Monday 18 August 2014

KWA WANAOLILIA MAPENZI NA WAGENI AU WAZUNGU- Sehemu ya 2...


 Karibuni rafiki yangu Mzungu alikuwa Afrika.
Taaluma yake ni uanahabari.  Anaipenda sana Afrika na watu wake. Zamani babu aliishi India na alipinga sana ukoloni. Ana mke  na watoto wawili. Shughuli zake humzungusha kila sehemu.  Analijua bara kuliko hata tuliozaliwa huko.  Baada ya  sifa na vicheko, ghafla alisuta mapenzi.
“Ningekuwa mmoja wa babu zenu zamani Bwana Freddy ningenyaka wake ishirini. Kila  nilikokwenda sikukosa sahiba.  Wanataka niwatumie tikiti za ndege. Waje Ulaya waishi raha mustarehe. Ni vigumu sana kuwahimiza dada hawa kwamba maisha yangu si ya kitajiri. Hata ningekuwa tajiri kwetu Ulaya ndoa za mitala haziruhusiwi.  Na mke wangu hatofurahi akisikia nina wake wengine!”
Inachekesha alivyosema, lakini ndiyo kichuguu cha mchwa hicho.
Kuna kaka mwingine naye karejea Afrika Mashariki alikotalii. Mnigeria.  Anawavika  sana taji Watanzania. Wakarimu. Si wakorofi kama kwao Lagos, anaremba.
Kweli Wanigeria ni watu wanaojituma sana. Wengi wamesomea shahada tatu kwa mpigo. Wamezagaa ulimwenguni. Wajuaji. Na huo usafiri kafiri hawakuuanza jana. Sisi tumegundua kuja Ulaya na kwingineko takriban miaka hamsini tu. Wanigeria wamesafiri na kuishi ugenini toka  karne ya 18. Walikuwa miongoni mwa Waafrika waliofanya kazi za uaskari doria na ubaharia, bandari za Uingereza - Liverpool, London na Blackpool, karne ya 19.
 Leo baadhi ya Wanigeria  wana shughuli halali na zisizo halali. Wakati nikiishi Brazil, (miaka 20 iliyopita )Waafrika waliokamatwa na dawa za kulevya walikuwa Wanigeria. Sasa hivi wanawake wa Kitanzania wanaoatilishwa na  ukahaba wa kishetani na kitumwa -China na Hongkong- wanahadaiwa na kupigwa na makuadi wa Nigeria.
 Miaka ya karibuni  Wanigeria “wameivumbua” Afrika Mashariki hususan Tanzania. Wamewagundua pia wanawake wa  Ethiopia, Uganda na Kenya. Wanawapenda  wasivyo wakaidi. Upole huu wa mademu wa Afrika Mashariki unawavutia sana. Wanawake wengi wa Kitanzania wameolewa au kuzaa na wanaume wa Kinigeria. Sidhani kuna ubaya wowote ila kinachogutua ni kule kuachwa wakilea watoto.

Mbali na sifa msela wetu alizongwa na moja.
“Nimempata bibi kwenu Tanzania.  Ninampenda sana. Niko tayari kujenga naye maisha. Lakini nieleze. Nimwamini au nisimwamini?”
Nini shida? Nikamjuza.
“Ah. Wewe umeshaishi kwingi. Umeshaishi na wanawake wa kigeni. Unafahamu tofauti za kitamaduni. Siongei Kiswahili. Siwajui wanawake wenu. Ninakunwa kidogo. Nilistuliwa namna mwanamke huyu alivyonichangamkia na sijamjua vyema. Tulikutana na kutoka mara moja mbili, ghafla tayari...  anataka arusi!”
Lakini si wanawake wetu tu. Nilipokuwa Marekani ya kusini niliwashangaa wanawake walivyonipapatikia. Kuna wakati miye na bendi yangu tulikwenda kupiga muziki Peru. Muziki wa Reggae. Kwa kuwa bendi  ilikuwa ya Wabrazili watupu na mimi pekee mgeni; wenyeji walidhani kwetu Jamaica au Marekani. Niliposema ni Afrika, mambo yakageuka pumba.
“Afrika bado mnakula wadudu? Mnakufa njaa? Bado watu wanalala kwenye nyumba za udongo na nyasi?”
Hamasa  ghafla ikapungua. Mabibi wakabadilika.
Peru  na nchi nyingine za Marekani ya Kusini zina matatizo ya umaskini na maendeleo kama Afrika. Wanawake wanapoona wageni hushangilia mbalamwezi na ukombozi.
Wanaume hali kadhalika.
Kila demu wa Kizungu anayetongozwa akija Afrika hulalamika lile lile. Jamaa wanataka urafiki wa haraka. Nahau “I love you” hutamkwa upesi upesi baada ya mkutano mmoja tu.  Ah na miye, nilipokuwa kijana sikukosa U- Bulicheka pia.  Kuna dada  wa Kiingereza alitaka nimpeleke kucheza dansi Kariakoo.  Nikampeleka. Sasa kwa vile alikuwa akivuta sigara, na miye nikajifanya navuta sigara. Sigara naiweka mdomoni moshi hauingii.  Hadi leo n’nashangazwa jinsi wanawake wa Kizungu walivyo wavutaji sugu wa sigara. Ukitaka cha mvunguni sharti uiname. Alipoomba somo la kupika chakula cha Kitanzania, nikampeleka Mwananyamala. Baada ya  mahusiano kuiva kama ule ugali aliojaribu kuusonga Uswahilini nikagundua siri ya sifuri. Mwenzangu alikuwa mtalii. Kaja tu kubadili mandhari. Miye nikajenga ghorofa ishirini na tano kichwani. Najua huyu wangu. Nafikiria ndoa na mbingu.  Alivyorudi sikumsikia tena. Miaka ishirini baadaye nilikutana naye kaoana na Mzungu mwenzake.

