Niko katikati ya kitongoji
cha matajiri, London...
Nimezungukwa na majumba ya ghorofa, vigae, matofali ya kisasa,
vioo vitupu; mseto wa ujenzi. Punde
nimekabiliana na Harrods- duka maarufu
la mamilionea la ghorofa tano. Harrods
imesimama mtaa wa Knightsbridge. Kando yake mna jumba dogo zaidi lenye matofali rangi kikahawia mtindo wa karne ya
kumi na tisa. Mtindo huu unalandana na
mila na desturi za Malkia Victoria aliyetawala karne hiyo (ya juzi) enzi za ukoloni.
Nyanyake malkia Elisabeth.
Jengo lina ofisi nyingi na
mojawapo ndipo ulipo Ubalozi wa Ecuador. Kawaida Ubalozi mdogo wa Ecuador
usingekuwa na haja ya kuandikwa katika safu kama hii. Ila katika kipindi cha
miezi miwili – umetajwa tajwa na kufahamika sana.
Hapa niliposimama nje
nawaangalia askari zaidi ya kumi wa Kiingereza waliojipanga nje,wakiulinda
ubalozi. Upande mwingine wamebana, paparazi na wanahabari na kamera zao;
watalii wanapita pita nao wakipiga picha na mkabala wa Ubalozi limejikita kundi
la watu, wakipiga kelele, wakiwasuta wale ma-askari. Mmoja wao kashika kipaaza sauti:
“Hakuna mtu aliyepiga simu namba 999 kuulizia msaada
wenu, wajinga nyinyi!”
Askari hawasemi kitu. Watasema
nini? Nchi hii ina Uhuru wa kusema na kujieleza. Ukiyatazama mabango waliyobeba waandamaji na mengine waliyoyabandika kando ya barabara
pia mkabala na Ubalozi wa Ecuador, yatakufahamisha nini kinatokea.
Mathalan:
“Kwanini askari wa Uingereza
wanashirikiana na Marekani?”
“Ujasiri Unaambukiza!”
"Chapisheni Ukweli!"
“Uhuru.”
“Ondoeni mikono yenu toka
Ecuador!”
“Serikali ya Uingereza ya
Aibu lakini si wananchi wake!”
Na mabango kadhaa yana picha
za mhusika.
“Mwacheni huru Assange! Msimpige
Mjumbe risasi!”
Yote, yumkini, yanamhusu mwanahabari Julian
Assange ambaye toka Juni 19 aliomba ukimbizi ubalozi wa Ecuador.
Kisheria, mtu yeyote
akiomba hifadhi katika ubalozi wowote na ubalozi ukimkubali, serikali mwenyeji
hairuhusiwi kuingilia. Kuingia ndani ya ubalozi ni kukiuka sheria ya kimataifa
ya itifaki. Alhamisi 16, Agosti, Ecuador ilimpa Assange hifadhi rasmi. Serikali
ya Uingereza ilikataa ikasema itamtia nguvuni. Anashtakiwa kwa kuwanajisi
wanawake wawili Sweden na pia Marekani inamtaka asafirishwe kujibu shtaka la
hujuma. Akishindwa kesi anaweza kuhukumiwa kifo.
Ndiyo maana Ubalozi huu wa
Ecuador unalindwa na askari wa Kiingereza. Polisi mjini hapa wamesema wazi, mara Julian Assange atakapotoka tu nje atafungwa
pingu. Wiki iliyopita mwanahabari huyu alijokeza nje ya ghorofa ya kwanza
akatoa tamko lililopigiwa makofi. Alikanusha madai ya mashtaka ya Waingereza,
Waswidi na Wamarekani.
Waliompigia makofi walikuwa
marafiki, watu wanaomuunga mkono na baadhi ya wanahabari na mabloga kibao
duniani.
Julian Assange ni nani?
Alizaliwa Julai 1971,
Australia. Akiwa na umri wa miaka sita wazazi wake walitengana akawa anatanga
tanga na mamake. Hadi akiwa na miaka 16 waliishi miji 50 na kuhudhuria shule
37. Haya si maisha ya kawaida. Mwaka 1987 akiwa na miaka 16 alianza kujihusisha na shughuli ya kuharibu
mitandao- inayoitwa kwa kimombo “hacking”. Alitiwa nguvuni na wenzake mwaka
1991- na kesi iligharimu dola laki moja. Hakimu alisema angehukumiwa jela miaka
10 kama asingekuwa na maisha ya kuhamahama na ghasia utotoni.
Mmoja wa watetezi wake Julian Assange alimlinganisha na mpigania haki na ukweli, Carl von Ossietzky aliyetunukiwa Zawadi ya Amani ya Nobel (1935) lakini akauawa wakati wa Vita Vikuu vya Pili...
