Yupo Mwingereza mmoja maarufu sana aliyetimiza miaka 40 mwezi jana.
Huyu jamaa ana kipindi chake katika TV anachodondoshwa mwituni, jangwani au vichaka vya sehemu mbalimbali za dunia na kuachwa. Hukaa bila chochote bali kisu kikali, mfuko mdogo na nguo alizovaa. Kuna wakati aliachwa pori moja la Zambia. Huko alizingirwa na wanyama, mito, chemchemi na nyika tupu. Alilala juu ya mbuyu. Chakula kilikuwa wadudu, nyoka na maji ya mvua. Na hii tabia yake ya kula chochote anachokiona nyikani kiwe buibui, chura, mchwa, asali, nyungunyungu,mbegu, matunda, madafu, majani, panya, fuko au ngiri ina malengo na mafunzo.
Mosi anajaribu kuonesha namna
wanadamu tunavyopaswa kujua kuishi (na kumudu) bila kukata tamaa iwapo majanga
yakitutokea au hakuna namna. Pili, anasisitiza wanadamu, (hususan Wazungu) tumeichangamkia
teknolojia tukapoteza ubunifu, tukawa wavivu na waoga wa mazingira. Tatu, huelekeza
kutokata tamaa, kujitegemea na kuwa wajanja pale shida yeyote inapojitokeza. Zamani nikiwa jeshi la kujenga taifa (JKT)
tulifundishwa ujuzi huu uliobatizwa nahau : “Ujanja wa Porini”...
Jina la huyu “mbabe”
anayezidi kupendwa na hasa watoto na vijana ni Bear Gryllis.
Ujanani, Bear Gryllis (pichani )
alikuwa askari wa kikosi maalum cha
Uingereza.
Bear Gryllis. Picha ya Wikipedia
Nchi mbalimbali duniani huwa na jeshi la
kawaida linalolinda taifa; na ndani
huteuliwa askari wachache makini zaidi, mashujaa, majasiri waliozamia mbinu za
kivita, wenye uwezo na akili ya hali ya juu. Vikosi hivi maalum huteuliwa kupambana
na mambo magumu ya kitaifa, mathalan ugaidi au ujambazi usio wa kawaida.
Kwa Wamarekani wanaitwa “Delta Force”, ilhali
Israel ni, “Sayeret Matkal.
SAS (Special Air Service) ya Waingereza ndiyo
mwasisi wa kikosi cha namna hii na wameigwa dunia nzima. Asili ya SAS ilikuwa
kupambana na jeshi la Wajerumani wakati wa Vita
vya Dunia vilivyokwisha 1945.
Kikosi hicho cha wachache kilipambana na maadui kikiwa na kila
aina ya silaha na mapigano na kilidondoshwa kwa ndege (parachuti) na kufanya
maajabu. SAS ilichangia sana ushindi dhidi ya majeshi katili ya Adolf Hitler.
Awali kazi
ya SAS ilikuwa faragha. Ila mwaka 1980 magaidi walipoteka nyara ubalozi wa Iran
hapa London polisi walishindwa kuwakomboa maofisa na wananchi 26 waliofungiwa pale kwa
siku tano. Serikali ilituma kikosi kidogo cha SAS kilichoingia kimbinu na
kusuluhisha tatizo. Huyu Bear Gryllis alikuwa askari wa SAS hadi alipostaafu
baada ya kuumia kazini.
Ameshaandika vitabu kumi na
tano vinavyozungumzia mbinu za kuishi, mtazamo wa matumaini, kufanya kazi na wenzako
kijumuiya, kujitegemea na kutafuta masuluhisho ya haraka bila kutegemea sana teknolojia au bahati nasibu. Kwangu mimi
mtazamo huu ulikuwa ndani ya maadili ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ya Azimio la Arusha la 1967, Tanzania.
Wazungu wanachukulia suala
hili kwa undani zaidi.
Leo watoto wadogo wanakua
wakiogopa kupambana na mazingira. Watoto wa Kizungu hata watu wazima wanahofia kuchinja mnyama
kusudi wamle. Lakini hapo hapo wako tayari kwenda dukani kununua nyama
iliyoshatengenezwa tayari katika makasha na mifuko ya plastiki.
Bear Gryllis anachosisitiza
ni sisi kukaribia maumbile.