Kinachotakiwa kufahamika mosi kabisa, jamani, ni utamaduni.
Sisi tunatafuta mahusiano na wageni shauri ya shida. Wao wanataka mahusiano ya kweli na undani zaidi.
Kwa vipi?
Kwanza kabisa Watanzania hatuna tabia ya kuchanganyikana na watu wa mataifa mengine.  Neno sahihi la Kiingereza ni “networking”...Mmh.  Neno muhimu sana katika ulimwengu wa biashara na mahusiano ya kimataifa leo. Humkuti Mtanzania kaenda mahali pasipo starehe ya kunywa, kula au manufaa ya aina hiyo. Siyo tu nyumbani; Ughaibuni, vile vile. Inaweza kuwa shughuli ya maonyesho mathalani ya picha za camera,kuchora, vinyago au sanamu.  Mtanzania atakuuliza niende kuangalia picha nitapata faida gani? Kumbe hajui huko ndiko atakapokutana na watu wa aina nyingi na nyingine.
Sasa tunapogongana ghafla na mgeni, siku hiyo hiyo tukamwambia tunampenda sana; kwamba tuoane au atuchukue kwao, hatuelewi. Je tutaoanaje na hatufahamiani?  Je tuna mambo yapi na mangapi yanayopatana?
Hapa ndipo  penye kidari na supu.
Utamaduni ndiyo kiini cha kuwaelewa wanadamu ulimwenguni.
Sisi huzingatia fedha, uchumi, maendeleo na kutaka kitu kipya kitakachotuondoa gizani.  Mzungu huweka kazi mbele kwanza.
Nikiwa na dada mzawa wa Afrika Kusini,  tamasha la Kahawa, Uingereza,  Aprili 2013...

Biashara, nidhamu, mahusiano na mapenzi ya kweli, baadaye.
Wageni wengine wanaotoka nchi zinazoendelea kama Afrika Kusini, China, Nigeria, Marekani ya kusini na kadhalika wanao mseto wa hayo mawili juu.
Wapo pia wageni waongo na fedhuli wanaohadaa watoto, wanawake na vijana. Hawa utawajuaje? Huzionyesha noti za Dola shauri wanajua utaipapatikia kama samaki aliyeonyeshwa ndoana. Ndiyo janga lililowafika wanafunzi kadhaa wa vyuoni toka Uganda, Kenya, Rwanda na Tanzania wakalazimishwa kufanya sinema za ngono mwaka jana.
Ikiwa unatafuta huba la hakika, chunguza kwanza maana ya mahusiano. Jaribu kuelewa watu wa mataifa mbalimbali wakoje. Kama lengo lako ni kupata ahueni ya maisha haraka haraka utadhurika tu.  Ukitaka mapenzi ya kweli  yakubidi uwe mtambuzi wa “itikadi ya kupeana na kubadilishana.” Mwenzio anataka urafiki; je maana yake nini? Kaja kwako, je utamloga akupende au utajenga urafiki wa dhati kwanza?
Hata ikitokea mkaoana, mahusiano hayatodumu shauri hamjuani kiundani. Huyu anafikiria Dola; yule anawaza Papai Bivu.

-London, Ilichapishwa, Mwananchi Jumapili  17  Agosti,  2014.














                                                                                                        

1 comment:

  1. Wewe jamaa nakukubali sana, umenielimisha mambo mengi katika dunia hii kupitia makala zako katika gazeti la mwananchi, nakufananisha na shujaa wangu, mungu amrehemu kwasababu ametangulia mbele ya haki prof Leonard Shayo

    ReplyDelete