Nilimhoji
Mkenya mmoja kwa kipindi cha Kwa Simu
Toka London. Jina nitalihifadhi kwa sasa.
“Nikiwa
mdogo sikupenda kabisa kwetu Kenya tulivyolazimishwa kujifunza Kiingereza. Tulichapwa...”
Nikasema
ndiyo maana Kenya na Waafrika wengine huzungumza
Kiingereza ( na lugha zingine za Kizungu
) kwa ufasaha sana.
“Lakini
nilipofika hapa Uingereza nilishangaa au tuseme nikajifunza. Waingereza
wanaipenda sana lugha yao. Huongea tofauti
na sisi tunavyoongea. Ukitaka uraia wa Uingereza lazima ujue Kiingereza
sawasawa. Wanakithamini Kiingereza.
Majina, barabara, shule, serikali, muziki,magazeti, vitabu, kila kitu. Hawatumii lugha nyingine. Hawakidunishi. Wala
hawakichanganyi na lugha nyingine. Nikatafakari. Ndipo nikaanza kuifikiria
Tanzania...”
Akadai
miaka mingi amependa sana msimamo wa Watanzania.
“Zipo nchi kumi na moja zinazungumza
Kiswahili. Lakini chimbuko la Kiswahili ni Tanzania. Hata wengine tukijidai,
hatuifikii Tanzania...”
“Miaka
michache iliyopita Tanzania imekichuja kabisa Kiswahili. Mimi sina zaidi ya miaka arobaini, lakini
nafahamu kuwa Tanzania ilikuwa ikitumia kila kitu Kiswahili. Miaka ya karibuni kizazi
chenu kipya kimeanza kukiua kabisa Kiswahili. Kila ninaposikiliza vipindi vya
TV naona watangazaji wakiongea Kiswahili kisha wanachanganya na Kiingereza.
Sijui mnakwenda wapi. Nadhani baada ya kizazi hiki kuzeeka, Kiswahili
kitatokomea...”
Mhojiwa
akaongea mambo mengi...
Hebu
tumwache...
Kila
kukicha mitandao jamii inasambaza video za wageni (hasa Wazungu) wakizungumza Kiswahili fasaha.
Walisoma vyuo vya nje. Wengine wameishi Tanzania mida sasa wanazungumza Kiswahili
vizuri sana.
Miaka
michache iliyopita video ya Wazungu wakiimba wimbo wa “Tanzania Tanzania
Nakupenda kwa Moyo Wote” ilisambazwa mtandaoni. Hawakuwa wakichanganya wimbo
huu mtukufu na lugha zao za Kizungu.
Karibuni wanafunzi wa lugha za Kiafrika walimfanyia
sherehe kumwaga mhadhiri wa Kiswahili chuo cha Leipzig, Ujerumani, Abdilatif
Abdala. Mmoja wa magwiji wakuu wa
Kiswahili; mzawa wa mwambao wa Kenya na kitabu chake cha mashairi “Sauti ya
Dhiki” kilicho maarufu sana. Wazungu hao walimwimbia kumuaga Bw Abdilatif huku wamevaa vitenge vya Kiafrika. Wanaume
kwa wanawake. Wakisifia na kuukabali Uafrika. Kama sisi tunavyosifia na kuukubali
Uzungu kwa majina, magari, simu za mkononi, nk.
Kwanini
wameuheshimu?
Na
ikiwa sisi tunadunisha lugha zetu nani atatuheshimu?
Akizungumza
na Mbeya TV Agosti 2017, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Harrisson Mwakyembe, alisema
kati ya lugha 6,000, Kiswahili ni lugha
ya kumi, na ya pili bara Afrika. Imepangwa kuwa lugha mosi Afrika 2063.
Wanaochangia
kudunisha lugha si wananchi wa kawaida. Ni watangazaji wa redio, TV, wanahabari,
mabloga, viongozi wa kisiasa, waalimu, nk.
Kiswahili kikizungumzwa lazima kipakiwe neno
la Kiingereza.
Kwanini
mtangazaji wa TV aseme “Legendary Remmy Ongala” badala ya “gwiji” au “nguli” ?
Au mwanasiasa adai nchi yetu inakosa “Organisation” si “Utaratibu”? Hapo kuna
ukosefu wa misamiati na udunishaji lugha.
Tunajidunisha.
Kama
wanawake wanaovaa nywele za maiti au Waafrika wanaojichibua ngozi wawe rangi
chungwa.
Wenzetu
wanatucheka.
Hutusema
hatuwezi Kiingereza sawasawa. Moja ya kazi zangu hapa Majuu ni kusahihisha
vitabu na miswaada ya Kiingereza. Waandishi wa Kitanzania wanashindwa kuandika lugha hii sawasawa. Sababu kuu ni kuzoea
kuchanganya- Kiswanglish- sasa unapokuja wakati wa kuandika Kiingereza tasnifu
tunaharibu.
London, Ilichapishwa, Mwananchi Jumapili, 15 Agosti 2018
No comments:
Post a Comment