Zamani wakati nikikua
tuliambiwa ukinywa madafu utaota busha.
Njoo sasa katika nazi na mapishi yake. Watoto wa kiume tulibezwa tulipokuna
nazi. Nakumbuka enzi nikiishi kikapera Mwananyamala , Dar es Salaam
nilitembelewa na dada fulani. Alipogonga mlango akanikuta nimekaa juu ya mbuzi
nikikuna nazi hakustahimili.
“Freddy hebu uko...pisha nikusaidie.”
Ilikuwa miaka 40 iliyopita.
Sina hakika kama leo mambo yamebadilika.
Tukirudi katika madafu.
Nilipokuwa likizo nyumbani
karibuni ilikuwa kazi sana kupata madafu mitaa ya Dar es Salaam. Wakwezi walilalamika
nazi hazipatikani. Miti imekatwa katwa. Ilibidi tuvuke Kigamboni kupata nazi.
Mji Mwema na kadhalika.
Ukija kwa watu wa mikoani ;
madafu ndiyo hayajazoeleka. Nimekutana na Waafrika wanaotoka kanda zisizo na
bahari kama Rwanda, Zambia na Zimbabwe. Madafu si mazoea wala kinywaji
wanachokienzi.
Si kweli , la hasha. Madafu hayaleti busha. Busha ni maradhi
yanayosababishwa na kirusi kupitia mbu. Kirusi hiki kinachoitwa “filarial” ni
aina ya nyungunyungu au mchango. Husambaa na madhara yake, tunaelezwa, hayana
tofauti sana na tegu, malaria, nk.
Uzushi na kutojua ndiyo
unaotudanganya eti tukila madafu tutavimba miguu au mbegu kuu za uume. Si
masihara miaka 50 iliyopita wengi wetu tuliogopa kula madafu tukihofia kupata “mshipa”
kama ilivyosemwa kwa lugha isiyo ya kitafiti au kisayansi.
Sasa tukirejea kwenye nazi
yenyewe.
Waafrika Mashariki tumezoea
nazi kwa mawili. Mafuta ya kujipaka, kupika au tui la kupikia. Nadra sana
kumkuta mwananchi wa sehemu hizi akila nazi. Madafu ndiyo , lakini kula nazi mh
mmh....
Njoo Ulaya kesho Jumatatu.
Miaka 30 iliyopita Wazungu
wameanza kuona na kutambua madhara ya teknolojia na mashine. Vyakula vingi
vinavyotengenezwa kwa mashine au kutumia “kilimo cha haraka” - vimegundulika
kutojenga ama kutostawisha mwili. Mifugo
inayokuuzwa upesi upesi ili kuuzwa na kufikia lukuki imeanza kukataliwa baada
ya wanancchi kugundua madhara yake. Chukua nyama ya kuku na mayai, kwa mfano.
Kuku wa Kizungu zamani
alifugwa nje, akaruhusiwa kukimbia kimbia kama ndege yeyote mwingine asiyeruka
hewani, mfano bata, bata mzinga, tausi, nk. Miaka ya karibuni kutokana na biashara,
ubepari na tamaa wafanyabiashara hufuga ndege ndani ya majumba maalum. Huwanyima
mwangaza na jua asilia. Huwachoma sindano na kuwanywesha dawa wakue haraka.
Miaka kumi iliyopita kuna kipindi kilifanywa na runinga maarufu ya BBC
kikiongelea kuku “ eti wa kisasa” anayefugwa kuanzia kifaranga akawa tayari
baada ya majuma matatu. Kuku huyu hana tofauti na picha fulani au mchezo wa
kuigiza. Mzuri, mkubwa, mzito, mnene. Malezi yake ni jela. Haruhusiwi kucheza
cheza na kuwa kiasilia. Hukua haraka ndiyo lakini akiteseka. Hukaa pale pale
alipozaliwa akijinyea, akila, akiimba, akilala;
hapo hapo.
Kipindi hicho cha BBC kilionya ukitaka kujua
ndege kateseka, angalia magoti yake utaona rangi na madoa meusi. Damu itakuwa
imesinyaa. Huwa ndege huyu si mtamu hata
kidogo.
Kinachomfanya ndege aina hii
wawe watamu ni vikolezo. Chumvi. Pilipili. Mafuta. Na kadhalika. Yote haya
huchangia maradhi kwetu walaji. Ugonjwa wa moyo. Ngozi. Utasa. Matokeo wananchi wengi hapa ama hawali
kabisa nyama au kama wakinunua...lazima
maduka maalum wa kuku waliokuzwa “kienyeji” walioruhusiwa kutembea nje na kula
wadudu kama ndege anavyotakiwa kuwa kiasilia.
