Watu wa kabila la Chwi kule Ghana
wanaozungumza lugha iitwayo Tshi wana methali kuhusu umuhimu wa kupendeza.
Inashauri: “Ikiwa mwenda wazimu ataiba nguo zako na kukimbia nazo wakati wewe
uko majini unaoga, itakuwa vyema utafute angalau kipande cha kitambaa ujifunge wakati unamkimbiza maana usipofanya vile
watazamaji watadhani na wewe umeheuka.”
Hakuna mwanaume ambaye hajawahi kupayukiwa
kuwa asuburi wakati ndugu yake wa kike anajipodoa akijiremba. Na kati ya
mapambo yote nywele zinaongoza foleni. Mwanaume waweza kutoka bila kuchana
nywele, unaweza ukawa nusu kipara (kama mimi mwandishi) lakini hujali mradi u
msafi utatoka zako mitaani. Kwa mwanamke kujisanifu nywele ni tendo muhimu
sana. Ndiyo maana waandishi mbalimbali wa hadithi hawakosi maelezo ya ususi
ndani ya riwaya zao.
Elvis Musiba aliyefariki miezi mitatu
iliyopita kaiweka taswira ya mwanamke aliyeshikilia panga na rungu juu ya
jalada la “Uchu” iliyochapwa 2000. Ingawa kisa cha “Uchu” kinahusu mauaji
yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 bibiye jaladani kasuka mabutu; hakuna damu wala machozi usoni mwake. Pamoja
na maudhui ya kuua kitabuni, msuko umempendeza.
Said Mohammed naye kawapamba wanawake vyema
katika riwaya ya “Utengano” iliyosukwa mwaka 1980. Maimuna mtoto wa mwanasiasa
fisadi anaamua kuyakimbia maisha magumu ya wazee wake na kufanya ukahaba.
Ingawa anaishi vichochoroni kwenye hali ya uchafu na mavi bado chumba chake
kimesanifiwa kwa picha maridadi, meza zilizosheheni vyupa vya mafuta na manukato.
Kifupi ingawa anasota, mandhari ya chumba “ni powa.” Kuna wakati Maimuna kakaa
akitafakari sura yake.
Mwandishi anatueleza ukurasa wa 114.
“ Akajitazama kiooni. Ama kweli urembo wa
kimwetu umekamilia. Hajui kwanini
wanawake wengine hupiga mbio kujibabua na kujifanya mashkuli.”
Na hii ndiyo
mada yetu leo. Mamilioni ya wanawake
wetu weusi duniani “wanajifanya mashkuli” wakikereketwa na uzuri wa bandia
kupitia tatizo la nywele. Desturi iliyoenea
ni ile ya kuchoma nywele (relaxing) iliyopenyeza Bongo miaka kama hamsini
iliyopita kutokea Marekani.
Z. Burhani mtunzi wa “ Mwisho wa Kosa” (1987)
anasisitiza ugeni huu unavyoathiri wananchi kupitia Monika, binti aliyesoma
Majuu.
“ Vijana wadogo pale mtaani nao
walifurahishwa na mazungumzo na mitindo ya Monika, hata siku zote
walijaribu kwenda kuzungumza na kusikiliza hadithi zake juu ya maisha ya huko
Ulaya na kujaribu kuiga mitindo yake ya nguo na ya nywele.” (Ukurasa 5)
Nywele msomaji!
Nywele
na mwanamke ni sawa na kucha na kidole; mti na tawi, gari na gurudumu; mchana
na jua; chai na kikombe...
Kiasilia wanawake wa Kiafrika hawakuwa na
tabia ya nywele bandia ndefu na laini za maiti wa India na China. Ubaya
ulianzia biashara ya utumwa karne ya kumi
na tano. Wanahistoria weusi wa Kimarekani wanasema Waafrika waliochukuliwa
walibakia na mitindo yao ya ususi na nywele hizi zetu ngumu hadi utumwa
ulipofutwa kisheria katikati ya karne ya 19. Baada ya kupewa uhuru sasa watumwa
walikuwa raia wa Marekani. Tatizo likaanzaje?
