Bondia Muhammad Ali alipotembelea Tanzania mwaka 1980 akiwakilisha Marekani kuhusu michuano ya Olimpiki Moscow iliyokuwa na ukinzani. Kushoto kwake ni Thomas Mweuka wa Ofisi ya Habari Marekani Tanzania, USIS. Picha ya Mtandaoni.
Mwanadamu anapofariki huacha
mali, watoto au maarifa. Mengi yameandikwa ( na yataendelea kusemwa) kuhusu
maisha ya bondia maarufu Muhammad Ali
aliyezikwa Alhamisi, Kentucky, Marekani.
Wapo
watu mashuhuri aina mbili.
Waliofahamika kwa kitendo au vitendo fulani na
waliobadili kabisa mambo au mitazamo. Ali yumo kundi la pili. Mifano michache ni Wagiriki Aristotle, Pluto, Socrates au
Mjerumani Karl Marx aliyesasambua fikra za kikomunisti . Yesu
Kristo, Buddha na Mtume Muhammad SAW, hawana ufafanuzi. Mwanasayansi
Albert Einstein alivumbua nadharia ya bomu la nuklia. Wanasiasa kama Mahtama
Gandhi, Abraham Lincoln na Fidel Castro ( bado hai) wa Cuba. Afrika tunaye
Mtemi Shaka Zulu, Nelson Mandela na Mwalimu
Nyerere aliyejitahidi kuunda jamii mpya.
Michezo? Pele wa Brazil, mwanariadha Jesse Owens aliyewika miaka 80 iliyopita.
Na Muhammad Ali.
Kwanini Ali yumo?
Tumgawe mafungu manne. Taaluma , maarifa ,
msimamo na udhaifu.
Kitaaluma Ali alianza ubondia akiwa na miaka 12...baada ya
kudhamiria kulipiza kisasi jamaa aliyemwibia baiskeli yake. Zamani mabondia
waliingia tu kilingeni , hawakusema sema, walituna madita tayari kuchapana. Kwa
watu weusi Marekani masumbwi yalikuwa ajira iliyotajirisha. Ali alibadili
kabisa mtazamo huo wa kuwaona mabondia mbu-mbu-mbu!!!
Aliifanya taaluma ya kustarehesha na kupendeza. Kiufundi alipiga kichwani tu.
Hakuendekeza desturi ya mabondia kurusha ngumi “popote tu” mwilini. Na akipiga sehemu
fulani ataidonoa pale pale hadi ipasuke, ivimbe au kutota damu. Ufundi huo anao
chui. Simba, duma au mbweha humkamata mnyama shingoni , mkiani au popote
pengine. Lakini chui akivizia hushika sehemu moja. Habadili badili hadi nyama
imegeuka kitoweo. Neno la Kiingereza ni “stealth”....Hila na werevu.
Ali alikuwa na wepesi wa kila kitu : miguu,
mikono na mwili usiotulia. Kwa
wanamasumbwi wa uzito wa juu si rahisi kuruka ruka na kucheza densi. Mbwembwe
zake zilichanganya kukwepa haraka akienda kinyume kinyume na kiupande upande kama kaa
baharini. Aliita mtindo wake sayansi. Si ajabu mpiganaji maarufu Bruce Lee
alimwiga. Ukitazama sinema ya “Enter The Dragon” utaona sanaa za Ali kwa Mchina
huyu ambaye wengine (nikiwemo) tunamhusudu kuzidi chapati na fenesi.
Maarifa.
Ali miaka ya Sitini, akifanya masihara na watoto mitaani...
Kidesturi wanamichezo si
watu wanaowekwa kundi la wanafikra. Ali alitabiri lini atamtumbua mpinzani
wake, na juu alitongoa mashairi na
kuunda misemo lukuki; yenye falsafa, ucheshi, sanaa na majigambo ya
kisakolojia.
“Nina
spidi kali. Jana usiku nilizima taa nikawahi kufika kitandani kabla chumba
hakijapata giza.”
Au utashi wa nahau na
fasihi:
“Nimepigana mieleka na mamba, nikabingirishana na nyangumi,nikautia
umeme pingu: na kuifunga radi jela. Wiki iliyopita niliua jabali, nikajeruhi
jiwe, nikalitia tofali hospitali. Mimi mkali
huzifanya dawa ziugue.”
Aliwasanifu aliopigana nao
ili kuwapiku kiakili...
Alimwita Sonny Liston “dubu”
, Joe Frazier “gorila” na kumtania George Foreman ( Congo- Zaire, 1974) kiasi
ambacho leo Foreman hucheka akikumbuka: “Kila nilipompiga ngumi, Ali alificha
uso nyuma ya mikono yake akinisanifu, Joji ni hicho tu ulichonacho? Na ukweli nilishamaliza nguvu zote. Ha ha ha.”
