Tarehe 23 Novemba 1963 wakati namalizia malizia darasa la pili, tuliambiwa tusiende shule. Jana yake, Rais
John F Kennedy wa Marekani alipigwa risasi akiwa ziarani mjini Texas. Nakumbuka
Watanganyika (tulivyoitwa miaka hiyo ) tulivyosikitika. Rais Kennedy alipendwa
sana. Marekani iliisaidia Tanganyika kwa misaada na wataalamu wa kujitolea – walioitwa “Peace
Corps.” Urafiki huu ulidhihirishwa na mifuko ya sembe na vyakula yenye picha ya
mkono wa Mzungu na Mwafrika vimeshikana kirafiki.
Mwalimu Nyerere alipokaribishwa na Rais John Kennedy na kuhutubia Ikulu ya Marekani- mwaka 1963. Walikuwa marafiki wakubwa. Miezi michache baadaye Rais Kennedy aliuawa.
Baada ya miaka mitano mdogo wake marehem, Robert F Kennedy naye aliuliwa
kwa risasi wakati akifanya kampeni za Urais. Wengi walitazamia angekuwa
kiongozi bora kama kaka mtu.
Toka walipouawa ndugu hawa, sinema mbalimbali na mandishi yametolewa kuhusu
kisa na sababu. Aliyezungumziwa na anayeendelea kuongelewa ni marehem John Kennedy-
rais aliyependwa kuzidi wote katika historia ya Marekani.
Mauaji ya Rais Kennedy yamechambuliwa sana. Habari zilizofahamika ni kuwa
alipigwa risasi na Lee Harvey Oswald – kijana rafiki wa Warusi kutokana na
msimamo wake wa siasa za mkono wa kushoto (ukomunisti). Oswald hata hivyo
aliuawa siku mbili baada ya kutiwa hatiani. Aliyemtungua (Jack Ruby), naye alifariki
jela – kabla ya kueleza sababu hasa za kitendo hicho. Sinema iliyotolewa na
Oliver Stone, mtengezaji maarufu wa mchezo wa “Platoon” (1986) mwaka 1991
ilijaribu kuonyesha kuwa mauaji ya Rais Kennedy yalipangwa na serikali. Sinema inaitwa
JFK.
Tathmini hii ingali ikiendelea. Kwa majuma mawili sasa runinga huku Majuu
zimeonyesha vipindi vingi vinavyodai kwamba serikali ya Marekani ilihusika na
kifo cha Rais Kennedy. Kwamba wanausalama walificha ukweli (“cover- up”) kwa kumsingizia
Bwana Lee Harvey Oswald.
Sinema ya mwisho niliyoitazama wiki hii inaangalia risasi tatu zilizopigwa
mchana ule wa Novemba 22. Ya kwanza iligonga taa ya barabara , ya pili ikamdunga
Rais Kennedy shingoni na kutokezea alikokaa Gavana wa Jimbo la Texas (John Connally)
–lakini hakufariki. Ya tatu ilimpiga tena Rais kichwani na kubomoa ubongo wote.
Dai linaendelea kueleza kuwa risasi ya tatu haikurushwa na Bw Oswald
aliyekuwa ghorofani- ilifyatuliwa na mmoja wa wana usalama nyuma ya gari la
Rais- ndani ya msafara. Dai na ushahidi vinasema baada ya Rais Kennedy kuingiwa
na risasi shingoni – mwanausalama George Hickey- alichomoa bunduki akijitayarisha
kujibu mapigo juu ghorofani (alipokuwa Oswald) sasa kwa vile msafara ulibidi kukitoa mbio- katika
mtafaruku na fadhaa mwana usalama Hickey akafyatua bunduki kwa bahati mbaya.
Tunaambiwa wakati maiti ikifanyiwa ukaguzi wa mwisho (“autopsy”),
wanausalama hawakutaka habari zifahamike. Walificha picha za mganga za kichwa
cha marehemu Rais. Kawaida mtu akipigwa risasi jeraha huonyesha ni risasi au
bunduki gani. Wajihi wa hayati Kennedy ulithibitisha jeraha la kichwa na shingo
vilipigwa na bunduki tofauti.
Sasa kuna hayo.
