Maradhi ya figo yamezidi
sana kwa watu weusi, seuze Watanzania.
Majuma mawili yaliyopita tulimpoteza Mtanzania
maarufu sana kwa ugonjwa huu. Ni muhimu kujadili kwanini figo linaendelea kuwa tatizo
kubwa kwetu.
Makala tatu zilizopita
zimeongelea ulaji wa Saladi, mazoezi na kufunga kama njia za kujali figo, ini,
moyo, ubongo,nk. Tumeambiwa matumizi
HOLELA ya dawa za kuzuia maumivu changia
tatizo au pia fadhaa (“stress”) dhalilisha figo.
Wiki iliyopita tulikumbushana
kuwa kufunga si tu Ramadhani au
Uislamu.Tulitazama faida zake ikiwepo kupunguza unene, maradhi, kuupumzisha
mwili na uwezekano wa kuwa na maisha marefu.
Tulitazama aina ya kwanza
ya ufungaji, yaani kunywa maji ( kidogo
kidogo kwa wastani wa saa 36-72).
Ni vizuri maji hayo yakichemshwa,
kama chai. Nilijifunza dhana hii kwa Wachina wanaoshauri
ikiwa ndani ya mwili ni joto (damu) vyema kujimiminia vile vile kitu cha moto. Maji wakati wa kufunga husafisha figo.
Mfungo wa pili ni kutokula chochote
(“dry fasting.”)
Faida na matokeo huwa haraka zaidi kuliko kufunga kwa maji. Kila
aina ya kirusi, maradhi au tatizo hutoweka upesi. Zingatia unapofunga, baada ya
saaa 21 virusi adui mwilini hukosa chakula na kuanza kusambaratika. Ukinywa
maji huchukua muda zaidi. Tuseme baada ya saa 36.
Mfungo wa tatu ni kunywa
juisi (ya matunda au mboga) kidogo
kidogo kwa muda takikana.
Wa mwisho ndiyo unaokua
haraka sana Ughaibuni. Unaitwa “Intermittent fasting.” Pendwa sana na wanaodhamiria kupunguza unene au uzito. Mfano unakula chakula kidogo tu asubuhi. Jioni huli. Kesho unakula
jioni. Unafuata kanuni hii kwa siku
tatu, kisha unaanza tena kula kawaida
(mara tatu kwa siku) hivyo hivyo
kwa majuma kadhaa. Ufungaji huu ni wa kudumu
zaidi na unapozoeleka huwa desturi ya mtu.
Mtindo wowote utakaoamua ni mzuri kwa afya yako.
La kuzingatia ni namna
unavyofungua. Kula milo mizito au haraka haraka wakati wa kufungua si vizuri
asilani. Unapofungua anza taratibu, ikiwezekana kwa matunda laini kama mapapai,
matikitiki maji. Au kama hukunywa maji, anzia na maji moto kwa saa kadhaa.
Baadaye ndiyo vyakula
vyepesi kama uji. Uji wenyewe usiwe na sukari na chumvi bali asali. Baadaye ndiyo mlo mzito.
Si vyema hata kidogo kufungua
kwa vyakula vizito kama nyama au mayai. Ukweli ikiwezekana usile nyama hadi
siku ya pili au ya tatu.
Mwisho tukumbushane kuwa
bado wapo wengi wenye fikra finyu kuhusu afya na kufunga. Huamini eti maradhi au kifo ni “kudra ya Mungu.” Dhana hii
inaturudisha sana Waaafrika nyuma. Tunaweka kila adha mikononi mwa Mungu huku
wenzetu wanasonga mbele. Wapo wanaosema kufunga ni kuendekeza njaa. Hawaelewi kuwa faida ya kufunga ni fikra
pevu, mwili safi, ubongo imara na maisha marefu. Askari wa Kizungu waliokamatwa mateka na
Wajapani wakati wa vita Vikuu vya Pili wakanyimwa kula waliishi zaidi ya miaka
90 hatimaye.
Ndiyo maana wanyama
wakiugua, hawali. Au kama ni paka au mbwa hula majani. Tujiulize kwanini.
Dini ZOTE duniani zina
kipengele cha kufunga. Wanaofuata kanuni
kwa dhati huwa Waislamu na Wayahudi. Wengine tumesahau au hatutunuku
masharti ya imani zetu mahsusi.
London, Ilitoka Mwananchi Jumapili, 10 Machi, 2019
No comments:
Post a Comment