Kufuatana na kampuni maarufu ya
huduma za uhasibu, Ernst na Young, yenye makao makuu London, kuanzia mwaka
2,000 hadi 2015, Afrika iko katika
maendeleo makubwa kiuchumi. Ingawa sisi wenyewe
tunajihisi hali mbaya, ulimwengu mzima unalitegemea bara kwa mali asili na hali ya hewa.
Na hayakuanza leo. Baada ya mkutano
maarufu wa Berlin , 1884- chini ya uenyekiti
wa Mfalme Otto Von Bismarck- wakoloni walikuja, wakaondoka. Watawala wenyeji wakaendeleza uzi ule ule wa
kikoloni: kupora; wakishirikiana na wakubwa; wakihadaa kwa maneno maneno na
bunduki. Dunia nzima inatushangaa vipi, sisi matajiri wa mali ghafi, bado
tunategemea misaada; vita vya wenyewe kwa wenyewe, magaidi wanaua hadi
wanafunzi na watoto : Nigeria. Wanawake wanabakwa, Kongo, Sudan na Jamhuri ya
Afrika ya Kati. Kwa maskini asiye na
mali au nguvu za kisiasa, elimu tu ndiyo ubwabwa uliosalia.
Asili mia ndogo sana wanafikia
shahada ya mwanzo (Bachelors) au Diploma; na kidogo zaidi kuendelea shahada ya kati
(Masters), uzamili.
Kama Francis Magomeni(jina la
bandia) aliyekuja kusoma shahada ya uzamili (uchumi), London, karibuni.
“Nataka niwe kama akina
Profesa Lipumba, Profesa Palagamba Kabudi, Profesa Muhongo. Si lazima niwe Waziri, lakini
niwe fresh. Nchi yetu yahitaji wataalamu. Wakenya, Uganda, Burundi wanachukua kazi
zote, kwa vile sisi hatujasoma.”
Hayati Nyerere. Mwanaelimu na mwalimu maarufu kuzidi wote katika historia ya Tanzania.
Picha ya Wikipedia....
Changamoto, changamoto.
Alinigusa zaidi alipotaja
suala la waalimu na wahadhiri wetu.
“Waalimu hapa Ulaya tofauti
kabisa na nyumbani. Wanachapa kazi. Hawana makuu, wala kujidai dai. Kuna siku nilipewa kazi, lakini kutokana na presha
za maisha, nikababaisha babaisha nikampa tu mwalimu, nikidhani atamezea. Lakini
mmh. Nilipomlalamikia akatingisha kichwa.
Hakutaka kuongea zaidi. Nikasimama pale nikisubiri, ah wapi. Nimezoea
nyumbani. Waalimu, wako kinamna. Anaweza kukupasisha au kukuchukia tu,
akakufelisha.”
Kwanini akuchukie?
“Ah linaweza kuwa jambo la
kipumbavu kama labda una gari zuri, yeye hana. Au wewe ni demu kakuomba mchezo
ukamkatalia. Au labda unapiga piga sana makelele darasani, kila saa katika
simu. Jambo kubwa au dogo, ili mradi waalimu kule kwetu wanaweza kukuharibia maisha,
makusudi.”
Tofauti na huyu Mzungu wa
London ilikuwa ipi?
“ Baada ya kumsimamia pale
nikimsubiri, akaniuliza kama nimesoma alichokiandika chini kabisa ya karatasi
zangu. Kumbe mimi na Uswahili wangu, sikuwa nimesoma. Nikatazama nikakuta maneno
mazito sana. Akasema, sikujibu maswali. Na vitabu vinne nilivyotakiwa
kuvitafuta na uchunguzi niliotakiwa sikuufanya.
Akaniamuru niende tena maktaba, kuchimba. Hakuwa na kosa. Miye ndiye
niliyelipua. Nimezoea nyumbani. Mwalimu anaweza kukufanyia kila aina ya hila;
fanya vizuri, ufanye vibaya.”
Hii si mara ya kwanza kusikia
malalamishi ya aina hii. Je, kweli waalimu wetu nyumbani wanafanya watakavyo?
Francis Magomeni:
“Kwanza, tabia. Nimeshakaa hapa miezi mitano.
Nimechunguza. Huyu jamaa niliyemsema ni
profesa. Ukimwona njiani huwezi amini. Anafika, anafundisha, anasahihisha; anatoa
orodha ya maswali, anaelekeza vitabu, anaondoka zake. Ukifanya vizuri unapewa
maksi za kufaulu, ukifanya vibaya unanyimwa, lakini unapewa sababu. Huwezi
kumhonga au kufanya usanii. Utamwanzaje?”
Sasa kinachotisha, kimoja.