La pili ni ushujaa wake Rais John Kennedy. Alizaliwa mwaka 1917 katika familia
ya watoto tisa na baba, Joseph Kennedy, alipenda siasa na utawala. Toka akiwa
mdogo John aliugua ovyo- ila alikua shupavu, kitabia. Aliingia jeshi la majini
la Marekani, akiwa kiongozi wa boti za kivita mwaka 1943 hadi 1945. Boti lao
liliposhambuliwa vikali na Wajapani, Kennedy - aliyekuwa na cheo cha Luteni-
alijitahidi kuwaokoa waliokuwa chini yake kwa muda mrefu jambo lililomfanya
abugie maji chumvi na mafuta ya petroli ya meli hiyo ndogo. Kutokana na hali
hii alisumbuliwa na matatizo ya tumbo- maisha yake yote. Mwaka 1943 alipewa nishani mbili za kishujaa. Kuanzia 1946 aliwakilisha jimbo lake la Massachusetts,
bungeni. Mwaka 1955 alipewa tuzo mashuhuri ya Pullitzer (inayotolewa kwa wapiga
picha, waandishi na wanahabari) alipochapisha kitabu cha maisha ya Wabunge wanane wa Kimarekani waliopigania
fikra zao bila kutetereka.
Baadaye 1961 alishinda uchaguzi wa
Rais kwa kura zaidi ya mpinzani wa chama cha Republican Bw. Richard Nixon. Rais
Kennedy amejulikana zaidi kwa mauaji yale ya Novemba 22 na mahusiano yake na
akina mama – alikuwa mwingi wa wanawake. Kinachosahaulika ni ushujaa wake
vitani, namna alivyozuia vita vya dunia mwaka 1962 na kuidhinisha muswaada wa
kuwapa haki watu weusi wa Marekani, kipindi kifupi kabla ya kuuawa.
Moja ya sifa kuu ya kisiasa anayokumbukwa ni uzalendo na ukweli. Kinyume na
wanasiasa wengi (duniani) hakutoa ahadi nyingi
kwa wananchi kabla na baada ya kuteuliwa kiongozi. Kennedy : “Usiulize
nchi yako itakusaidiaje. Uliza nini unaweza kuchangia kwa nchi yako.”
Mwingine wa kukumbukwa aliyefariki mjini London, Jumapili iliyopita- ni
mwandishi wa Kiingereza Doris Lessing. Bi Lessing aliyezaliwa mwaka 1919,
alichapisha vitabu zaidi ya hamsini vya riwaya, michezo ya kuigiza, hadithi
fupi na makala . Mada zake kuu zilitetea haki za binadamu, udhalimu na ubaguzi wa
Waafrika – (aliwahi kuishi Zimbabwe) na haki za wanawake.
Kwanini safu inamzungumzia Doris Lessing?
Doris Lessing - akionyesha tuzo aliyopewa mwaka 2011.
Picha ya gazeti la Guardian - Uingereza
Ujuzi wa lugha Tanzania wazidi kudidimia. Leo vijana wengi – hata walio
masomo ya juu chuo kikuu hawawezi kuandika au kusema Kiingereza fasaha. Wapo
wanaojifaragua kwa kuchanganya hiki “Ki-Swanglishi” lakini wanajidanganya tu.
Usipopika chakula kikaiva ya nini kukiwekea eti binzari, pilipili na iliki
kiliike?
Moja ya njia kuu za kuboresha lugha ni kusoma. Tukiwa sekondari zamani tulishindana
kusoma riwaya (mathalan James Hadley Chase na Faraji Katalambula) Kiingereza na
Kiswahili. Je, vijana wangapi wanatembea na riwaya mifukoni leo? Maandishi ya
Doris Lessing yameandikwa kwa usafaha sana. Hadithi alizotungia Afrika- mathalan “Grass is
Singing”, “A Man and Two Women”, “A
Proper Marriage” na “African Stories”- zina maelezo murua ya mazingira, ushairi
na mandhari ya bara hili. Ingawa ni Mzungu tungo zake zina mapenzi kwa
anachokielezea. Alikua mpinzani mkubwa wa ubaguzi wa rangi Zimbabwe na Afrika
Kusini. Fasihi yake pia inawatetea wanawake na wanaume wanaoteseka katika
mahusiano ya ndoa, mapenzi au kazi. Si ajabu alishinda tuzo mbalimbali ikiwemo
–Nobel Prize- ya 2007.
Ukimsoma utaitajirisha lugha yako.
Sababu nyingine ya kuelezea habari zake ni kukukutaka msomaji uwajue
waandishi wazuri, duniani. Doris Lessing alikula chumvi nyingi. Alifariki akiwa
na miaka 94. Alizaliwa Uajemi (Iran) akaishi Zimbabwe na Uingereza. Ni
mwandishi muhimu sana kumjua na kumsoma; sidhani atakosekana maktaba za Kiingereza,
Afrika Mashariki.
Ilitoka pia -Mwananchi - KALAMU TOKA LONDON
No comments:
Post a Comment