Tuesday, 7 June 2016

SERA KUFUTA PLASTIKI TANZANIA SAMBAMBA NA HARAKATI ZA KIMATAIFA





 Mazingira machafu Tanzania- pic by Juma Gurumo, 2016

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa January Makamba ametangaza kufutwa kabisa mifuko ya plastiki Tanzania mwakani. Agizo hili  linakwenda sambamba na kilio cha dunia nzima sasa hivi. Si tu Afrika ambapo mwamko wa kuyaweka mazingira katika hali ya usafi bado kushadidi vyema.

 Hata nchi zilizoendelea, bado utamwona mtu akimaliza chupa ya bia, juisi, maziwa hata mifuko ya sigara,  chokleti au biskuti akaitupilia nje ya gari – vichakani, barabarani au nje ya nyumba. Tofauti iliyoko kwa wenzetu  ni namna halmashauri za miji na vijiji, zinavyozingatia mara moja kuwatuma wasafishaji na wahudumu wa mazingira kuondoa takataka hizo. Vile vile kila mita chache zimejazana mapipa maalum ya kila aina ya uchafu. Mapipa ya chupa, ya plastiki, vinyesi vya wanyama nk. 

Majuzi kwangu nje alipita mlevi fulani usiku wa manane akajisaidia chini ya mti. Alipomaliza akaendelea kunywa bia yake kitarumbeta. Alikuwa akitetesuka, akiimba na kubwajabwaja ovyo ovyo.
Sikiliza.
Kidesturi, iwapo ningemchukua video kwa simu kisha nikaituma kwa halmashauri ya kijiji au askari wa mazingira wangemtafuta. Kwa vipi? Kila barabara huwa na video au kamera inayochukua picha ya kila tukio. Hutumiwa kukamata wahalifu, kutoa ushahidi,  pia kuzuia ujambazi na ugaidi.
 Wahusika wangetumia video hiyo ya simu kumtafuta jamaa. Wangefuatilia baa aliyotoka, hadi nyumbani kwake. Wangempata tu na kumfikisha mahakamani. Lakini sikuhangaika.
Sasa yule mlevi alipomaliza bia aliitupa chupa chini ya dirisha la mmoja wa majirani zangu mbele kidogo. Kesho yake ilikaa pale kwa saa kadhaa. Lakini kesho kutwa haikuwepo tena. Wafagizi wa barabara na mazingira (wafanyao kazi kila siku), waliiondoa. Si tu walevi na chupa. Wazungu ni wapenzi wakubwa wa mbwa na paka. Kisheria, mbwa hawaruhusiwi kutembea tembea ovyo bila mshipi kooni.
 Mbwa au paka koko akionekana, mara moja atanusuriwa na watu wa mazingira na wasamaria wema wanaohudumia, kulinda  au kuzuia ukatili wa wanyama (TSPCA) na kuhifadhiwa sehemu maalum ya wanyama yatima. Wamiliki mbwa wanapotembea na wanyama wao wanatakiwa kusafisha vinyesi vyao ...

Hivyo basi hutembea na mifuko kama ambavyo sisi wanadamu tunavyohakikisha usafi wa mtoto.
Lakini hutokea wachache wasio jali. Kwa hiyo  mara moja moja moja utakuta lundo la mavi barabarani.  Kisheria kuna adhabu ya kifungo au faini ya paundi elfu moja ( takriban shilingi milioni 4) kwa asiyesafisha uchafu wa mnyama wake, akakamamtwa na kufikishwa mahakamani.  Sasa ukikuta kinyesi kama hicho...huwa cha ama vijana wenye mbwa, magangwe wasio na makazi maalum au walevi wa pombe na dawa za kulevya. Kitamaduni , takriban kila mwananchi, hata akiwa hohehahe asiye na kazi, hufuga mbwa au paka.
Kati ya sababu ni upweke. Mnyama hufidia mapenzi.  Licha ya hali nzuri za kiuchumi, wenzetu walioendelea wapweke  ukilinganisha na Afrika.
Uzuri ni kwamba kama ilivyo ile chupa ya mlevi (tulioisema awali juu), siku hiyo hiyo, kinyesi kitaondolewa na wahudumu wa mazingira. Niliwahi kuzungumza  kirefu na  msafishaji barabara ...aliyehudumia barabara ninayoishi. Alidai kila siku mkuu wake wa kazi  hupita kuchunguza kama amefagia sawa sawa au la.
Akalalamika:
“Mama wa Kizungu kanipita  na jibwa lake (Alikuwa Mwarabu wa Algeria hivyo alitumia neno “kelbu”). Mbwa akachutama.  Akanya. Walipokuwa wakiondoka, nikamwita. Nikamwambia samahani mama. Vipi tena husafishi kinyesi? Mama akaniangalia kama mimi takataka. Akanitukana. Akaondoka zake. Nikajiuliza hawa watu mbona wabaguzi namna hii? Ni kwa vile kaniona miye mgeni?”
Lakini hiyo ndiyo ilikuwa kazi ya jamaa.
Alivaa magwanda maalum:maglavu mkononi na buti. Alibeba toroli ambalo ndani alisomba vichungi vya sigara, vikopo, chupa, magazeti, mifuko ya plastiki, nk.

