Wakati Mwalimu Nyerere
akiwa Rais wetu, alisemwa vibaya, aliogopwa, alitaniwa. Ni ajabu namna leo, (nusu
karne baadaye) anazungumziwa kwa staha, tija na hata kupendekezwa aitwe
mtakatifu. Asiye na hatia au kosa. Sisi wanadamu wanafiki sana. Mtu akiwa nasi
tunamsuta. Akishatutoka tunamvalisha kila suruali, viatu, bangili na kofia za
jaha.
Nakumbuka tukiwa bado
sekondari, tulisafiri sana Nairobi kutembea. Miaka hiyo ya Sabini Kenya ilifananishwa
na Ulaya. Majuu. Nairobi ilijaa klabu
nzuri nzuri, mavazi ya Kizungu, sinema tele zikiwemo za ngono. Tuliwaona ndugu
zetu wa Kenya wenye bahati sana.
Tulimsikia Rais wao, Jomo
Kenyatta akisema: “Kuleni matunda ya Uhuru...”
Baadaye nilipokuwa mtu
mzima, nikasafiri Ulaya. Kwa mara ya kwanza nikaona sinema ya ngono, mwanzo hadi mwisho. Ilikuwa kioja. Sikuziona
nikiwa shuleni, ( tuliposafiri Kenya) shauri ya masharti ya kiumri. Ziliitwa
sinema za X. Yaani za watu wazima tu.
Sasa nikiwa Ughaibuni mtu
mzima niliyeshapitisha miaka 25 sikuzuiwa. Niliufurahia uhondo uliokatazwa na
Baba wa taifa na serikali ya TANU na CCM.
Lakini baada ya “kipya
kinyemi” kwisha, nikazoea, nikazikinahi.
Nilianza kugundua watu walioangalia filamu hizo walikuwa wanaume wapweke
wasiokuwa na wapenzi. Kila mtu alikaa peke yake, mle giza la sinema; akijishika
shika; wengine wakinywa pombe kisirisiri. Kifupi waliotazama michezo hii
walikuwa wapweke wenye matatizo ya kisaikolojia. Watu na wake zao
hawakuhudhuria sinema za ngono. Ndiyo walikuwepo wapenzi walioziangalia. Mmoja
mmoja na mkewe, lakini wachache...
Ziliitwa “pornography.”