Thursday, 20 September 2012

OLIMPIKI YA VILEMA IMEMALIZIKA -TUJITAYARISHE KWA MICHEZO YA MADOLA GLASGOW 2014


Awamu ya pili ya michezo ya Olimpiki ilishamalizika  London. Tokea 1988, mashindano haya ya vilema yalifanywa sehemu mahsusi  ya Olimpiki kule Korea Kusini, ingawa tukio lilikubalika rasmi  Olimpiki, Roma, Italia, 1960 .
Zaharani Mwenemti akiwa na wahudumu waliojitolea Olimpiki...picha na F Macha

 Mwaka huu Tanzania iliwakalishwa na Zaharani  Mwenemti aliyeshiriki utupaji tufe (“shotput”) na kisahani (“discus”). Mwenemti aliongozana na kocha, John Ndumbaro(mwenye ulemavu wa mguu mmoja) maofisa wawili – mkuu wa msafara, Johnsoon Meela na afisa utawala, Iddi Kibwana- (pichani chini) wote pia walemavu wanaotumia viti vya magudurumu au fimbo kutembelea.

Nilipohudhuria mashindano haya katikati ya juma nilishangazwa na kiasi kikubwa cha watazamaji. Bidii na juhudi za wanamichezo walemavu inasisimua na ni somo kwetu wote.
Suala la michezo ya vilema duniani lilianzishwa na mganga wa upasuaji na mishipa ya fahamu, Profesa Ludwig Guttman mwaka 1948.

Profesa Guttman....aliyeanzisha na kupigania uwezo na maendeleo ya walemavu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia...
<--more--!>


Profesa Guttman alikuwa Myahudi aliyetoroka unyanyasaji uliofanywa na Nduli Adolf Hitler, akahamia Uingereza 1939. Kutokana na heshima aliyoshaijenga baada ya kazi ya miaka mingi kuendeleza maslahi ya wagonjwa na walemavu Profesa Guttman alipewa paundi 250 (leo kama £10,000 ambazo ni takribani shilingi 25 milioni). Pesa hizo zilimsaidia kuanzia maisha na kuendeleza utafiti Idara ya Majeruhi ya uti wa mgongo, hospitali ya Radcliffe, Oxford, mji wenye chuo maarufu cha kimataifa.
Mganga huyu wa Kijerumani aliona haja ya kuwasaidia wagonjwa na majeruhi wa kivita kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwepo michezo. Awali askari majeruhi walijiona hawana bao katika maisha na asilimia 80 walifariki miezi mitatu tu baada ya kurudi nyumbani. Profesa Guttman alitumia michezo na shughuli mbalimbali kuusaidia mwili na akili kukarabati viungo na maisha yao. Mwanzoni alipambana na mtazamo finyu ulioenea kuwa ulemavu ni nusu-kifo na jambo lisilokarabatika. Alifanya majaribio ya kwanza uwanja wa Mandeville ambapo walemavu walishindana mwaka 1948. Michezo hii ilifanywa kila baada ya miezi 12 hasa na askari. Chama cha kimataifa cha wanamichezo walemavu kiliundwa Uholanzi mwaka 1952 na  michuano ilipoanza ilihusisha zaidi washindani waliotumia viti vya magurudumu.
 Baadaye mwaka 1960 michezo ya ulemavu katika Olimpiki iliwekwa rasmi ikifuata baadhi ya nguzo zilizowekwa na Profesa Guttman.
Halaiki ya maelfu ya watazamaji toka kila pembe ya dunia waliohudhuria mashindano ya walemavu kwa moyo, uchu na hamasa...Picha na F Macha.

Toka 1960 hadi sasa michezo ya ulemavu imeenda sambamba na Olimpiki na ilianza kuitwa “Paralympic” (Olimpiki ya Los Angeles, Marekani, 1984) ikatambuliwa rasmi na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC). Neno “paralympic” ni muungano wa  “paralyse” (kupooza viungo au mwili) na “olympic”...Uuandaji  huu wa maneno huitwa kwa kimombo “portmanteau” na hutumiwa na lugha mbalimbali ulimwenguni. Tunayo arusi hii pia katika Kiswahili-mfano: “runinga” (televisheni) linalotokana na “rununu” (sauti kutoka mbali)  na “maninga” (macho yaonayo mbali) au “Tanzania” (Tanganyika na Zanzibar).
Idadi ya washindani imeongezeka sana. Paralympiki ya Rome, ilikuwa na wanariadha 400 toka nchi 23, ambapo Atlanta (1996) wanariadha vilema walikuwa 3,500 (mataifa 104) na mwaka huu idadi imeshagonga 4,233 (nchi 204). Hili ni ongezeko la mataifa 100 katika kipindi cha miaka 16.
Nembo ya tovuti ya Wanamichezo walemavu Tanzania...

