Jumapili iliyopita wanawake
watatu wa Kihabeshi walishinda
mbio za Marathon hapa London. Zilishirikisha wakimbiaji 38,000, wengi wananchi wa kawaida ( wasio wanariadha wa kulipwa); mataifa mbalimbali. Baada ya ushindi “
wanariadha hawa wenye fahari” walipeperusha bendera rangi kijani, manjano na
nyekundu. Bendera hii ya Ethiopia iliyosanifiwa mwaka 1897 imekuwa kielelezo maarufu cha Umoja wa Waafrika na
watu weusi duniani zaidi ya miaka mia moja sasa. Wekundu ni nguvu na imani, kijani ardhi na
manjano, kanisa. Tufasili hili kifupi.
Mwanamuziki maarufu wa Reggae kutoka Ivory Coast, Alpha Blondy. Picha ya Reggae Ville.
Ethiopia na Liberia ndiyo
mataifa pekee Afrika ambayo hayakutawaliwa na Wazungu au Waarabu. Sifa na
fahari hii iliwapa motisha watu weusi waliochukuliwa utumwa Ughaibuni na kuiita Ethiopia
(Abyssinia) taifa la Wafalme. Kanisa (rangi njano ya bendera) lina historia
ndefu Ethiopia. Ingawa mna madhebehu mengine,
Ukristo umejizatiti Ethiopia toka karne ya kwanza. Kabla hata ukoloni haujabuniwa
au Uislamu kukanyaga barani.
Wiki mbili zilizopita
Wahabeshi 30 waliuawa na magaidi wa ISIS
shauri ni Wakristo. Akilaumu mauaji hayo yaliyofanyika Libya, Papa Mtakatifu
Francis, alimtumia salamu mkuu wa kanisa
la Tewahedo, Abuna Matthias. Kanisa hilo ndilo lenye wafuasi wengi Ethiopia.
Tukio la tatu lililowakumba
Wahabeshi tulilitaja juma lililopita. Kati ya maelfu ya wakimbizi waliotaabika
bahari ya Mediterranean walikuwepo raia
wa Ethiopia. Taifa hili la kale halikutawaliwa na wageni shauri jeshi lake la kifalme
lina zaidi ya karne 20 sasa. Sifa hii ndiyo ilichangia kuanzishwa makao makuu ya Waafrika mjini Addis Ababa
mwaka 1963. Umoja ulifanikishwa na
viongozi Kwame Nkrumah (Ghana) Mwalimu Nyerere (Tanzania), Kenneth Kaunda
(Zambia), Ben Bella (Algeria), Ahmed Sekou Toure (Guinea) na Mfalme Haile
Sellasie (Ethiopia). Bahati mbaya leo ukitafiti maandishi mengi wanaotajwa ni
Nkrumah na Haile Sellasie tu. Yabidi kizazi kipya kifahamu historia ya kweli.
Tufukue zaidi.
Hadhi ya Ethiopia na bendera ya Ethiopia ndizo zinazojulikana kama
rangi za Rasta.
Aliyeongoza msisimko huu ni
kiongozi wa watu weusi, Marcus Garvey. Marcus Garvey alisisitiza imani ya
kuupenda Uafrika nchini Marekani, visiwa vya Karibian na Uingereza. Bw Garvey
aliyezaliwa Jamaica mwaka 1897, alikuwa mwanahabari, mfanya biashara, mchapishaji
vitabu na mzungumzaji mzuri. Alianzisha chama cha kuwarejesha watu weusi Afrika
kwa meli aliyoiita Black Star. Kwa miaka hiyo ya 1920 – 1940 alikuwa jasiri na
mwanamapinduzi thabiti aliyewasisimua viongozi tosha mathalan, Jomo Kenyatta,
Kwame Nkrumah, Malcolm X, Nelson Mandela, nk.
Baada ya mapambano makali, alihamia London alipofariki 1940 akiwa na
miaka 52. Athari ya kazi ya Marcus Garvey ni kubwa sana katika historia na
harakati za watu weusi.
Enzi Marcus Garvey akipigania
haki hizi, kundi la Wajamaika walioipenda na kuiheshimu Ethiopia lilianzisha
dini ya Rastafari mwaka 1930. “Ras” ni
kichwa (au aliyeteuliwa) kwa Kimhariki (lugha ya Kihabeshi). Kimaudhui ni mfalme au mtoto wa mfalme. “Tafari”
inatokana na “Tefar” ambayo kwa Ki- Amhariki
ni “anayeogopewa”, au “kustahiwa”...Urasta pia hutumia neno “Jah” toka Jehovah – Mungu kwa Kiebrania, lugha ya Wayahudi. Marasta wanaamini Haile Sellassie anatokana na
damu ya Yesu Kristo; mrithi wa kizazi hicho.