Mmoja wa watetezi wake Julian Assange alimlinganisha na mpigania haki na ukweli, Carl von Ossietzky aliyetunukiwa Zawadi ya Amani ya Nobel (1935) lakini akauawa wakati wa Vita Vikuu vya Pili...
Kati ya 1993 hadi 1999,
Julian Assange alihusika na kazi, shughuli mbalimbali za kompyuta na uchunguzi
wa siri za mitandao. Mwaka 1997 alichangia uchapishaji wa kitabu kuhusu
uharibifu huu(“hacking”) kama mtafiti.
Kati ya 2002 hadi 2005 Assange(tamka “Asanji”)alijiunga na vyuo vikuu
vya Melbourne na Canberra kusomea hesabu, fizikia, falsafa na sayansi.Alikatisha
masomo yake alipoona wanafunzi wenzake “wakiisaidia serikali ya Marekani
kufanya utafiti wa kijasusi.”
Ndipo alipoanzisha tovuti
maarufu ya WikiLeaks, mwaka 2006.
Akiwa mhariri wa tovuti hii
anasema lengo la WikiLeaks ni kubadili mifumo ya serikali:
“ Lazima tufikirie zaidi ya
wale walioshatupita- ili kugundua njia za kubadili teknolojia.” Akaendelea
kublogi: “Kawaida mifumo isiyo ya haki huzua wapinzani kufichua madhila yake
kusaidia kuwadhoofisha- ili kujenga
mifumo bora zaidi ya uongozi.”
Kuanzia hapo WikiLeaks
iliweka wazi madhila ya serikali na makampuni mbalimbali duniani.
Kati ya mambo tovuti hii
iliyofichua ni mauaji ya Wakenya wanaopigania haki za binadamu na mawakili,
Oscar Kingara na John Paul Oulo. Wengine
wanne waliojaribu kuchunguza mauaji haya nao waliuliwa. Baada ya WikiLeaks
kutangaza habari hizi- Julian Assange alizawadiwa Amnesty International Media
2009 Award- ambayo ni tuzo la wanahabari wanaofukua udhalimu wa kijamii.
Baada ya kufichua ufisadi na
wizi wa serikali ya Zine Al Abidine Ben Ali wa Tunisia WikiLeaks ilichangia
mapinduzi na kuanguka kwake mwaka jana.
WikiLeaks imefichua habari za
Bongo pia. Mosi kuhusu mauzo ya shirika la ndege la Tanzania (ATCL) miaka minne
iliyopita na namna shirika hili liliponunua ndege mpya kwa njia za upendeleo.
Pili, kuhusu mauzo ya rada za Uingereza (BAE) na namna mkuu wa kikosi cha
kuzuia rushwa, Edward Hosea alivyolalamika kuogofya atauawa. Malalamiko mengine
yalihusu Dk Hosea akisononeka kuwa baadhi ya viongozi Tanzania hawaguswi na
mkono wa sheria.
WikiLeaks imefichua sumu na
takataka za kimazingira zilizotupwa Ivory Coast, matatizo ya wafungwa wa
Kiislamu walioko jela la Guantanamo, Cuba na mengine mengi.
WikiLeaks ilianza kustua
zaidi ilipotoa habari kuhusu Marekani na vita. Kwanza ni hati 250,000 za siri
za Marekani, kufichua majeshi ya Marekani yalivyoua wananchi Iraq (Wairaki 11 waliuawa na ndege za Kimarekani,
Julai 2007) na Afghanistan(wanawake na watoto 145 waliouliwa na jeshi la
Marekani). Habari hizi zilitolewa na askari wa Kimarekani, Bradley Manning,
ambaye yuko jela.
Haya na mambo kibao
yanayoweza kusomwa zaidi katika tovuti ya WikiLeaks na yameiudhi sana serikali ya Marekani. Ongezea
habari za siri za mabenki makubwa makubwa ya Ulaya na habari nyeti za
wanadiplomasia mbalimbali duniani.
Yote hayawezi kuenea
kuandikwa hapa. Yamemfanya Julian Assange awe mmoja wa wanahabari hatari sana
duniani. Si ajabu keshapata tuzo kibao ikiwemo Martha Gellhorn Prize 2010 kwa uchunguzi jasiri wa habari, na hadhi
ya mtu muhimu wa dunia iliyoandikwa na jarida marufu la Kimarekani “Time” mwaka
juzi. Si ajabu sasa hivi kajificha ubalozi huu wa Ecuador akitafutwa na nyoka
na mafahali wa dunia.
Tazama video tuliyotengeneza kuhusiana na suala hapa
No comments:
Post a Comment