Lengo aliloweka Profesa Guttman lilikuwa kusaidia kurejesha hali ya walemavu hasa waliopooza uti wa mgongo, ila kadri miaka ilivyokwenda shabaha hiyo imepanuka zaidi.  Wahusika wa michezo walitangaza mwaka 1996 kwamba nia ya “paralympic” ni kujenga mwamko kuhusu vilema, usawa na uwezo wa walemavu.
“Ushindani wa michezo unafuta makovu kuhusu ulemavu na kuonyesha uwezekano wa hali ya juu,”  walisema.
 Je kwetu Afrika, seuze Tanzania tunawaonaje walemavu na vipi tumewakilishwa na mlemavu mmoja tu?
Kabla ya kujibu swali hebu tuangalie historia yetu ndani ya michezo.
Wabongo tulianza kushiriki Olimpiki ya Barcelona (1992)  tulipokuwa na mchezaji wa tennis, Noorel Shariff. Hatukuonekana tena hadi 2004 tulipowakilishwa na mwanamme na mwanamke, Wilbert Constatino (mbio mita 100 na 200) na Mwanaidi Ngitu (mita 800). Mwaka 2008, mjini Beijing tulimpeleka Ernest Nyabalale, pia mkimbiaji. Habari za hawa watu hazipatikani kirahisi ndani ya mitandao , jambo linalodhihirisha sisi kutotangaza, kujali, kujua au kufahamu sana habari hizi za walemavu.
Kitaaluma michuano hugawanywa kati aina ya mchezo na ulemavu. Kimichezo huangaliwa ipi inayotumia viti vya magurudumu (k.m. mpira wa kikapu) au kukaa chini sakafuni ( mpira wa nyavu). Misingi  ya michuano ya ulemavu huangalia aina kadhaa mfano upofu wa macho. Ndani ya utaratibu huu mna migawanyiko ya kiufundi zaidi. Mathalan katika riadha mna migawanyo zaidi ya ishirini inayoangalia ulemavu wa akili, kupooza miguu au viungo vingine. Ndiyo maana utawaona wanariadha wengine wanakimbia kwa miguu ya chuma (kama M-Afrika Kusini Oscar Pistorius mkimbiaji maarufu anayetumia miguu  iliyobatizwa jina la “duma”) kwa kuwa walikatwa miguu chini ya magoti.
Kifupi masharti ni mengi. Je, kwetu mambo yakoje?
Meela akiwa na mshabiki toka Marekani...picha na F Macha

Nilipoongea na mkuu wa msafara, Johnson Meela alinipasha ingawa tumewakilisha mtu mmoja tu bado yapo mengi sana ya kujifunza. Kwa kukutana na wanamichezo wengine, kuhudhuria mikutano ya kimataifa na mashirika mbalimbali ya michezo ili kupanua hadhi na maingiliano yetu Watanzania.
Lakini si rahisi. Suala kuu anadokeza Meela ni uchumi.
“Mafanikio ya michezo hutegemea uchumi na nini kinapewa kipaumbele. Serikali, mathalan inajiuliza itoe kiti cha magudurumu kwa mgonjwa wa hospitali – kinachogharimu shilingi milioni 6-au kwa mwanamichezo?Tunaweza kulaumu lakini je, kiuchumi tunaweza?”
Ndiyo maana, anasema Meena, utawakuta Waafrika wanaoongoza katika michezo ya walemavu (na hata ya kawaida) ni wale wanaojiweza kiuchumi- Afrika Kusini, Uarabuni na Kenya.  Katika nchi nyingine sekta ya binafsi ndiyo mfadhili mkuu wa michezo hii. Je, kwetu sekta hii ikoje?
Je walemavu wakikidhiwa  haja zaidi itamfaidia nani?
Je kwanini Nigeria ambayo haikupata hata medali moja katika michezo ya awamu ya kwanza lakini walemavu wamepata nyingi tu? Je, nini faida ya taifa kujivunia ushindi wa medali? Kwanini wanamichezo wa Kenya wanapopita popote duniani leo wanaheshimika na kuwapa fahari wananchi wao? Vipi Tanzania haifahamiki wala kuheshimika kihivyo? Mbona wakati wanamichezo wetu walipokuwa wakipita katika gwaride la ufunguzi wiki jana, runinga husika hapa Uingereza ilipitisha tangazo la biashara na kuwaziba lakini haikufanya hivyo kwa Wakenya? 
Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili...






No comments:

Post a Comment