Niko katikati ya kitongoji
cha matajiri, London...
Nimezungukwa na majumba ya ghorofa, vigae, matofali ya kisasa,
vioo vitupu; mseto wa ujenzi. Punde
nimekabiliana na Harrods- duka maarufu
la mamilionea la ghorofa tano. Harrods
imesimama mtaa wa Knightsbridge. Kando yake mna jumba dogo zaidi lenye matofali rangi kikahawia mtindo wa karne ya
kumi na tisa. Mtindo huu unalandana na
mila na desturi za Malkia Victoria aliyetawala karne hiyo (ya juzi) enzi za ukoloni.
Nyanyake malkia Elisabeth.
Jengo lina ofisi nyingi na
mojawapo ndipo ulipo Ubalozi wa Ecuador. Kawaida Ubalozi mdogo wa Ecuador
usingekuwa na haja ya kuandikwa katika safu kama hii. Ila katika kipindi cha
miezi miwili – umetajwa tajwa na kufahamika sana.
Hapa niliposimama nje
nawaangalia askari zaidi ya kumi wa Kiingereza waliojipanga nje,wakiulinda
ubalozi. Upande mwingine wamebana, paparazi na wanahabari na kamera zao;
watalii wanapita pita nao wakipiga picha na mkabala wa Ubalozi limejikita kundi
la watu, wakipiga kelele, wakiwasuta wale ma-askari. Mmoja wao kashika kipaaza sauti:
“Hakuna mtu aliyepiga simu namba 999 kuulizia msaada
wenu, wajinga nyinyi!”
Askari hawasemi kitu. Watasema
nini? Nchi hii ina Uhuru wa kusema na kujieleza. Ukiyatazama mabango waliyobeba waandamaji na mengine waliyoyabandika kando ya barabara
pia mkabala na Ubalozi wa Ecuador, yatakufahamisha nini kinatokea.
Mathalan:
“Kwanini askari wa Uingereza
wanashirikiana na Marekani?”
“Ujasiri Unaambukiza!”
"Chapisheni Ukweli!"
“Uhuru.”
“Ondoeni mikono yenu toka
Ecuador!”
“Serikali ya Uingereza ya
Aibu lakini si wananchi wake!”
Na mabango kadhaa yana picha
za mhusika.
“Mwacheni huru Assange! Msimpige
Mjumbe risasi!”
Yote, yumkini, yanamhusu mwanahabari Julian
Assange ambaye toka Juni 19 aliomba ukimbizi ubalozi wa Ecuador.