Thursday, 13 February 2014

UBORESHAJI LUGHA NCHINI WATEGEMEA SANA WANAHABARI NA UJUZI WA FASIHI -1




Mzee Adam Shafi, mwandishi nguli aliyeanza shughuli zake kama mwanahabari zamani. Leo lazima kumsoma. Umahiri wake wa lugha hausemeki. Picha na F Macha, 2007.


Wiki iliyopita kulikuwa na mdahalo na majadiliano moto bungeni. Lugha ipi itumike kufundisha watoto wetu mashuleni? Tatizo hili si ngeni kwa nchi zinazotumia zaidi ya lugha moja kimawasiliano. Wakati ninaishi Canada miaka iliyopita niliepuka matatizo kwa vile kitongoji nilichoshukia kiliongea zaidi Kifaransa. Nilikuwa nimekwenda kusoma  mwaka mmoja. Kawaida Mtanzania unapofika  nchi isiyozungumza Kiingereza- hubidi utumie wastani wa mwaka mmoja kujifunza lugha. Haya yamewasibu wanafunzi waliokwenda Urusi, Ujerumani, China, Cuba nk.
Mwandishi nikifanya shughuli ya kutengeneza bustani, Canada, mwaka 1995...picha na S Vanessa.

Canada inazo lugha mbili : Kiingereza na Kifaransa.  Bahati  yangu wakati nikifanya kazi magazeti ya Uhuru na Mzalendo,  nilijifunza Kifaransa na ingawa ujuzi wa lugha hiyo si mzuri kama Kiingereza, ilinisadia sana masomoni.

 Hali kadhalika nilipoishi  Marekani ya Kusini uelewa  wangu wa Kifaransa ulisaidia kujifunza upesi  Kireno na Kispanyola.  Lugha hizi (pamoja na Kitaliano) kama Kibondei, Kizigua, Kisambaa na Kidigo – au Kiswidi, Kidenish na KiNorwe-  ni  binamu hazipishani sana, ki-isimu.  
Mwandishi nikipiga kinanda (keyboards) na bendi la Os Galas, mjini Rio De Janeiro, Brazil, mwaka 1988. Picha na Clori Ferreira.

Uswisi iko hivyo pia.   Ukiwa Geneva ( mji wa makutano ya kimataifa) ni Kifaransa zaidi. Ukienda Zurich na Bern (kwenye masuala ya kibiashara) wahitaji Kijerumani. Lugha nyingine ni Kiitaliano na Kiromani. Wapo wananchi wanaoongea Kiingereza ndiyo (kama zilivyo sehemu mbalimbali za bara Ulaya) ila kufaulu shughuli zako vizuri shurti ujue Kijerumani na Kifaransa.
Kwa bara Afrika suala la maongezi ya lugha kadhaa si mastaajabu.
Kwanza  kwa sababu tulitawaliwa na wageni mbalimbali, pili kutokana na makabila mengi. Wastani wetu ni lugha mbili.  Kutokana na matatizo ya ukabila na ukinzani wa kisiasa serikali zetu ziliamua kutumia lugha za Kizungu juu ya lugha mama: Senegal kuna Ki-Wolof na Kifaransa lakini lugha ya Bunge, masomo, serikali na vyombo vya habari ni Kifaransa. Ukiwa mgeni kule si lazima sana ujue Kiwolof maana Kifaransa ndiyo lugha ya biashara na mawasiliano ya kimataifa. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire) hali kadhalika: Kilingala, Kifaransa na Kingwana (Kiswahili cha kule) ndiyo lugha kuu. Tunavyofahamu  muziki wa Ndombolo –tunaohusudu- huimbwa Kilingala. Lugha ya elimu ni Kifaransa. Matokeo kila mwananchi aliyesoma kidogo toka Kongo au Senegal  anakimanya Kifaransa vizuri. Wakenya hivyo hivyo. Ukiwa Mombasa, Lamu, Malindi , Nairobi na Kisumu-Kiswahili kimo- ila Kiingereza lugha ya mawasiliano ya wote, wenyeji na wageni.
Kinyume nasi Watanzania, Mkenya aliyesoma kidogo, (hata anayefanya kazi sokoni) hashindwi Kiingereza fasaha. Shule zao (Congo, Senegal, Kenya) hufundishia lugha za Kizungu.  
Bara Asia hali kadhalika.  Bara Hindi huzungumza Kipanjabi, Kigoa, KiUrdu na Kihindi. Ingawa lugha inayotumiwa na wananchi (kama tulivyoona Senegal na Kongo) ni Kihindi, bado  mawasiliano ya kimataifa huangukia Kiingereza.
Sasa tutafakari zaidi.
Nchi zinazotumia lugha zaidi ya moja leo hukubali lugha za Kizungu zitawale mawasiliano ya kielimu na kisiasa, kutokana “urahisishaji” wa kadhia.  Ila inapokuja katika “roho” na hisia za jamii, lugha mama ya wananchi hutumiwa mitaani, vijijini na majumbani. Kwetu “roho” hiyo ni Kiswahili. Mtanzania na Kiswahili ni kama kidole na ukucha.
Tangazo la biashara jijini London-linalocheza na ushairi, nahau na lugha kutafuta wateja wa mikopo ya nyumba...kama hukimanyi Kiingereza sawasawa utadhani wanazungumzia suruali za "jeans". Je, lugha huendelezwa vipi kama si kusoma fasihi?

