Wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea miezi kadhaa iliyopita, Mtanzania mmoja mkazi London alikuwa na mtazamo tofauti. Mwanamuziki na mcheza sarakasi huyu anaitwa Fab Moses.
“Nyinyi semeni yenu mnayotaka, lakini CCM na Bw John
Pombe Magufuli watashinda tu.”
Fab Moses si maarufu kwa utabiri bali kwa ucha Mungu
wake, upole na ukarimu. Si wale wanaojifaragua au kupiga kelele mbele za watu.
Mtaratibu anayejishughulisha na kazi mbalimbali za ajira za uchovu tosha. Chukua mfano siku
niliyomtembelea kwake kumfanyia mahojiano haya. Ilibidi miadi ipangwe saa tisa
alasiri, maana aliingia kitandani asubuhi hiyo baada ya kazi ya usiku kucha.
“Ukiwaeleza Bongo kazi tunazofanya hawawezi kuamini,” Fab
Moses alisema akitabasamu bila nadama, majuto au kauli mbaya, “Wanadhani Ulaya
ni kula kuku tu? Nimeingia kazini usiku
wakati wenzangu wanakoroma.”
Moja ya kazi azifanyazo ni usambazaji wa bidhaa ambapo huendesha gari inayoinulia
bidhaa juu ya ardhi iitwayo “fork lift ”
kwa kimombo. Ilibidi asomee kazi hiyo ingawa tayari alikuwa dereva. Hurudi asubuhi
hoi. Mtanzania huyu hufanya pia shughuli nyingine za sulubu kama kusambaza
magazeti madukani. Lakini kipajhi chake mahsusi, Fab Moses ni kucheza sarakasi,
utunzi wa mashairi na nyimbo za Kiswahili anazoziimba kwa sauti inayoghani.
Huimba vile vile nyimbo maarufu za Afrika Mashariki mathalan, Sina Makosa,
Kalubandika, Rosa Nenda Shule nk. Mara
kwa mara huwa na bendi maarufu ya Watanzania, Wakenya na Wakongo, “Afrika Jambo” aliyoiasisi na mpiga gitaa maarufu Kawele Mutimanwa na
wanamuziki wengine : bwana besi Billy Mwangura (Kenya) na RamaSax – mpiga sax m
wa Tanga aliyekuwa zamani kikosi cha
Simba Wa Nyika.
Jina la “Afrika
Jambo” alilibuni yeye Fab Moses.
Fab Moses akiimba na gwiji mwingine wa muziki wa kijadi wa Tanzania, Saidi Kanda.
Fab Moses akiimba na gwiji mwingine wa muziki wa kijadi wa Tanzania, Saidi Kanda.
Picha na Jonathan Pace.
Kabla ya Afrika Jambo, Fab Moses alikuwa pamoja na Kawele
Mutimanwa ndani ya bendi ya No Tchuna Cha iliyotoa albam ya “ Alama Za Vidole”
mwaka 1998.
Ukiacha bendi hizi na muziki, Fab Moses ameendesha kikundi
cha wanasarakasi watatu- The High Flyers (Wapaa Juu), miaka mingi.
Leo anapofanya maonesho yeyote (mbali ya sauti yake inayolinganishwa na ya marehemu nguli Marijani Rajabu) lazima Fab Moses atoke mzima mzima,
atembee kwa mikono, ajirushe , huku akipigiwa makofi , ngoma na vigelegele.
Hivyo ndivyo maisha ya wanamuziki Ulaya huwa. Siku moja moja atakuwa jukwaani
akitumbuiza, nyingine akimenyeka kutafuta fedha ya kulipia nyumba, gari, bima,
chakula na familia. Maisha ya Uzunguni mazuri – ila ghali na kila
kitu huenda kwa muda, muda na muda tena.
Ndani ya haya maisha, aghalabu, yanayodai nidhamu ya saa
mkononi na mbio miguuni, hutafutwa wasaa wa kwenda studio kurekodi. Studio za muziki
Majuu ni nzuri ila aghali sana. Kiwastani studio kubwa, safi, hudai paundi 150
kwa siku (kama shilingi laki nne). Ukitaka za bei rahisi, uchochoroni, labda
nyumbani kwa mwanamuziki mwingine mwenye vyombo, huwa kama paundi 50 kwa siku
yaani shilingi laki moja na robo. Na hizi ni za kubabaisha babaisha, maana vyombo
si vya hali ya kuridhisha sana. Pamoja
na pepesa pepesa hiyo, Fab Moses keshajitahidi kutoa albam yake ya nyimbo kede kede za Kiswahili iitwayo “Nengua”...niliwahi
kuhakiki CD hii ilipotoka 2010. Kati ya waliofagilia “Nengua” ni
mfanyabiashara wa Kiganda John Kizito,
aliyechangia baadhi ya gharama.
