Mwafrika mwenzangu umegundua
nini jipya miaka ya karibuni?
Ukichunguza utaona maradhi
yaliyokuwa yakiwang’ong’a wazee, leo
yanaua vijana. Ugonjwa wa moyo, utasa, mapafu dhaifu, uume tata, uchovu kila mara bila sababu, kisukari, chafya
upitapo kwenye vumbi, magari au moshi wa sigara; kiharusi, nk. Maumbile na
mazingira yana sheria kali sana. Tusipoyaheshimu hutufunza adabu. Je, kweli
tunayaona? Maana sikio la kufa halisikii
dawa...
Matokeo nini?
Leo tumejenga tabia ya lawama kwa wengine
kuhusu matatizo yetu. Hatuisikilizi miili yetu. Wanyama tu ndiyo bado wanaheshimu
maumbile. Siku Tsunami kubwa la mwaka 2004 lilipoutingisha ukanda mzima wa nchi
za bahari ya Hindi, wanyama wengi walikimbilia milimani au nyanda za juu
kujiokoa. Wanadamu wasiojali wala kuhisi tena maumbile walibaki kama vigogo (vyenye
kiburi cha teknolojia) wakisubiri kiama kiwakute. Tumepoteza hisia asilia
tulizozawadiwa na Mwenyezi Mungu.
Madhila yetu wanadamu
yametokana na sisi wenyewe kutokubali nguvu tulizo nazo. Imezuka desturi ya
wahubiri kuzusha eti huu mwisho wa
dunia. Ukweli haya yamesikika kila karne. Hakuna kipindi chochote cha historia ambapo sisi wanadamu hatukupiga kelele kuwa
tamati ya sayari yetu inawadia. Hutokana na kushindwa kujua au kuona kiini cha
matatizo yetu. Tunaposhindwa kuelewa tunabaki “kuotea” alamsiki ya kila kitu,
kukata tamaa na uhai.
Kila karne ina matatizo na
raha zake.
Starehe ya karne ya 21 ni
kukua kwa teknolojia ya habari na
mawasiliano. Shida ni namna teknolojia
hii inavyotumika. Siku hizi pamezuka
majambazi wa mtandaoni (“hackers”) wanaotumia msitu huu ( wa raha) kuhujumu.
Siku chache zilizopita, mathalan, shirika la upelelezi Marekani, FBI, lilitangaza
lilivyomtia mbaroni mjuzi wa usalama wa kompyuta , Bw Chris Roberts. Bw Roberts alitumia tarakilishi yake
kuingilia mitambo ya ndege na kuipaaza
kiupande upande mapema mwaka huu. Alishawahi pia kuingilia ndege kadhaa kati ya
2011 na 2014.
Mwezi jana magaidi wa Mashariki ya Kati
waliingilia moja ya idhaa za televisheni za Ufaransa (TV5 Monde) na kuiteka
(kupitia kompyuta) kwa siku kadhaa.
Lazima tuwe macho na
majambazi wanaotumia ujanja huu kutuhadaa. Eti tumeshinda bahati nasibu na
mamilioni ya fedha . Nadhani msomaji unayetumia barua pepe umewahi kupokea
nyaraka hizo. Teknolojia hii nzima imeanzia kwa Mzungu. Na hapo hapo...
Iko chuki inayozagaa Afrika
kwamba kutoendelea kwetu ni kosa la Mzungu. Hatukatai Wazungu wameua wanadamu wengi
sana kwa miaka 500 sasa. Wiki iliyopita safu hii ilizungumzia ustaarabu wa
demokrasia ya Wazungu; lakini hawa hawa Wazungu walikuwa wakichinjana wakati wa vita vyao vikuu vilivyokwisha mwezi
Mei 1945 na kusababisha vifo milioni 80. Leo Wazungu wamejifunza. Mtoto mdogo huwa haogopi
kijinga cha moto hadi kinapomchoma. Waafrika tuliteswa na utumwa. Hadi leo
makovu yapo. Waafrika tunapitia majanga yaliyokwisha kwaruzwa na Wazungu. Bado tunalaumu, bado tumeathirika;
wengine tuna vinyongo...
Vinyongo vimetuelemea;
tumejaa maluwe luwe; hatuoni, hatutathmini sawasawa. Tunasahau ukweli mmoja,
lakini.
Siyo sisi tu tulioteswa au
kutawaliwa. Kila taifa lina historia ya kunyanyaswa. Wachina walitawaliwa na Wajapani;
Waingereza walitawaliwa na Warumi ( Italia); Waarabu walitawaliwa na Waturuki; Wahindi
walitawaliwa na Waingereza, nk.
