Miaka
ya karibuni wananchi wengi- hususan
vijana- wameulizia mahusiano ya kimapenzi na wageni hasa Wazungu. Hayakuanza leo, jana wala juzi.
Yamekuwapo daima. Ukweli idadi fulani ya watu wa mataifa yote duniani hutaka
kuwa na mahusiano na wageni. Mosi, kutaka kuondokana na udhia wa wananchi wenzao;
pili, kutafuta maisha bora; tatu,mapenzi na ndoa na nne, udadisi (kipya
kinyemi).
Mwandishi nikitumbuiza ngoma wakati wa Carnival la London, Agosti, 2012.
Picha na Urban Pulse Creative Media
Miaka
arobaini au hamsini iliyopita nakumbuka waliopenda mahusiano na wageni walikuwa
zaidi wanaume. Wanawake waliojamiiana na wageni waliitwa malaya, na wachache ni
wale tu waliofanya kazi mahoteli makubwa ya kitalii kutafuta ajira. Mathalan
nakumbuka miaka ya Sitini na Sabini, Tanzania ilijazana wakimbizi. Sera ya TANU
na siasa ya Azimio la Arusha ilisaidia walioathirika na udhalimu wa kikoloni,
ubaguzi nk. Toka Kongo, Afrika Kusini,Palestina, Malawi, Marekani, Uganda, nk.
Wengi
wa wakimbizi wa Kongo (iliyoitwa Zaire enzi za utawala dhalimu wa Jemadari
Joseph Mobutu) walikuwa wanaume, hasa wanamuziki, waliohusudiwa sana na wanawake wetu. Mzaire
aliongea Kiswahili -chenye lafudhi ya
Kifaransa na Kilingala- kilichomfanya
avutie kwa utofauti na mwanaume wa Kitanzania. Au wakimbizi wa Afrika Kusini, Namibia na
Zimbabwe. Tuliwaita Waafrika Kusini, “Wasoweto”
kutokana na harakati au machafuko ya kitongoji cha Soweto mjini Johannesburg
mwaka 1976. Wasoweto walikuwa tofauti. Walivalia suruali pana pana. Waliongea
Kiingereza fasaha. Vijana wa kiume na kike tuliona akheri kubwa kwenda na
Wasoweto kuliko wazalendo wenzetu. Miye kwa mfano nilikuwa na sahiba aliyependa fasihi, mashairi na kupiga muziki.
Awali
nilipata shida sana – na miaka yangu ishirini na moja au miwili-, kupata sahiba
wa kike aliyependa fasihi na muziki. Wasichana wa rika langu walitaka kwenda
baa, kunywa bia – na vile ka- mshahara kangu ka uanahabari magazeti ya Chama
(Uhuru na Mzalendo) kalivyokuwa nyau, haikuwa rahisi kubembelezana na dada
zangu, hata wawe wazuri namna gani. Aghalabu, kadri uzuri ulivyozidi ndivyo
karaha ilivyoongezeka.
Wasoweto
hawakujali. Azma yao ilidai uhuru; walipenda utamaduni wa michezo na kusoma
vitabu. Mkikosa fedha ya basi au teksi mnatembea tu kwa miguu mkiongelea haiba
ya mawingu, maua waridi, misufi, twiga, muziki wa Jazz, Taarabu, hadithi za Ali
Nacha na siasa za Wapalestina. Mkifika hivyo hivyo ugali kwa maharage na ndizi kisukari. Mnasoma
mashairi ya Shaaban Robert na Christopher Okigbo (Mshairi wa Nigeria aliyefariki
angali kijana mwaka 1967) baadaye usingizi wa mapenzi ya joto la Dar es Salaam.
Au mnakwenda tu ufukwe wa bahari kufurahia mandhari. Hayo ndiyo mapenzi ya
kweli. Si mapenzi ya kutegemea mfuko kwanza. Fedha na baa hufuata baadaye. Kinachotangulia mapenzi asilia.
Kwa kina dada mambo pia hayakuwa rahisi.
Kijana wa kikwetu akishakutoa dada, -akikununulia zito, jepesi na la wastani-
ukishafurahi unakuwa sasa mtwana wake. Kuna siku utapigwa. Utasutwa. Iko miezi utawekwa hata mimba na jamaa hatoonekana
kumtunza mtoto. Baadaye utagundua ala kumbe! Kapata mwingine.