Fikra za Marcus Garvey na
Urastafari vilipewa uzito na muziki wa
Reggae, ukiongozwa na bendi maarufu ya The Wailers. Bendi iliasisiwa mwaka 1963
na Peter Tosh (aliyefariki 1987), Bunny Wailer (yungali hai) na Bob Marley
(fariki 1981). Reggae ilichanganya imani
ya Rastafari (kutukuza Uafrika), mafundisho ya Marcus Gavey ( muungano wa Waafrika) na harakati za walala
hoi.
Mahadhi ya Reggae na Rasta yalitukuzwa na masharti rasmi mfano kutokula
nyama, kusoma Biblia,kutokata nywele, mazoezi
ya mwili, amani, nidhamu na kuvuta jani (herb) liitwalo bhang (Kihindi),
marijuana (Kispanyola, tamka marihuana) na
spleef (Kijamaika, tamka splif).
Si kila mfuasi wa dini ya
Rastafari huvuta bangi. Mutabaruka, mshairi mashuhuri wa Reggae (asiyevaa viatu,
asilani) havuti bangi, hanywi pombe, hali nyama. Mjamaika, Mutabaruka hutumbuiza
kwa muziki, redio na duka lake la vyakula vya afya.
Zaidi ya miaka arobaini sasa Urastafari
umezagaa duniani. Mbali na wanamuziki, yapo mambo ya kifani mathalan namna
Marasta wa Kijamaika walivyobadili nywele za msokoto (“locks”) kwa kupachika
neno “dread” yaani “kuhofia” jambo
fulani.
“Dreadlocks” ni nahau
inayoendeleza mapigano ya Marasta na ukombozi dhidi ya mateso ya maskini,
wanaoonewa na weusi duniani. Kwetu
Uswahilini hutumia neno “nywele za rasta”
kufasiri (au elezea) mtindo. Ukweli “kusokota nywele” si jambo jipya. Nywele za mtu mweusi kiasilia zimejisokota, na
zisipochanwa, zikiwa ndefu hugeuka “kuwa Rasta.”
Mau Mau wa Kenya, waliopigana dhidi ya wakoloni
wa Kiingereza kati ya 1952 hadi 1956, aliponyongwa kiongozi wao shupavu, Dedan
Kimathi, walikuwa na nywele hizi. Walichofanya wanamuziki wa Reggae na Marasta
ni kutukumbusha tu asili yetu. Urasta si dawa za kulevya, au wenda wazimu. Mtanzania unapoacha nywele chafu, huku ukivuta
bangi na kufanya mizaha inayowatisha au kuwahasimu wanajamii wenzako, kama
kutukana wazee katika mabasi au kukaba usiku, hufuati Urastafari. Urastafari ni ukombozi, kujitambua, kujipenda, elimu na
maendeleo ya jamii.
Tupeane mfano muafaka?
Mchimbe mwanamuziki maarufu wa Reggae, Ivory Coast, Alpha Blondy.
Karibuni kaanzisha kituo cha redio mjini Abidjan. Malengo ya “Radio Alpha
Blondy FM, 97.9” ni kutumbuiza muziki wa
Reggae na vichekesho, kutoa ajira, na kuhimiza kusoma vitabu.
Kila juma, Alpha Blondy
husoma kitabu kilichoandikwa na Mwafrika.
Alipohojiwa na runinga ya Ufaransa, TV5, mwezi
Machi, Alpha Blondy (aliyeingia uwanja wa muziki
mwaka 1982 na kibao, Brigadier Sabari) alisisitiza hana malengo ya kisiasa :
“Kuna mtu aliwahi kuandika ukitaka kumficha
mtu mweusi habari iweke ndani ya kitabu. Sababu sisi weusi hatupendi kusoma. Nimeamua kutumia
redio sababu kinyume na runinga ambayo ni ya kutazama, inakubidi kusikiliza na
kuzingatia maneno. Azma yangu ni kujenga mapenzi ya lugha, fasihi na vitabu.”
Hii ni ithibati adhimu ya Urasta na hulka zake.
Ikiwa unaendekeza bangi, matusi hadharani, kupiga watu, kupora na utovu wa nidhamu; ndugu yangu Mwafrika, tafakari
na tafiti zaidi.
-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili, Mei 3, 2015.
No comments:
Post a Comment