Usiku mmoja miaka zaidi ya
ishirini iliyopita, nilikaa na kundi la Wazungu baada ya kuwatumbuizia ngoma.
“Vipi Tanzania?” Wakaniuliza.
“Kwema tu.”
“Kwanini ulihama?”
“Kutafuta maisha.”
“Nimewahi kufika Tanzania.
Kuzuri. Wenyeji wema sana.”
“Kweli.”
“Mbona unaishi huku? Baridi
kali...”
“Mbona Tanzania pia kuna
wenzenu, wamehamia, wanapahusudu? Kila mtu anaruhusiwa kwenda atakako.”
“Lakini ni vigumu zaidi kwenu
Waafrika kuishi hizi nchi zetu.”
Gumzo likaendelea. Ghafla
nikawachamba.
“Nyinyi lakini mna dhambi
sana. Mmesababisha vita kila mahali. Ukoloni, ukoloni mambo leo, uporaji mali...”
Mwanamke mmoja wa makamo,
nywele ndefu, nyeupe kama sungura, sigara mkononi; akatingisha kichwa.
“Unajua huu ukoloni,
ukiuchunguza ulikuwa ni sera tu ya watawala. Uingereza ni jamii ya matabaka.
Walioshika madaraka walikuwa wanaume wachache waliotoka familia za kitajiri.
Hata wanasiasa wa sasa ni milionea
wachache. Humwoni rais au waziri mkuu yeyote duniani maskini...”
Nikanyamaza. Ukipewa somo
kubali. Mwanamke wa Kizungu akasambaza moshi wa sigara lake.
“Huu ukoloni ulikuwa siasa ya
wachache. Wachache hao waliohodhi dhahabu, farasi, bunduki, majambia na meli
ndiyo walioamua kila kitu. Wachache hawa
hawa walikwenda zao nje wakapora makoloni, wakatwaa ardhi za wengine, wakaua,
wakaiba madini. Sisi wanawake tulifuata tu mkumbo. Enzi hizo wanawake tulifanya
kila mwanaume alichosema. Ukombozi wa kina mama hauna zaidi ya miaka 30. Maskini
hawakuwa na la kusema. Ukoloni si Uzungu. Ulikuwa uamuzi wa tabaka dogo la
waliojiweza.”
Kimya kikatua pale. Nikabaki nikitafakari. Iko siku nilikuwa
warsha fulani ya lugha, hapa London. Waafrika hupandwa sana na jazba kuhusu
mada hii. Ukaanza mjadala kuhusu lugha za Kiingereza na Kifaransa zinazotumika
zaidi barani. Kwamba ni lugha za kikoloni. Baada ya malumbano makali tukakubaliana
kuwa lugha haina kabila au rangi. Lugha ni chombo tu cha anayeitumia.
Wenzetu Wachina, Wajapani,
Wahindi na wengine bara Asia wameshaachana na lawama. Wameachana na vinyongo
kiasi ambacho Wazungu sasa wanajiuliza mbinu za kukabiliana nao kiuchumi. Hii
ni kwa vile wenzetu ni wachapa kazi. Hawapotezi tena muda kupiga domo. Sisi
bado tunawashtaki kunguru, mwewe na yange yange, walioshapaa zao.
Juu ya lawama tumeyaacha ya
kwetu tunaiga ya wengine. Mosi kabisa, tumbo. Chakula kinachopendwa na wengi
siku hizi si tena ubwabwa, ugali, ndizi au chapati ila viazi Ulaya vya
kukaanga. Asili yake ni hawa hawa wakoloni wetu. Waingereza. Chips kwa samaki. Chips
kwa kuku. Mafuta yaliyoko vyakula visivyo vya asili yetu yanatuvimbishia
vitambi na unene unaotuumiza kwa visukari na viharusi.
Wazungu waliotuletea teknolojia
wameshagundua dhila lake. Wanarejea siri
ya maumbile. Leo Ulaya na Marekani utakuta vyakula vingi vilivyojazana Afrika vinauzwa aghali maduka ya afya. Viazi vitamu, madafu, maparichichi, komamanga, mibuyu, Alo Vera,
upupu, nk. Mzungu anatafuta bidhaa ambazo sisi tumezitupilia mbali. Anajua
faida ya kuzila ni haiba (na siha) ya mwili wake.
Tumalizie mada juma lijalo.
-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili, Mei 24, 2015.
No comments:
Post a Comment