Karibuni alitoa kipindi
(documentary) ambapo wanaume na wanawake walipelekwa visiwa viwili tofauti bahari ya Pacific
wakaachwa pale kwa mwezi mmoja na nusu bila ya vifaa vyovyote vya kisasa mbali
na camera (kurekodi waliyofanya) na vifaa vya huduma ya kwanza. Wananchi hawa wa
kawaida walikuwa mseto wa taaluma mbalimbali tofauti na hawakuwahi kuishi
porini.
Baada ya siku chache wachache walishindwa kutokana na shida kama namna ya kuwasha moto,
maji ya kunywa (yalikuwepo kisiwani, ila ilibidi kujua kuyapata) au nge, nyoka,
nk. Humo humo tulionyeshwa hisia zao mfano wanaume kuzozana na kupigana wenyewe
kwa wenyewe, wanawake kulia ovyo, nk. Waliomudu waliwinda mamba, ngiri, nyoka
na samaki na wakakaa hadi mwisho wa kipindi. Walikiri kujifunza mengi.
Mwisho, jasiri Bear Grylls
aliporudi kuwachukua alitoa fundisho
kuwa leo mwanadamu kasahau kupambana na mazingira.
“Kipindi kinatufundisha
kuishi kijumuiya. Ilibidi wahusika washirikiane, watumie mikono na akili ya
kuzaliwa. Katika shida mtu hujiwa na nguvu mpya...”
Alisisitiza herufi TATU kuu.
Wanadamu hatuwezi kukaa zaidi ya dakika tatu bila kuvuta pumzi, siku tatu bila
kunywa maji na majuma matatu bila kula.
Yote haya yatuelemisha nini?
Sisi Waafrika tungali na
maarifa haya. Bado tunaishi mbugani na mazingira yenye wanyama pori na mimea
asilia. Bado hatuogopi kuchinja mnyama ili kumla kitoweo. Bado tunaishi mazingira
yenye jumuiya inayosalimiana na kujamaamiana.
Waafrika tuko karibu na
maumbile kuliko wenzetu.
Wazungu wameshaanza kupoteza mengi kutokana na
teknolojia na mashine za kisasa. Ingawa kuendelea huku kumerahisisha maisha,
pia kumewapooza kiasi ambacho yabidi Mzungu ajifunze tena mambo mengi ya msingi
ambayo kwetu ni kawaida. Mifano michache ni kama kuwasha moto mbugani na
kutumia kuni. Je kwanini watoto wa shule za Kizungu waoga wa wadudu au moto?
Juma lililopita tulitoa mfano
wa jinsi ambavyo Waafrika tumeacha kula vyakula asilia. Tukichunguza wakati
sisi tunaanza kuparamia maendeleo ya teknolojia wenzetu wameshajua madhara
yake. Tumechangamkia magari, wao wanahusudu kutembea kwa miguu au kupanda
baiskeli. Meya wa London, Bwana Boris Johnson huoneshwa kila mara akienda
kazini kwa baiskeli huku kavaa suti na walinzi. Lengo ni kupunguza unene.
Je, kweli utamwona kiongozi wa Kiafrika
akienda kazini kwa baiskeli na suti? Wakati ambapo sisi tunaanza kuchangamkia
mazoezi ya mashine (Gym) wenzetu wanahusudu zaidi kutembea mbugani, kupanda
milima, kuogelea nk. Hii ni sababu mazoezi ya vyuma yamethibishwa kuhatarisha
mifupa, viungo, magoti na mgongo. Wameshaona madhara. Wakati ambapo sisi tunachangamkia simu za
mkononi na kompyuta, wenzetu wametahadharishwa na hatari za mionzi yake
inayochangia saratani. Muda wa kula, kulala au kupumzika, simu huzimwa kabisa. Sisi tuko
nayo saa 24. Wakati ambapo sisi tunachangamkia
TV kwa kuiwasha saa 24 , Wazungu huwa kimya, kusikiliza redio na kuzima runinga
wakati wa mlo. Teknolojia hutumiwa kwa nyakati muhimu kama kusaka wahalifu na
kulinda nyumba. Maendeleo ya kiteknolojia ni muhimu sana. Ila yahitaji matumizi
ya akili na uangalifu.
-Ilichapwa pia Mwananchi Jumapili, Mei 31, 2015
No comments:
Post a Comment