Itakuwaje waalimu wetu waitwe
“wafidhuli” ilhali takwimu zinatueleza mengine?
Wakati TANU ikidai Uhuru miaka 60 iliyopita,
idadi ya waalimu ilikuwa ndogo sana, na Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa kati
ya wachache. Mwaka 1970, elimu kwa wote
(UPE) ilikuwa asilimia 100. Ilipofika mwaka 1974 wakati namaliza kidato cha
sita; Azimio la Musoma, liliwapa wanafunzi wa kike kipaumbele. Kawaida baada ya
kidato cha sita tulitakiwa kwenda jeshini miezi 12, na kuajiriwa miaka miwili
kabla ya kuendelea chuo kikuu. Sera ya Musoma iliwapa fursa wasichana waendelee
moja kwa moja. Kutokana na azimio hilo la kimaendeleo, leo tunao akina mama wanataaluma
wa kujivunia baadhi viongozi kama Dokta Asha Rose Migiro, mwanadiplomasia
Mwanaidi Maajar (aliyekuwa Balozi Uingereza na Marekani), Balozi Radhia Msuya
(Afrika Kusini) na hata Waziri Profesa Anna Tubaijuka (ingawa yeye alisoma
kabla ya sera hii). Baada ya vita vya
kumwondoa Idi Amin, 1979, uchumi ulipoanza kuanguka, idadi ya waliosoma ilidondoka.
Kitwakimu, tunaambiwa na mtaalamu wa Haki-Elimu, Rakesh Rajani, mwaka 2000, “Idadi ya watoto walioandikishwa
iliporomoka hadi asilimia 77. Utafiti ulionyesha takriban zaidi ya nusu ya
watoto wote walikuwa hawamalizi shule ya msingi, ambapo waliotoka familia
fukara ndiyo wengi. Ubora wa elimu ambao haukuwa wa kuridhisha tangu awali
ulizidi kushuka kufikia moja ya viwango vya chini duniani.”
Mwanauchumi Francis Magomeni
anatujuza:
“Kutokana na hali ngumu ya elimu
nyumbani, waalimu wana nguvu ya
masultani. N’na dada yangu fulani tulimaliza naye chuo kikuu , 2008. Aliendelea
na kazi ‘afu, akaanza kusomea diploma ya
utawala; mimi nikawa natafuta vyuo vya nje. Ananiambia hasomi kwa amani.
Waalimu vijana wanawaandama wasichana. Anasema hakuna siku inayopita bila
kutongozwa. Ukikataa unafelishwa.”
Je, hawa waalimu
wanazingiatia maadili na kanuni za kufundisha? Francis Magomeni akacheka:
“ Kweli hayo ya huku hayapo
nyumbani. Kila siku tunasoma katika magazeti ya Uingereza namna mwalimu
kafukuzwa kazi au kapelekwa jela kwa kutongoza au kulala na mwanafunzi. Juzi hapa si kuna
yule mwalimu mwanamke aliyetangazwa kalala
na mwanafunzi wa miaka 17? Wakakutwa wakifanya ngono ndani ya gari? Si
ameachishwa kazi? Nyumbani, nyoo. Mpaka mtu atangazwe gazetini? Hutokea ndiyo
lakini nadra; ukilinganisha na mamia ya waalimu wasiokuwa na zile adabu na
heshima, nyinyi wenzetu mlizopitia enzi za Nyerere. Huyu sista ananieleza
waalimu kutongoza wanafunzi wa kike imekuwa nongwa kiasi ambacho wasichana wanadhani ukisoma unatongozwa na mwalimu!
Usipotongozwa si kawaida! Shule zimekuwa
sehemu za ukahaba? Wasichana watasoma wawe kama akina Profesa Tubaijuka na
Dokta Migiro kweli?”
Duu.
Magomeni alikuwa akipandisha
jazba.
“Waalimu wa huku si noma. Anafanya
kazi yake, anaondoka. Halafu
nimechunguza jambo moja kubwa sana. Watu wa huku hawajifaragui na elimu.
Unamkuta mtu ana udokta au uprofesa, lakini hakwambii wala haweki cheo mbele. ”
Nikatafakari aliyosema Bwana
Magomeni. Nikawazua kuhusu taaluma zinazotegemewa na mwananchi mitaani. Askari asipotulinda, tutaishi kwa amani kweli? Dereva akilewa au
kuvuta bangi kazini, si hatari kwa abiria? Je, mganga akikosea kumpa mgonjwa
dawa, si kifo? Mwalimu ni mzazi wa pili wa mtoto. Kama walivyo waganga, madereva,
wanausalama, mwalimu ana jukumu kubwa sana !
-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili, Januari 25, 2014
No comments:
Post a Comment