Tanzania ndiyo imemaliza vita kumwondoa Jemadari Idi Amin Dada ; maisha magumu maana serikali imetumia mabilioni ya shilingi kununua silaha kujenga jeshi imara kuwasaidia Waganda. Bidhaa adimu madukani. Hata chakula kinacholimwa nchini (mathalan unga) kazi kukipata. Utata.
Licha ya kitatange na mahangaiko maelfu ya wakimbizi wamekaribishwa nchini toka Afrika Kusini, Angola, Namibia na hiyo Uganda yenyewe. Kisiasa Watanzania waungwana sababu ya uongozi wa Mwalimu Nyerere aliyeujua wajibu wake wa kijadi kwa Waafrika wenzetu. Ni kipindi hiki ndipo miye na wenzangu watatu tulipounda bendi ya mseto wa fasihi na muziki tukaiita “House of Africa.” Ilikuwa vigumu kumpata mwanamke maana enzi hizo jamii yetu iliwabeza kina dada waliofanya sanaa. Imetolewa pia safu ya "Kalamu toka London" kila Jumapili, gazeti la Mwananchi:
Waliitwa mabahaluu, wavuta bangi, machangu doa; kuimba jukwaani hakukuwa na heshima wala ajira kama walivyo Kizazi Kipya leo...Wakati sisi tukihangaika, Anna Lukindo alikuwa akionyesha mavazi hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam siku za wikiendi. Kikazi aliajiriwa na kampuni ya kusanifu nyumba barabara ya Mkwepu. Bado mdogo ana miaka 19, lakini mchapa kazi ile mbaya.
Anna Lukindo akiwa kazini. Anayevalishwa ni mwanamitindo, mpiga picha na mwanabloga, Jestina George . Picha na See Li.
<--more--!>
Kwa kuwa Anna alitoka familia ya heshima ndugu zake walituangalia kwa macho manne; hawakutaka tumharibie binti maisha yake. Anna alipojiunga na “House of Africa” aliwasili na karata nyingi. Kwanza kwa kuwa alikuwa mpenda mavazi yaliyonakshiwa vyema; tukapata moyo; kila tukiingia jukwaani, mbali na nyimbo na mashairi, tukahakikisha tunavalia nguo zilizotengenezwa Tanzania za pamba, vitenge na rangi rangi. Pili akashauri jina la bendi liwe la Kiswahili yaani Sayari. Ilikuwa 1981. Kuanzia hapo tukaitwa Sayari.
Miaka mingi imepita, siku hizi Anna Lukindo kahamia Uingereza ambapo keshafuzu shahada ya BA (hons) katika usanifu wa mavazi, toka chuo Kikuu cha Middlesex. Tarehe 8 mwezi huu alifanya maonyesho ukumbi wa Alto Private Members Venue, London. Mada ilikuwa rangi na Anna alisanifu matumizi ya kamba katika nguo na wajihi wa wavaaji.
Anakumbusha : “Nimejishughulisha na ubunifu kwa muda mrefu. Nakumbuka nilipojiunga mashindano ya ubunifu wa mavazi pale hoteli ya Kilimanjaro zamaaani...(anacheka, maana zamani ni hiyo miaka ya 1980-81) nikanyakua ushindi wa kwanza.”
Ukimuuliza kwanini anapenda sana mavazi na sanaa atakueleza kuvaa ni muhimu kwa kila mwanadamu, kwamba ni kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Toka akiwa mtoto alipenda kubadilisha vitu mbalimbali hata kama sio nguo. “Mama yangu naye alikua alikua ni mwanachama wa YWCA na walinihusisha katika shughuli za monyesho ya mitindo.”
Kuendeleza mada hebu tumchimbe Anna atufafanulie nini faida ya mavazi na usanifu wake katika jamii? Kwanini kila kukicha vyombo vya habari hasa nchi zilizoendelea haviishi kutangaza maonyesho ya fani hii? Kwanini vijana wengi ( Bongo pia) wanapania sana kuonyesha mavazi (modelling)?
Anna: “Kila mtu anapenda kuvaa vizuri na kupendeza. Nikichukulia mfano wa YWCA ni chama kilichoinua akina mama kwa shughuli mbali mbali na kuuza nguo zao kupata faida ya kusaidia vyama mbali mbali vya jamii Tanzania. Naamini wengi walifaidi kwa kupewa kazi na kufundishwa namna ya kujitegemea kwa mfano kufundishwa kushona nguo.”