Bw Kizito : “Fab Moses
ananikumbusha wananamuziki wa Kiswahili wa zamani. Hapigi makelele wala
hachanganyi matusi na maneno ya Kiingereza. Tena kajaaliwa sauti nzuri sana.”
Ndani ya muktadha huu ndipo Fab Moses akaamua kujitolea
kutunga wimbo wa kuchangia uchaguzi wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Wimbo
huo unaoweza kusikika katika mtandao wa You Tube, unaitwa “Magufuli CCM”
Unaanza na maneno na sauti yake inayofanana na ya marehemu
Marijani Rajabu mwana Sokomoko
“CCM Oyee
CCM
Kanyaga
Kanyaga!
Kanyaga! Kanyaga! Kanyaga!
Kidumu
kidumu chama cha Mapinduzi....”
Baada ya muda wosia kwa Mheshimiwa John Magufuli.
“Baba
Magufuli ushike chombo bahari ni kubwa usituache sasa tukaangamia
Bahari ni
kubwa yenye papa na nyangumi wenye uchu wa madaraka Baba...”
Hapo maneno yanachimba anapokwenda ndani ya maudhui ya
chama na sababu gani baadhi yetu Watanzania
tuna imani na CCM.
“Angalia
Somalia – wanachinjana
Kule
Congo- Zaire- wanachinjana
Sudan
Ooh- Wanachinjana!
Kwa
Gaddafi Libya-wanachinjana!”
Ujumbe mkubwa wa maneno haya ni kwamba ingawa wapo
tusiopenda CCM na wale tuliotaka isishinde uchaguzi mwezi uliopita, CCM
imehakikisha Tanzania nchi ya amani. Ndiyo kisa cha kuyataja mataifa yenye
tafrani : Somalia, Congo, Sudan , Libya nk
Wimbo huu uliochangamka sana umechangia gitaa la Mkongo
ajulikanye kwa jina la Burkina Faso.
Fab Moses ana kipaji cha utunzi wa mashairi na kuimba
lakini hakusoma sana. Alimaliza shule ya msingi, Tandale , Manzese. Angali bado
shuleni na miaka kumi na moja, alianza kujifunza kuruka ruka na kucheza
sarakasi mwaka 1980.
“Enzi hizo tulitumia pumba za mahindi kuangukia (kama
kitanda) mitaani. Baada ya muda
nilipojiamini zaidi nilianza kwenda na wenzangu mitaani kufanya maonesho
yaliyoitwa mwaga mwaga. “
Fab Moses akitembea kwa mikono katika moja ya maonesho yake Uingereza wakati wa tamasha la kutimiza miaka 40 ya urafiki kati ya Uingereza na Tanzania, Novemba 2015. Picha ya Jonathan Pace
Walikuwa wakiruka wanarushiwa fedha na hatimaye mwaka 1982 Fab Moses alichukuliwa na kiwanda
cha majembe cha UFI na kuanza kupata mafunzo rasmi. Hatimaye alihama hama
mashirika mengine ya umma mfano Bandarini na Urafiki ambapo kulikuwa na vifaa
na taaluma zaidi. Taaluma ilipokomaa mwaka 1984 sasa alicheza na vikundi vikubwa vikubwa mathalan Super Mwongozo,
Kigongo cha Mpingo, Super Fanaka na
hatimaye Makutano chini ya hayati mzee Kingalu Ghadhaba aliyewaboresha vijana
zaidi.
Ni katika kipindi
hiki alipokuwa akihudhuria mazoezi na
maonesho ya bendi maarufu iliyoongozwa na Marijani Shaban, Dar International. Humo humo pia alianza kuimba nyimbo za
Taarabu na kikundi cha Bima taarabu kwa mfano. Baada ya kutembelea sehemu
kadhaa nchini ikiwemo ziara ya muda mrefu Mwanza mwaka 1988 ndipo ikaja safari
ya kwendas Ujerumani na kikundi cha sarakasi cha Black Scorpions. Maonesho ya
nchi mbalimbali barani Ulaya hatimaye yalimshusha Uingereza anapokanyaga hadi
leo.
SIKILIZA WIMBO HUSIKA HAPA
-Ilichapishwa na Mwananchi Jumapili, 22 Novemba 2015.
No comments:
Post a Comment