Miaka sitini (hadi 100) iliyopita-
sigara, ilivutia sana.
Sinema na TV ziliionyesha waigizaji wakiivuta mithili ya starehe ya hali ya juu sana.
Nikiwa kijana tuliambiwa mwanamke alipovuta sigara kisha akampulizia mwanaume
moshi usoni ni ishara ya kum-enzi, kumhitaji, kumtaka.
Sigara haikuonekana ni dhara.
Ila saratani
ilipounganishwa na sigara- makampuni ya tumbaku yalichachamaa. Mvutano huu wa
kibiashara ulichukua muda mrefu kupingika- hata mauaji na rushwa vilipita.
Vitisho. Ufisadi. Mabavu.
Hapa Ulaya matangazo ya biashara –kuhusu pombe
na sigara- redioni na TV yalianza kuzuiwa kama miaka 30 iliyopita. Leo ni
kawaida kabisa kutoona matangazo hayo. Karibuni sigara zimepigwa marufuku ndani
ya majumba ya hadhara na vyombo vya usafiri. Paketi za sigara zinatakiwa
kisheria kuonesha uharibifu wake kiafya – kwa picha zenye
mapafu au viungo vilivyovimba, kuoza na kusinyaa.
Karibuni madhara ya simu
za mikononi yameongelewa. Ila kwa kuwa utafiti haujafanywa vya kutosha, bado
mada i jikoni.
Halafu, sasa kuna GMO.
Neno hili ni geni - si tu
Afrika, hata kwa Waafrika tunaoishi Uzunguni. Hatari na maana havifahamiki kwa
wengi.
GMO ni kifupi cha “Genetically Modified
Organisms.” Kama hukuwahi kusikia, tafadhali baada ya kusoma safu hii ingia mitandaoni fanya
utafiti zaidi.
Genetic imetokana na
“gene”- kifupi cha DNA- tafsiri ya kamusi ni tabia, umbile, nasaba, ukoo,
kizazi cha kiumbe hai. Mfano mzuri ni pale askari anapochukua alama ya kidole
cha mhalifu. Kila mtu ana alama au mistari asilia tofauti. DNA au “gene” (tamka “jinn”), ni
msingi unaomtofautisha KILA mnyama,
mwanadamu au mmea.
“Modify” ni kubatilisha.
Sayansi ya GMO iligunduliwa kujaribu kupambana
na adha za kiafya. Njia mosi ilitengeneza vidonge vilivyopigana na magonjwa
Bab-Kubwa. Ya pili iliingilia sasa mimea. Chukua mfano wa magugu au virusi
haribifu shambani. Dawa zilizotumika kupambana na bakteria ziliposhindikana,
wanasayansi waliingia maabarani na kuunda chembe hai (hizo “genes” tulizozisema juu) na
kuzipachika na mbegu bora za mimea mingine. Mbegu mpya zilitumiwa sasa
kuchapana na magugu.
Sayansi hii imetumika
kuunda wanyama bomba (“super”)...mathalan kumwekea kondoo mbegu za mbuzi nk.
Kiumbe anayezaliwa atakuwa na nguvu kuliko wenzake asilia.
Leo GMO ni biashara bomba.
Wakulima wa mazao na mifugo ya kibiashara wanaihodhi taaluma kubatili mimea KUTENGENEZA
mazao bora zaidi. Mathalan, ukiona matunda na mboga kubwa zaidi, zilizofanana na kupendeza
kitaswira, zimebatilishwa ZIUZIKE.
Huku Ulaya ukiingia baadhi ya masoko bomba
utashangaa namna nyanya mathalan zinavyokuwa kubwa- rangi nyekunduuuu. NI
kawaida kuona matunda na mimea isiyokuwa na mbegu. Hapo ndipo lilipo somo.
Mungu kaumba mimea na mbegu vipi hazina mbegu?
Afya za wanadamu kidogo
zimeanza kuathirika. Wanaume na wanawake wanashindwa kuzaa, kutokana na mayai
yao kuwa tasa. Unene usiojulikana unachapuka, nk.
Ingawa GMO imeyafaidisha makampuni makubwa, kibiashara; afya zetu hazijatafitiwa sawasawa.
Na ndiyo maana umezuka upinzani mkali sana wa bidhaa za GMO. Hapa Ulaya mapapai
kutoka Hawaii ambayo ni GMO mfano hayaruhusiwi. Unga wa mahindi ( kwa ugali
Afrika Kusini) unatumia GMO.
Tuendelee na mada hii
muhimu sana wiki jayo.
Ilichapwa Mwananchi Jumapili, 10 Juni, 2018
No comments:
Post a Comment