Tanzania ndiyo imemaliza vita kumwondoa Jemadari Idi Amin Dada ; maisha magumu maana serikali imetumia mabilioni ya shilingi kununua silaha kujenga jeshi imara kuwasaidia Waganda. Bidhaa adimu madukani. Hata chakula kinacholimwa nchini (mathalan unga) kazi kukipata. Utata.
Licha ya kitatange na mahangaiko maelfu ya wakimbizi wamekaribishwa nchini toka Afrika Kusini, Angola, Namibia na hiyo Uganda yenyewe. Kisiasa Watanzania waungwana sababu ya uongozi wa Mwalimu Nyerere aliyeujua wajibu wake wa kijadi kwa Waafrika wenzetu. Ni kipindi hiki ndipo miye na wenzangu watatu tulipounda bendi ya mseto wa fasihi na muziki tukaiita “House of Africa.” Ilikuwa vigumu kumpata mwanamke maana enzi hizo jamii yetu iliwabeza kina dada waliofanya sanaa. Imetolewa pia safu ya "Kalamu toka London" kila Jumapili, gazeti la Mwananchi:
Waliitwa mabahaluu, wavuta bangi, machangu doa; kuimba jukwaani hakukuwa na heshima wala ajira kama walivyo Kizazi Kipya leo...Wakati sisi tukihangaika, Anna Lukindo alikuwa akionyesha mavazi hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam siku za wikiendi. Kikazi aliajiriwa na kampuni ya kusanifu nyumba barabara ya Mkwepu. Bado mdogo ana miaka 19, lakini mchapa kazi ile mbaya.
Anna Lukindo akiwa kazini. Anayevalishwa ni mwanamitindo, mpiga picha na mwanabloga, Jestina George . Picha na See Li.
<--more--!>