PIcha maarufu ni ile ya Ali alipomchapa Sonny Liston aliyekuwa akiogopewa mwaka 1963. Hata hivyo watu hawakuamini ngumi aliyomwangusha nayo ilikuwa kweli. Ilibidi pambano lirudiwe na ukweli ukabainika. Picha ya Mtandaoni.
Enzi hizo George Foreman na
Sonny Liston waliogopewa kama Mike Tyson alivyokuja kuwa. Kabla ya pambano waganga walishatayarisha
gari ya kumbeba Ali kumkimbiza hospitali. Aliwazidi.
Funzo kwetu hapa ni kutumia akili na
saikolojia kupambana na maisha. Ali hakusoma na kipimo cha Wazungu cha akili
yake ( IQ) kilimpa namba78 ambayo ni chini sana. Hiyo inatuelezea nini kuhusu
mizani za Wazungu na uwezo wa mwanadamu?
Tatu.
Msimamo wa Ali.
Watu weusi waliteswa na kudhalilishwa kwa
neno: “nigger”....Wakati Ali akianza kupigana miaka ya Hamsini, weusi walikuwa wakinyongwa hadharani na Wazungu. Hivyo michezo
na sanaa ilikuwa tegemeo kuu la kujiendeleza.
Baada ya kushinda medali ya
dhahabu (Olimpiki, Roma, 1960) na kuwatangwa mabondia zaidi ya 20, akiwemo
Sonny Liston, Ali alibadili jina la
Cassius Clay kuwa Muhammad Ali mwaka 1964. Dini ya Kiislamu kwa weusi Marekani
kipindi hicho ilikuwa dini ya kimapinduzi. Hata leo Waislamu weusi wamejenga
jamii zao zenye nidhamu na kutofuata mienendo iliyowekwa na Weupe. Kila
alipoanza pambano alionekana akiinama na kusali. Alikuwa na nidhamu na alisema
yeye mzuri, akiwa na maana watu weusi wazuri na shupavu.
Alikataa kupigana
vita vya uenevu Vietnam. Ukitazama sinema ya Ali (aliyocheza Will Smith, 2002),
utashuhudia pale Ali anapotoka mahamakani akishutumu serikali na kusema yuko radhi
kwenda jela kuliko kusafiri mbali kuua watu ambao hawajahi kumdhalilisha. Anachotaka ni uhuru. Huu ni uanaharakati wa
hali ya juu. Walimvua taji lake la ubingwa 1967 hadi 1970.
“Huduma
kwa wengine ni kodi tunayotakiwa kulipa kwa chumba tulichopewa hapa duniani,”
alidai.
Funzo kwetu ni
kuwa na msimamo thabiti, kutotetereshwa na mali, uongo au vitu. Ali aligeuza taaluma
yake kuwa chombo cha kuwakomboa watu wake kutoka utumwani. Kila alipoweza
aliitaja Afrika ambapo mabondia wa leo kama Floyd “Money” Mayweather wanadharau.
Ali alitembela Tanzania mwaka 1980.
Udhaifu.
Ali alioa mara nne. Kati ya
wanawe tisa, Laila Ali, binti, ndiyo
aliyemrithi ubondia na hadi alipojiuzulu 2007 hakupigwa. Mke wa mwisho Lonnie alijitolea
kumuuguza na kusimamia mali zake. Inadaiwa
mtoto wake pekee wa kiume Ali Junior yuko katika hali mbaya kimaisha. Kabla ya mazishi, habari kwamba dola
milioni 55 alizoacha Ali tayari zimeanza
kugombaniwa zimezagaa magazetini.
Ali akiwa na binti yake Bondia Laila, aliyepigana hadi 2007 bila kushindwa. Picha ya Mtandaoni
Mganga na kocha wake Ali, Ferdie Pacheco,
alimwonya mwaka 1975. Hii ni baada ya
pambano kali kati yake na Joe Frazier, lililoitwa “Thriller in Manila.” Lilichukua raundi 15 na Joe Frazier alilazwa
hospitali. Dk Pacheco anasema Ali
alipokataa kujiuzulu, aliachana naye. Kuanzia hapo Ali aliendelea kupigana hadi
1981. Akapatwa na maradhi ya Parkinson mwaka 1984. Ugonjwa wa Parkisons
hushambulia ubongo.
Funzo hapa ni mwanadamu kujua kikomo cha nguvu na udhaifu wako.
Kusikiliza ushauri na kutokuwa mwenye tamaa. Utunzaji wa mali, kuhakikisha
tunaacha wosia unaofaa na familia.
Mwanamuziki maarufu, Bob Marley, alieacha
watoto kumi na moja alikataa kuacha karatasi ya mirathi. Suala lilichukua miaka
kumi kusuluhishwa mahakamani. Mjane wake, Rita Marley, ndiye anayesimamia mali
hiyo iliyokuwa dola milioni 30, leo ni 130 milioni. Rita amewakubali watoto
wote Bob aliowazaa na wanawake saba , na kuhakikisha hawadhaliliki.
-London, 8 Juni ,
2016
-Barua pepe: gmacha52@gmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com
No comments:
Post a Comment