Wamarekani weusi ni asilia mia 13 tu ya jamii
ya nchi hiyo. Wengi jamii hiyo ni Wazungu wenye nywele ndefu laini. Sasa
wanawake weusi walioshalazimika kuwa sehemu mahsusi ya raia wa taifa jipya la
Marekani (lililojikomboa toka kwa Waingereza mwaka 1776) walijiona wana sura
mbaya wakijilinganisha na Wazungu. Licha ya kutaka kuwa weupe, walilainisha
nywele zao kutumia magadi na viazi jambo lililoleta michibuko na madhara mengi.
Moja ya kanuni za wanaonyanyaswa ni kujaribu kuiga tabia za wanaowanyanyasa
kusudi wasionekane kinyume cha mambo. Leo
desturi hiyo ya kulainisha nywele kama za Wazungu imeenea ulimwenguni hata
Tanzania.
Mwanariwaya maarufu Shafi Adam Shafi anaonyesha
jamii ya Kizanzibari miaka hamsini iliyopita. Wanawake bado walithamini ususi
na uzuri asilia.
Mfano mzuri ni mashoga wawili Mswahili, Mwajuma
na Mhindi, Yasmin katika “Vuta Nikuvute” kitabu kilichoshinda tuzo la uandishi bora wa
Kiswahili mwaka 1998:
“Yasmin alichana nywele zake vizuri
akazizongazonga na kuzifungua juu zikawa kama sega la nyuki. Na Mwajuma naye
alizipasua zake njia ya kati, akazifunga kwa pini huku na huku na kila mmoja
kati yao alipachika kishada cha asumini kichwani.”
Tabia iliyoenea ulimwenguni leo ya wanawake
weusi kulainisha nywele kutumia dawa mbalimbali
zinazozilainisha, nywele bandia za maiti, kuzichoma kusudi ziangukie
mabegani kama za Wazungu na Wahindi imeenezwa na wanawake weusi maarufu.
Mwaka juzi mchekeshaji wa Kimarekani, Chris Rock alitengeneza sinema maalum (“Good Hair”) kukejeli namna wanawake mashuhuri
na wasanii wanavyoeneza kasumba hii kwa wanawake duniani. Chris Rock aliamua
kutoa sinema baada ya binti yake wa miaka mitano kumuuliza kwanini hana nywele nzuri kama za Kizungu? Sinema hii pia inaonyeshwa kifupi katika mtandao wa You Tube, kwa watakaoweza kutazama.
Chris Rock anawahoji wanawake maarufu
mathalan Oprah Winfrey mwenye nywele hizi vile vile.
Biashara
ya kulainisha nywele inayapatia makampuni ya uzuri duniani fedha nyingi sana. Nchini
Marekani inaingiza dola bilioni tisa kila mwaka. Pamoja na nywele zinazouzwa toka maiti wa
Kihindi na Kichina ni pia matumizi ya dawa
kama “Jehri Curl” zinazosababisha michubuko ya ngozi, fuvu la kichwa na
kunyofoa kabisa nywele. Kati ya magonjwa yanayotokana na usokotaji mbaya wa
nywele ni “Alecopia” unaowaletea
wanawake vipara miaka 35 kuendelea. Zamani wanawake wa Kiafrika walipokuwa
wakisuka nywele ama kuzichana mtindo wa “Afro”
hawakuwa na maradhi haya. Mbali na maradhi
fani hii ni aghali sana. Wanawake wasiojiweza leo Bongo wanalazimika
kuwa na nywele fupi na baadhi kujiona kama wana sura mbaya; kumbe sivyo. Wao
ndiyo wazuri wa kweli!
Wanawake wachache maarufu mfano hayati Miriam Makeba na Angela Davis wameishi hadi uzeeni na nywele zao bila tatizo kwa kuwa
hawakutumia dawa au nywele za maiti. Leo tunao baadhi ya wanawake viongozi kama
kaimu balozi Umoja wa Mataifa, Asha Rose Migiro, ambaye hupigwa picha na nywele
safi asilia. Baadhi ya wanawake maarufu wameanza kampeni kupinga tabia hii
inayoharibu uzuri asilia mathalan Rihanna na Solange Knowels dada yake mwimbaji
Beyonce aliyeamua kukata nywele na
kuanza kusuka mwaka 2009. Ajabu mara
Solange alipokata nywele alipingwa vikali na washabiki walioshalewa kasumba ya
nywele hizi muflis.
-Ilichapwa Mwananchi Jumapili, 31 Januari, 2011
Kaka siku soma hii makala. Nimeipenda sana. I have something to criticize my wife. Asante sana
ReplyDelete