Lakini kipaji, ubunifu na mapenzi havitoshi katika uhalisi wa ulimwengu leo. Mbali na kwamba Anna kufuzu shahada chuo kikuu cha Middlesex dunia ya mavazi imelowana mashindano. Washoni na wapambaji ni wengi sana Uzunguni. Je, ni rahisi kwake kama Mwafrika ?
“Ugumu upo, hasa kwa sie wenye ngozi nyeusi, huo ni ukweli. Kitu cha kwanza kinachonishangaza ni ubaguzi ulio kuweko baina ya sisi wenyewe ; hilo linanishangaza na kuniuma kuliko vyote. Lakini mimi nina mwelekeo wa kutokunasa kwenye mawazo hayo na kujitahidi sana kupigana kwa kuonyesha ubunifu wangu.”
Ubunifu na upambaji wake Anna Lukindo kimavazi umeanzia katika macho yake yanayoona uzuri na sanaa katika kila kitu. Mfano ni picha hii aliyopiga bustani ya maua ya Kenwood mjini London.
Kusoma, kujiamini, kipaji vyote havitoshi. Yabidi kufanya maonyesho. Akiwa bado chuoni, Middlesex, Anna alifanya maonyesho madogo madogo na toka amalize masomo mwaka jana keshafanya maonyesho matatu. La karibuni anafafanua “lina umaarufu wake jijini maana liliandaliwa na kampuni inayojulikana mjini London, yaani LGN.”
Labda msomaji uliyeko Bongo utadhani kutokana na maonyesho machache Anna Lukindo keshatajirika, ana nyumba kubwa na gari. Bado. Bado usafiri wake mjini hapa ni wa baiskeli na bado hajahama nyumba ya kupanga ambayo amekuwa akiishi na familia yake kwa miaka mingi.
Anna : “Kwa sasa nimemudu kupenyeza sehemu ambazo sikutegemea kufika, lakini, lengo langu ni kufanya kazi kwa dhati nina uhakika kwa sasa hivi kazi iko ya kujenga msingi. Namshukuru Mungu kwa kunifungulia njia na ninaamini kwa rehema zake, nitafika kule ninapopataka.”
Pamoja na kuwa msanii wa dhati Anna Lukindo ni pia mcha Mungu anayehudhuria ibada kila Jumapili. Juu ya hapo Anna ni mzalendo fika anayefikiria sana hali na mustakabal wa nchi yetu ya Tanzania. Mpamba mavazi huyu anayetumia jina la Anna Luks kazini ni mmoja wa waasisi wa Chama cha wanawake wa Tanzania Uingereza (TAWA) kilichoundwa mwaka 2006. Anasema walianzisha TAWA “kujaribu kuunganisha akina mama wote waishio Uingereza na kupeana changa moto kwa mambo mbali mbali yatakayoboresha, maisha ya akina mama Wakitanzania.”
Anna ( wa nne kulia) akiwa na wake wenza toka jumuiya ya TAWA London. Toka kushoto, Mariam Kilumanga, Uli Kyusa, mkewe Balozi wa Tanzania, Uingereza, Bi. Joyce Kallaghe.
Picha ihsani ya Annaluks Blog.
Anna ( wa nne kulia) akiwa na wake wenza toka jumuiya ya TAWA London. Toka kushoto, Mariam Kilumanga, Uli Kyusa, mkewe Balozi wa Tanzania, Uingereza, Bi. Joyce Kallaghe.
Picha ihsani ya Annaluks Blog.
Mapenzi yake kwa wanawake wenzake huonekana anavyokuuza utamaduni wa mavazi ya wanawake wetu kupitia Kanga. Anasisitiza Khanga ni kitu cha kujivunia maana ni “nembo ya Waswahili na Watanzania.”
Ila, anauliza ni nani anayeitengeneza? Na je, kiwanda ni kipi? “Je kiko mikononi mwa wananchi au wageni? Hili ni suala zito linalohitaji kichwa chake pekee,” anahimiza.
Wakati matayarisho ya sherehe za miaka 50 yakiendelea inategemewa kwamba Anna ataonyesha kazi zake kujenga wajihi wetu huku Ughaibuni. Anakumbusha kwamba “ kuna haja ya kutumia sherehe hizi zaidi kama muda wa kukusanya hela na kuangalia masuala muhimu mfano Umeme, Maji na Elimu; kwa kweli tumerudi nyuma vibaya sana.”
Bila shaka miaka ya baadaye tutategemea kumwona zaidi mchapa kazi huyu mbunifu. Habari zaidi tembelea blog lake : http://annaluks.blogspot.com/
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/14070-anna-lukindo-taswira-ya-wabongo-london
No comments:
Post a Comment