Wasiokuwa na tatizo hili ni wazungumzaji wa lugha moja :  Waingereza, Wajerumani, Wafaransa, Wabrazili, Warusi, nk.
Sisi Watanzania tulifanya uamuzi wa busara zamani sana kukishika kiuno Kiswahili kiwe lugha ya taifa. Uamuzi huu ulisukumwa na kiongozi ambaye hakuwa tu na ujuzi wa lugha. Mwalimu Nyerere alitafsiri vitabu vya gwiji wa Kiingereza, William Shakespeare (Julius Kaizari na Wafanya Biashara wa Venice) kuja Kiswahili. Kama walivyo viongozi wa sasa ambao walikulia enzi Mwalimu akiwa Rais, huongea Kiingereza na Kiswahili fasaha.
Hadi mwaka 1984 Mwalimu alipotoa tamko la “Kiingereza ni Kiswahili cha Dunia,” Watanzania tuliongoza kwa Kiswahili. Vitabu vilipatikana madukani,  maktaba zilijaa mijini, wanahabari na wanasiasa waliijua lugha na Wakenya walituogopa. Waganda hawakupenda sana Kiswahili shauri kilitumiwa na wanajeshi kunyanyasa wananchi. Leo Ki-ganda kinakumbatiwa zaidi kuliko Kiswahili. Kenya  kama alivyodai  Mbunge wa Mgogoni (Kombo Khamis Kombo) wiki jana, inaongoza kwa Kiswahili. Wakenya wanachukua kazi za kufundisha Kiswahili duniani, hapa Uingereza wakalimani wengi wa Kenya (wakiwemo Wahindi wanapigania kazi hii).  Kampuni ya uchapishaji vitabu Nairobi (Sasa Sema- Longhorn) inaongoza kwa vitabu vya Kiswahili, Afrika Mashariki. Waandishi mahiri wa Kitanzania, Adam Shafi na Profesa Said Ahmed Mohammed wamechapa kazi zao Nairobi.  Mkenya, Profesa Ken Walibora anatoa kitabu kila mwaka cha Kiswahili- vitabu vyake vizuri. Tovuti na blogu kabambe la kihabari “Swahili Hub” liko Nairobi. Kenya inakwenda kasi kwa Kiswahili. Wakenya wanatuzidi kwa kuwa wanabidii, wanahangaika. Sisi je?
Kwa mtazamo wangu tatizo si lugha.
Tatizo letu ni ulimbukeni na kutojituma.
Kuna tatizo kubwa sana la ulegevu wa kiakili Tanzania. Mathalan inakuwaje Libya iliyopigana vita mwaka juzi, isiyokuwa na uongozi wa hakika imeshinda Kombe la Afrika la 2014?
Inakuaje Wachina wanakuja Tanzania wanajenga viwanda vya mafuta yanayoweza kulipuka na kuua mamia katikati ya makazi ya watu? Je, tuko macho au tunasinzia?
Jukumu liko mikononi mwa waelemishaji. Ukiacha wanasiasa na waalimu mashuleni muhimu ni wanahabari. Mwandishi anatakiwa kiwastani asome kitabu kimoja-hususan mkusanyiko wa mashairi au riwaya - kila mwezi. Je waandishi wangapi  wanajisomea vitabu vinavyohusu maisha ya mashujaa (au watu waliofanya mambo ya kuigwa) kama Mahatma Gandhi, Nelson Mandela, Barack Obama au aliyekuwa Waziri wa Fedha zamani, Edwin Mtei? Hata kama hukubaliani na fikra za mwandishi, je unachota wapi ufundi wako wa lugha? Kuna dhana iliyoenea eti kuwa mwanahabari ni mtangazaji wa miito ya serikali, starehe, udaku na michezo tu, basi. Mwanahabari (awe mwandishi, bloga, mtangazaji redioni au TV) ni msukuma jamii: ni kijiko,  sufuria na chumvi ya kuendeleza ujuzi wa lugha. Lazima (si hiari) , lazima, asome fasihi. Humo mna nahau, msamiati, misemo, nk. Fasihi kwa mwandishi ni shamba. Rutuba. Duka. Mwanahabari asiyesoma  hastahili kuifahamisha jamii yake lolote. Kwa kuwa Watanzania hatuna tabia ya kusoma vitabu, waandishi tuna jukumu la kusaidia kupunguza udhaifu huu. Tukihimiza na kuonyesha umuhimu wake, bila shaka itachangia wananchi wasiopenda kusoma, kutaka kusoma. Matokeo lugha zetu zitaboreka. Iwe Kiswahili au Kiingereza.
Tuendelee na mada wiki ijayo.                           

London, Ilitoka pia gazeti la Mwananchi Jumapili

                                                                             





                        




                                     






                                             

No comments:

Post a Comment