Kifupi msomaji nakueleza yanayojiri ufahamu kuwa wenzetu pamoja na utashi na kiburi cha kibanadamu, bado wanahakikisha mazingira masafi. Kodi wananchi tunazolipa ndizo zinazogharamia huduma kama hizi za halmashauri ya vitongoji.
Wenzetu wamebobea katika teknolojia. Walianza kuimarisha tasnia hii karne tatu zilizopita. Vyoo na barabara zao safi....
Sisi tumeanza kuisadifu teknolojia  rasmi miaka 60-70 iliyopita. Hatujaizoea. Ingawa Waafrika tulikuwa na teknolojia zetu ( kabla ya ukoloni na utumwa)  imebidi tufuate waliyoyagundua wao. Huenda tungeendelea na yetu kabla ya ukoloni labda tungekuwa vingine. Hatujazoea vyoo vya ndani. Ndiyo maana vyoo vyetu huwa katika hali mbaya. Hatujazoea magari. Gari bado ni chombo cha fahari, Afrika.
Uzunguni gari ni chombo cha usafiri chenye uchaguzi wa kukitumia au kukiacha nyumbani. Huwezi mathalan (kama wewe mwanaume) ukajifaragua kwa mwanamke kuwa una gari kumtongozea.
Gari kwetu bado, anasa. Kutokana na hilo miji yetu inaanza kuchafuliwa sana na magari na mashine. Vumbi na mioshi inaziparamia anga za Afrika. Uchafu wa mazingira utokanao na mashine na magari unatuletea maradhi (ya Kiteknolojia )kama saratani za mapafu na ngozi.
Miji kama Dar es Salaam na Arusha inaelekea  ilipo New Delhi , Beijing na New Mexico. Miji hii ni michafu sana na wenyeji wake hutembea wameziba pua na midomo kwa vitambaa maalum kuzuia hewa chafu (“pollution”).
Tukirejea sasa katika hii mifuko ya plastiki ni tatizo kubwa sana.
Tukianza hiyo plastiki yenyewe. Utafiti nchi zilizoendelea umeonesha madhara ya kula vyakula na vinywaji vilivyofungwa katika plastiki. Unapoacha kinywaji au chakula ndani ya  chupa (au mfuko wa plastiki), juani mathalan ile plastiki huyeyuka ndani yake na kusababisha maradhi mengi yanayotiririkia  ndani ya damu.

Dunia nzima inasikitika namna plastiki inavyozidi kuyaharibu mazingira. Si tu mifereji, mito, maziwa na bahari. Mimea, wanyama na ndege wanaotegemea vyakula asili vyote vinaathirika leo. Wanasayansi wanaeleza sumu ya plasiki hukaa ardhini miaka 500. Hii ni sumu ya vizazi vingapi mbele?
 Sera  ya Ofisi ya Waziri January Makamba kupiga marufuku kabisa mifuko ya plastiki 2017, shurti ipigiwe makofi. Wazungu wameshafuta matumizi ya mifuko hii. Wengi duniani  wameanza kutumia mifuko ya karatasi na vitambaa badala ya plastiki. Watanzania tukifuta plastiki  ni hatua njema kwa afya ya vizazi vya sasa na vijavyo. 


Ilichapwa Mwananchi Jumapili, 5 Juni, 2016 na Oktoba 2015.


1 comment:

  1. Hakika mifuko ya "plastic" ni changamoto kubwa. Sijauona mkakati mahususi wa kuidhibiti mifuko hii lakini ama kwa hakika tamko la Waziri ni la kupigiwa makofi ila isiishie kwenye tamko

    ReplyDelete