Uafadhali
ulionekana kwa Wamarekani weusi. Warefu, wazungu weusi, wenye tabia tofauti na
zetu. Waliongea kile Kiingereza cha “bradha- man” na “sista-du” kiliichoonekana
kitamu. Wakimbizi na watembezi wa Kimarekani walijazana Tanzania ya kipindi
hicho. Walizikimbia tafrani za Marekani: ubaguzi wa ngozi, harakati za chama
cha Black Panther kilichochukua bunduki kupigana na nguruwe weupe. Hadi leo
haujaisha. Enzi hizo mwanamke wa Kitanzania akimwona “Mniga” (kama tulivyowaita
mitaani) ni kama kumshuhudia mdogo wake Mungu. Astakafurlah! Macho huwatoka
kina dada; ndimi nje. Walijua kuongea na mwanamke, walifuzu mapenzi. Ni kama
Wanigeria wanavyohusudiwa na wanawake wetu leo. Kipya kinyemi. Baadaye
iligundulika hawakuwa tofauti na wanaume wazalendo.
Miaka
imevuta miguu; leo wanawake weusi hawataki wanaume weusi ki- jumla. Mwanaume
mweusi hakosi nyumba ndogo au tatu. Mwanamke mweusi keshamfahamu kaka yake.
Keshamjua. Akishamkubalia huba au mahaba, hatokuwa yeye tu. Hilo limeenea Majuu
yote. Limeenea kiasi ambacho dada weusi hawana imani na kaka zao. Wameanza
kusaka Wazungu. Zamani Mzungu hakupendwa sana na mwanamke mweusi. Wapo dada
wachache waliokwenda na Wazungu ndiyo; ila wengi walidai ah Mzungu hana nguvu
kitandani. Au walilalamika wajihi wa ngozi haukuwavutia.
NGOZI IKOJE SIJUI...
Leo
mengine. Kinachotafutwa ni mapenzi na mahusiano si kitanda au fedha tu..
Hivyo
basi, mapenzi yanayodumu, yanayowezekana ni baina ya mwanamke mweusi na Mzungu.
Sikiliza...
Wakati
harakati za ukombozi wa wanawake wa Kizungu zilizofoka moshi miaka ya Sitini, wanawake
waligeuza mahusiano. Miaka ya Sabini uzunguni kote ulikuwa wakati wa wanawake
kudai usawa makazini, kuwataka wanaume waache udhalimu nk. Leo wanawake wa
Kizungu ndiyo watawala wa nyumba, hata
sehemu za kazi za kijamii. Wanawake wa Kizungu wanatawala mazingira kiasi ambacho
kura za kisiasa zinawaegemea. Hapa Uingereza kuna mfano mzuri, kisiasa.
Mwezi uliopita Bwana David Cameroon, Waziri
Mkuu (na kiongozi wa chama cha Conservative) alibatilisha baraza lake la
Mawaziri. Badala yake alichagua wanawake zaidi. Inadaiwa kafanya hivyo kutafuta
kura za wanawake uchaguzi ujao wa 2015.
Mbinu hizi zilitekelezwa pia na Waziri Mkuu wa
zamani, Chama cha Leba, Tony Blair, alipoingia madarakani, 1997. Alifanya
historia kwa kuwa na wabunge 101 wa kike , baadhi walishika vyeo vya uwaziri! Waliitwa “Blair’s Babes.”Hadi leo wengi bado
wamo serikalini. Huo ni mfano mdogo unaodhihirisha namna mahuasino
yalivyobadilika kuanzia mapambano ya haki za akina mama yalipochachamaa Ulaya
miaka hamsini iliyokwenda.
Wanawake
wanatawala na ni wakali. Baadhi ya wanaume wa Kizungu huona afadhali kuwa na
wanawake wa mataifa mengine – Asia na
Afrika. Hawa nao huwa wamechoshwa na wanaume wasioaminika. Hapa basi watu
wawili hawa walioshakereka, hukutana.
Ndiyo maana leo mahusiano baina ya wanawake weusi na wanaume wa Kizungu
yanastawi sana.
Tanzania
je? Wengi wanaandika kuulizia mahusiano na Wazungu. Ugumu wa maisha unajenga
ari za kumpata mgeni kujiendeleza. Je kuna wepesi na uzito gani? Tuendelee na
mazungumzo juma lijalo.
-Ilichapishwa 10 Agosti 2014 na Mwananchi Jumapili
No comments:
Post a Comment