachage (aliyenyoosha ngumi mwanzo) ...tukiwa pamoja Mzumbe katika timu ya ndondi shuleni. Picha ya Harold Mhando, 1974.
Hii ni mifano michache ya
wanaume mashuhuri weusi.
Ni kitu gani kinachomfanya
mtu mweusi asiendelee zaidi ya 65? Ndiyo
wapo wachache wanaosonga mbele lakini kwanini matarakimu huwa wastani huu zaidi?
Labda msomaji unayo majibu.
Kitabu kipya cha hayati Chachage kilichotoka 2014. Mkusanyiko wa makala zake mbalimbali. Kimechapwa na E & D Limited, Dar es Salaam. Picha ya F Macha, 2015
Kitabu kipya cha hayati Chachage kilichotoka 2014. Mkusanyiko wa makala zake mbalimbali. Kimechapwa na E & D Limited, Dar es Salaam. Picha ya F Macha, 2015
Kwa tathimini yangu naweza
kuwaangalia hawa niliowataja juu.
Sababu ya kwanza iliyowakumba ilikuwa ulevi na dawa za kulevya. Ulevi
kupindukia husababisha kisukari. Na kisukari husababisha kifo. Vijana wengi
duniani hupenda kuvuta bangi. Unapotumia
bangi hatimaye utataka vikali zaidi. Matokeo huharibu mapafu, ubongo nk. Miles
Davis alikiri katika kitabu cha maisha yake (Miles, 1989) kuwa dawa za kulevya
zilichangia kuharibu mahusiano na
familia yake.
Ya pili ni maradhi ya ngono
kama UKIMWI.
Hili huwafika watu mashuhuri
kutokana na maingiliano yao kirahisi na wanadamu wengine. Kukosa nidhamu,
kutoangalia hatari ya matokeo ya unachokifanya ni kati ya majanga. Na kwetu
sote tuliobakia tujifunze nini?
Kila kifo kinapotokea huwa
huzuni. Huwa wakati wa kumwomba Mungu atunusuru. Wakati mgumu. Wakati huo huo
ni vizuri tukaanza kuchunguza nini sababu zinazotufanya wataalamu weusi
kufariki mapema zaidi, hasa pale sababu
zinapoweza kuzuilika.
Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili katika gazeti taslimu, Novemba Mosi 2015....
No comments:
Post a Comment