Monday, 24 December 2018

SINEMA ZA NGONO ZINAVYO ATHIRI VIJANA ULIMWENGUNI LEO-3



Tuendelee na mada ya Jumapili mbili zilizopita.
Tumezungumzia sinema za ngono na namna zinavyohasidi afya na mahusiano ya watu. Sawa. Vipindi vya maisha yetu wanadamu hutofautiana. Kama ambavyo makala hii inakashifu sinema za ngono na changamoto zake ndivyo wazee wa miaka ile ya Sitini na Sabini walivyokasirishwa na suruali za vijana zilizotanuka chini (“Pekos”) , na sketi na magauni yaliyoishia mapajani (“Mini”).
 Linganisha na leo.  Vijana wanavalia suruali makalioni, kama wako maliwatoni  na wanawake wanaanika kabisa kila kitu mitandaoni au  maonesho.

Mtindo wa kuvalia suruali makalioni (Kata K),  ulianzia kwa wanaume mashoga. Utafiti uliofanywa na mbunifu mavazi mweusi, shoga,  hapa Uingereza takriban miaka 20  iliyopita (na kuandikwa gazeti la weusi The Voice), ulidai waliofanya ushoga Marekani walilazimika kujificha jificha miaka themanini- tisini,  iliyopita.
Enzi hizo wanaume weusi walisakwa na kunyongwa kwa makosa kama kulala na wanawake wa Kizungu na ushoga. Walioyafanya walikuwa wasiri sana. Walining’iniza suruali  makalioni  kujitambulisha na kupotea haraka haraka wasionekane. Dhana kuwa mtindo huu  ulihasisiwa jela za Marekani ni MPYA.
Mbunifu mavazi huyu alichotaka kusisitiza ni kuwa sayansi ya mavazi yetu leo ina chimbuko pia katika ushoga. Si ubabe au uume!
Tatizo letu Waafrika ni kuiga ovyo.
Inatokana na utumwa wa kikoloni mambo leo kuwa cha nje, bora zaidi. Hakuna ubaya kuhusu Uzungu. Mimi naishi Uzunguni. Tatizo si Uzungu. Tatizo ni kuiga  yanayotuchuja na kutufanya tusahau yetu. Kufuata mrama bila mwelekeo.
Sinema za ngono zina  idara nyingi. Kama ushoga.
  Kabla ya kuendelea tukubaliane kuwa mapenzi ya jinsia moja yamekuwepo toka mwanadamu alipokayaga dunia. Humu Afrika yapo makabila yenye mpaka ngoma na michezo ya kusifia au kujigamba kuhusu mwenendo huu. Kimapenzi basi, ngono ni uchaguzi wa  mtu.   Tatizo ni pale inapopitishwa sera kuwa tusipofuata mwenendo huu tutazimwa kiuchumi na kisiasa.
Mwezi jana Tanzania ilinyimwa msaada wa dola milioni  laki tatu kutoka  Denmark kwa kile serikali hiyo ilichodai unyanyasaji wa wapenzi wa jinsia moja.  Mwaka 2013,  Uganda ilishutumiwa kwa kuyakataza. Mfanya biashara tajiri maarufu wa Uingereza Richard Branson alitoa kauli Uganda ihukumiwe kiuchumi. Hilo ndilo lililoipata Tanzania.
Wazungu wameusujudia kabisa utamaduni huu.  Kiongozi wa serikali ya Luxemborg kaoa mwanaume mwenzake . Mwanamuziki mashuhuri Elton John ana “mume” - David Furnish. Sababu ni nyingi. Kama tulivyoona makala ya wiki jana, ngono na mapenzi hufuatana na  hali ya hewa ya jamii.  Baridi imewafanya weupe wawe na udhaifu kitengo hicho. Ongezea harakati za haki za wanawake kubadili kabisa mahusiano ya kifamilia. Ni rahisi zaidi kuwa na mpenzi wa jinsia yako kuliko ilivyo desturi. Wazungu wanayaangalia mahusiano haya ki kawaida. Imeshavuka mipaka hadi watoto wadogo wanabadilishwa jinsia zao. Mambo haya ndiyo tunayoyaparamia kupitia hizi sinema za ngono na mitandao. Hatuchunguzi. Hatusomi. Hatutafakari. Ni ukoloni mambo leo. Shurti tujielemishe. Kama safu hii ilinavyosisitiza miaka mingi sana...
 Waafrika tuthamini utajiri na uasilia wetu.

ILITOKA MWANANCHI JUMAPILI, 23 DESEMBA, 2018



No comments:

Post a Comment