Tuendelee na mada ya wiki
jana.
Zamani sinema za ngono
zilikatazwa kabisa na serikali ya Mwalimu Nyerere na hata awamu zilizofuata. Leo zinaonekana
waziwazi katika simu na wanawake kwa wanaume wanazikodolea macho. Matokeo kuna
kudhalilishana pande zote mbili. Hii ni kutokana na taswira za waigizaji
wachache wenye maungo yasiyofikana na hali halisi za wanadamu wengi.
Starehe hii kama zilivyo
nyingi za kisasa zimeletwa na utandawazi na teknolojia za Kizungu. Sisi
Waafrika hatukuwa na matatizo ya ngono au ufanyaji mapenzi. Mwalimu Nyerere na
viongozi waliopita wallifahamu hilo ndiyo maana wakalikataza.
Miaka 30 hadi 50 iliyopita
hatukuwa na matatizo ya mapenzi.
Hii ni kutokana na mosi
hali ya hewa ya baridi, pili, biashara na uchumi wa kibepari unaouza kila kitu.
Si kwamba Afrika hakukuwepo (au hakuna) uchumi huu, ila utamaduni wa mapenzi
ulikuwa kawaida. Tukiwa watoto tayari
tunacheza ngoma na kutumia miili yetu bila kujali.
Sivyo Uzunguni.
Watoto wadogo huanza kucheza kwa kuruka ruka
badala ya kutikisa miili yao hasa sehemu za kati. Watu wazima hawana utamaduni
huu, na watoto wa kiume hawapendi kabisa kucheza densi au kukatika viuno. Kwetu
kukatika kiuno (chakacha, mathalan) , si hoja, kwa wenzetu ni matusi
yanayopaswa kwenda kujifunza darasani. Ndiyo maana sinema za ngono ( au za
matusi ) zikawa ( na zingali) jambo muhimu sana, Majuu.
Leo utamaduni huu umeenea
si tu katika hizo sinema , pia, video na sanaa za maonesho ambapo wanawake
maarufu huuza kazi zao, uchi, au nusu
uchi, kisanaa. Kwao ni jambo zito. Lakini mahusiano baina ya watu si huria kama
inavyodhaniwa – na ndiyo maana sinema za ngono hutumiwa sana “kuchangamsha”
hisia.
Tuchukue mfano wa tukio la
wiki mbili zilizopita jiji la Bournemouth (tamka “Bonmuth") ....kusini
mashariki ya Uingereza. Kijana wa miaka 20 alihukumiwa kifungo cha maisha na
mahakama ya Winchester. Roy Thornton, alizoea kutazama sana sinema za ngono na
kuvita bangi. Mseto huu ulikuwa Ibilis kwa mwanaume huyo aliyefanya kazi ya
upishi.
Mosi alipenda sinema za ubakaji (ngono ya nguvu)
na pili, alipanga chumba na jirani mwanamke kijana (34) mzawa wa Venezuela,
Marekani ya Kusini, Stela Domador- Kuzma. Haielezwi ilikuwaje. Ila siku moja, ushetani wa bangi ulimpanda kichwani, Roy Thornton akaingia chumbani kinguvu,
akamchoma dada, Stela, visu 17. Alipofariki
sasa AKAINAJIS MAITI.
Hayo ndiyo matokeo ya hizi
sinema, hususan zikichanganywa na dawa za kulevya. Na ndiyo mambo yanayoigwa
sana Afrika karibuni.
Sasa sisi wenye ngoma
motomoto, tunaoigwa na watu wengi duniani, tumejisahau na kuanza kuiga utumbo. Matokeo vijana wetu wana shida tele za
kimapenzi. Wanawake wanalalamika wanaume
hawana tena urijali. Wanaume wanalalamika wanawake hawajiheshimu, kila jambo
uchi tu. Huu ni ugonjwa wa kisaikolojia uliostawi Uzunguni miongo mingi.
Leo Waafrika ni watu
TUSIOJITAMBUA. Hatujui utajiri na uasilia wetu. Tunaiga mengi yanayotudhalilisha
na kutuchuja.
Ilitoka, Mwananchi Jumapili, 16 Desemba, 2018
No comments:
Post a Comment