Maskini tu ndiyo hula nyama hizi za ndege aliyeteswa. Maana
bei rahisi. Hata kuku wanaosemekana ni “Halal” huwa hao hao. Na wageni wanaofika toka nchi mbalimbali
maskini hununua haraka haraka bila kuchunguza. Tatizo limezagaa na kufahamika
Uzunguni.
Kwetu Afrika wananchi wanaanza kukataa kufuga
kuku kidesturi. Kuku wa kienyeji siku
hizi hawaliwi. Waafrika tunaanza kuiga Uzungu ulioshakataliwa. Matokeo tunaanza
na sisi kupata maradhi ya Kizungu. Saratani. Kukohoa ovyo. Mafua na vikohozi
vya ajabu ajabu. Maradhi ya ngozi, nk.
Ndiyo sababu sasa Wazungu
wanatafuta sana vyakula asilia. Ilianza Aloe Vera. Ishazoeleka.
Yakaja matunda kama mapapai, maparachichi, maboga, nyanya nk. Karibuni
limeingia wimbi la mbuyu na nazi. Mbuyu bado haujajizatiti sana. Lakini nazi? Kuna
sabuni za kila aina za kuoga na kufulia, mafuta ya kujipaka na kuosha nywele (“shampoo”)
na kupika; dawa za mswaki, juisi na keki, pombe, mvinyo; ili mradi kila kitu
sasa hivi maduka ya afya ni nazi, nazi, nazi. Coconut. Tena aghali sana. Vipindi lukuki mitandaoni na runinga
vinatathmini manufaa ya nazi.
Kinga maradhi (kama yalivyo
maparachichi, Alove vera, mbuyu nk), kuzuia kukatika nywele, kucha, kubabuka ngozi na kupunguza unene. Tuzungumzie
unene. Miaka michache iliyopita nazi ilikuwa ikipigwa vita kwa sababu ina
mafuta. Lakini karibuni utafiti umegundua kuwa mafuta yaliyoko katika nazi
hayadhuru. Ni kama yaliyomo katika mbegu. Korosho. Karanga. Mbozi. Mbegu za maboga,
nk Mafuta asilia. Hupunguza unene au
“cholesterol” – kwa lugha ya kitaalamu
Uchunguzi mmoja uliofanywa
kupitia wanawake 40 na wanaume 20 wanene sana ulikubali kuwa walipungua kiasi
kikubwa baada ya kulishwa mafuta ya nazi kwa majuma manne.
Juzi hapa nilikuwa nikitazama
kipindi cha jamaa aliyeshaandika kitabu kinachozungumzia faida 99 za nazi. Tisini na tisa! Kati ya faida hizo nikusukutua. Anadai ukisukutua kwa nazi unaua virusi mdomoni.
Kingine jamaa alichosema ni
kuimarisha kazi ya ubongo na kichwa. Tunafahamu kadri tunavyozeeka ndivyo kadri
mwili na viungo huzeeka. Sasa uzuri wa nazi uko hapo. Mafuta na ule weupe weupe wake una kitu kinachoitwa
“ketone” ambacho mbali na kukupa nguvu kinaimarisha uwezo wa kufikiri na
kupunguza kudhalilika kwa ubongo.
Utafiti umeonesha (na
kudhihirisha) kuwa wakazi wa visiwa vya bahari ya Pacific (Fiji) huwa hawana
matatizoya kupotewa na akili au
kumbukumbu (Alzheimers Disease) kwa vile
asilimia 90 ya mlo wao ni nazi.
Afya yako msomaji
inakutegemea wewe mwenyewe. Kama ulidharau nazi au madafu; ukidai huleta busha
au ni chakula cha Waswahili wa pwani wasiosoma, achana na mawazo hayo finyu.
Nazi ni muhimu sana katika maisha yetu.
Tusisubiri wenzetu nchi
zilizoendelea watukumbushe kila mara kuwa tulicho nacho Afrika ni cha thamani sana.
Tuache ulimbukeni wa kuiga
na kula vyakula duni na nyama zinazotudhuru tukidhani hayo ndiyo maendeleo.
Ilichapwa Mwananchi Jumapili, 29 Mei , 2016.
No comments:
Post a Comment