Monday, 24 December 2018

SINEMA ZA NGONO ZINAVYO ATHIRI VIJANA ULIMWENGUNI LEO - 1

Wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais wetu, alisemwa vibaya, aliogopwa, alitaniwa. Ni ajabu namna leo, (nusu karne baadaye) anazungumziwa kwa staha, tija na hata kupendekezwa aitwe mtakatifu. Asiye na hatia au kosa. Sisi wanadamu wanafiki sana. Mtu akiwa nasi tunamsuta. Akishatutoka tunamvalisha kila suruali, viatu, bangili na kofia za jaha.
Nakumbuka tukiwa bado sekondari, tulisafiri sana Nairobi kutembea. Miaka hiyo ya Sabini Kenya ilifananishwa na Ulaya. Majuu. Nairobi  ilijaa klabu nzuri nzuri, mavazi ya Kizungu, sinema tele zikiwemo za ngono. Tuliwaona ndugu zetu wa Kenya wenye bahati sana.
Tulimsikia Rais wao, Jomo Kenyatta akisema: “Kuleni matunda ya Uhuru...”
Baadaye nilipokuwa mtu mzima, nikasafiri Ulaya. Kwa mara ya kwanza nikaona sinema ya ngono,  mwanzo hadi mwisho. Ilikuwa kioja. Sikuziona nikiwa shuleni, ( tuliposafiri Kenya) shauri ya masharti ya kiumri. Ziliitwa sinema za X. Yaani za watu wazima tu.

Sasa nikiwa Ughaibuni mtu mzima niliyeshapitisha miaka 25 sikuzuiwa. Niliufurahia uhondo uliokatazwa na Baba wa taifa na serikali ya TANU na CCM.
Lakini baada ya “kipya kinyemi” kwisha,  nikazoea, nikazikinahi. Nilianza kugundua watu walioangalia filamu hizo walikuwa wanaume wapweke wasiokuwa na wapenzi. Kila mtu alikaa peke yake, mle giza la sinema; akijishika shika; wengine wakinywa pombe kisirisiri. Kifupi waliotazama michezo hii walikuwa wapweke wenye matatizo ya kisaikolojia. Watu na wake zao hawakuhudhuria sinema za ngono. Ndiyo walikuwepo wapenzi walioziangalia. Mmoja mmoja na mkewe, lakini wachache...
Ziliitwa “pornography.”
Neno Pornography leo limefyekwa  kuwa Porno. Porn. Au Kiswahili, Pono.
Asili yake  ni Ugiriki. “Porni”  ni kahaba, na “graphien”, kuandika. Enzi hizo yalikuwa maandishi tu. Baadaye karne ya 19 Wafaransa walionesha michoro  kama suala la kibiashara na starehe. Karne ya 20 ndipo sinema zikatengenezwa. Ziliiitwa sinema za watu wazima zilizopangiwa hiyo herufi X.
Toka mitandao jamii ianze kuonesha picha hizi karne ya 21,  viwango vya umri vimetupiliwa vichakani. Hakuna cha mtoto, wala babu. Mtu yeyote anaweza tu kulipia akatazama, ingawa hata usipokuwa na fedha siku hizi kuna jinsi...
Na hili ndilo janga la 2018.
Vijana, wavulana kwa wasichana wamelewa “starehe” hii. Wanawake wanaoneshwa kama vyombo na vijana wa kiume wanaokua wanadhani mapenzi maana yake ni ngono tu, bas. Wasichana ( au wanawake) nao wanadhani kila  mwanaume  astahili kuwa na sifa na matarakimu “fulani” kama ilivyo ndani ya sinema hizi.
 Matokeo?
 Mosi, wanawaume kwa wanawake hawaheshimiani kimapenzi. Kila mmoja ana taswira isiyo ya kweli kichwani. Pili, kwa kuwa vitendo vinavyooneshwa  vinasisimua, rika hili la karne ya 21 (“millenials “ kwa Kimombo) hujaribu kukidhi mahitaji na hatimaye maradhi ya kisaikolojia yamesambaa kama mashamba makubwa ya mahindi. Mojawapo ni nguvu za kirijali kupungua. Vijana dunia nzima wanaandamwa na tatizo hili.
Hapo ndipo tukiri, Mwalimu Nyerere aliona mbali. Vijana tuliokulia kipindi cha TANU tulinyimwa kabisa kuona “uhondo” huu. Hatukujua kingine. Wala hatukufikiria bamia, tango au ndizi mbivu. Tuliishi kiasilia.
Tuendeleze mada juma lijalo.

Ilichapishwa ,Mwananchi Jumapili, 9 Desemba, 2018





No comments:

Post a Comment