Juma lililopita
tulifahamishana kuhusu GMO.
Kabla ya kuendelea
tukumbushane hulka ya biashara hususan huku nchi zilizoendelea. Siku hizi ni
kawaida kabisa kwa wateja, Uzunguni,
kutaka kujua nini wananunua, nini kitakachoingia tumboni, tarehe gani bidhaa itaoza au kukosa thamani, nk.
Wasiojali sana ni maskini au wasiosoma. Lakini hata hawa hulazimika kuchunguza pale maradhi yanapobisha hodi. Tutoe mfano...
Uzunguni kuna tatizo kubwa
la “allergies”
Allergies ni nini?
Haya ni maradhi ya kisasa,
ambayo nimedokezwa yanashanyemelea Afrika kutokana na teknolojia
inayokithiri pia. Huja pale kitu kinapoingia mwilini na kuushambulia kwa vile
viungo vimeshindwa kukizuia mathalan vumbi, moshi au kiyoyozi. Dalili mahsusi
ni kupiga sana chafya- au kuvimba vipele
unapokula au kujigusa na mmea fulani. Ndipo waganga husema : “Allergic
reaction...”
Miaka michache iliyopita
mteja wa Kizungu alikula chakula hoteli. Akafariki. Mwenye hoteli akashtakiwa
kwa kutoeleza katika muhatasari wa vyakula kuwa kitoweo kilitumia mbegu ( karanga, korosho, nk). Marehemu alikuwa na
hiyo “allergy” iliyosababishwa na kokwa (“nuts”)...
Hii mifano inadhihirisha namna
ambavyo wafanya biashara hutakiwa
kuorodhesha Virutubishi, dawa zilizotumika kuhifadhi (“preseravatives”)
na Uasilia ( Organic) wa bidhaa. Vile
vile, GMO.
Mbali na “allergy” -sasa
hii GMO (“Genetically Modified Organism) – yaani vyakula vilivyobatilishwa- vyatakiwa kuoneshwa, makasha ya bidhaa,
kisheria.
Miaka kadhaa imekwisha
toka nilipofurahi sana kufuma Unga wa Ugali unauzwa London. Nilipoona “Made In Tanzania”- nikachangamka. Kabla ya kulipia (kama ilivyo desturi)
nikasoma mfuko. Unga ulitumia GMO. ..
Kichwa upande sikuununua
unga wa nyumbani.
Wapo wasiojali wanakula nini. Wazungu wameshaona
madhara na matatizo, sasa kwa kuwa sisi Afrika hatutahadhari sana, tunageuzwa
soko la GMO
Mwaka 2004 , mtaalamu wa mkusanyiko wa mashirika 170 ya maendeleo ya
Ardhi Afrika (PELUM), Bw Zakary Makanya-
aliandika makala ndefu kushutumu wanasayansi wa nchi zilizoendelea wanavyolitumia
bara letu kama jaa la takataka- kusambaza GMO. Alieleza sababu kumi na mbili kwanini
Afrika isikubali GMO. Ni vizuri msomaji ukajaribu kumsoma mtandaoni.
Alidai kilimo cha GMO ni kizuri
kibiashara- huwafaidi wenye mashamba
makubwa. Ila kwa wakulima wadogo - unaa tu. Pili, akaonya mbolea au dawa
zinazotumika kuzuia vijidudu zina madhara kwa ardhi na mimea. Ukitumia kilimo
cha GMO inakubidi kununua dawa wanazouza wataalamu. Tegemeo hili la dawa ni
sehemu ya biashara. Akasisitiza Waafrika tumetumia mbegu asilia kwa karne
nyingi. Hatuhitaji dawa haribifu. Kwa mfano sasa hivi kuna kampuni
(iliyoshajenga makao yake Dar es Salaam) - Mosanto - kazi yake ni kuendeleza
kilimo hiki. Swali ni je viongozi wetu wanaelewa vipi madhara na faida za GMO?
Je utafiti gani umefanywa na Waafrika tusijeharibiwa? Hadi sasa Zambia, Sudan,
Angola na Benin zimeikataa GMO – ilhali
Ethiopia, Burkina Faso na Afrika Kusini zimechangamkia sayansi hii. Tajiri
mkubwa duniani Bill Gates amepingwa sana karibuni kwa kusisitiza anasaidia
kilimo Afrika kupitia GMO.
Wakati mijadala
ikiendelea, kila msomaji anatakiwa kuchimba zaidi kuhusu mada hii. Hatari zake
kama tulivyotaja sigara wiki jana hazijaeleweka. Tufungue macho.
-ilichapwa Mwananchi Jumapili, 17 Juni, 2018.
No comments:
Post a Comment