Monday, 7 February 2011

HAJA NDOGO NJE KWA WANAWAKE SI JAMBO RAHISI...

Tupo sebuleni kwa jirani yangu mmoja mwanamke. Katualika majirani kusherehekea siku ya kuzaliwa miaka themanini. Themanini nakwambia! Wanawe wawili wamewasili na wajukuu na vitukuu toka Australia na Afrika Kusini kushangilia siku hii maalum ya ajuza mcheshi, roho safi; kibibi anayependwa na kila mtu hapa mtaani ninapoishi London. Nyumba imetota baraka. Harufu mbalimbali za makulaji zinazitesa pua. Vyakula vimetandazwa mezani. Viazi Ulaya vya kuchemsha na kuoka vinavyotengeneza msosi maarufu uliovum buliwa na hawa hawa Waingereza unaojulikana kama Chips. Mboga mbichi safi za saladi, nyanya, matango, vitunguu, jibini (chizi), mikate ya kila sampuli, samaki na kuku wa kukaanga. Kawaida karamu za Majuu hutenganisha walaji wa nyama na wasiokula nyama (Vegetarians).

Meza vile vile ina maziwa mtindi, chai, kahawa na juisi za matunda kwa wasioafiki pombe. Kwetu walevi haukosekani mvinyo, wiski na bia. Kifupi ni sherehe muhimu ingawa siku hizi kutimiza miaka themanini (hasa kwa wanawake) nchi zilizoendelea si maastajabu. Wastani wa maisha ya mtu wa kawaida Majuu ni miaka 75 hadi 80. Karibuni serikali ya hapa ilitoa takwimu kusisitiza kwamba idadi ya wazee inazidi kuwa kubwa kuliko ya vijana. Linganisha na kwetu Afrika ambapo wastani wa maisha ni miaka 40 hadi 55.
Iko haja ya kujiuliza kwanini.
Mwaka 2003, mtalaamu wa elimu jamii chuo kikuu cha Dar es Salaam, marehemu Profesa Chachage S. Chachage aliandika katika insha kuhusu muziki wa Bongo Fleva kwamba idadi ya Watanzania waliozaliwa mwaka 1978 kuendelea ni kubwa kuliko ya waliokuja wakati wa Uhuru, 1961. Katika miaka hamsini iliyopita idadi ya wazee inazidi kufifia. Zamani jamii zetu Afrika zilithamini sana busara ya ajuza shauri ya maarifa, busara na hekima zao. Tujiulize je ikiwa idadi ya vijana inazidi kuwa kubwa kuliko ya wazee tutaishia wapi nchi zetu?
Je, nini kiini cha maisha yetu kuzidi kuwa mafupi na magumu? Je, adui wa maendeleo yetu ni mwananchi mwenyewe au nani?
Ah, wahenga, mtusamehe.
Nipo bado katika pati la Mama Jones. Hataki kuitwa mzee au Mummy Jones. Husisitiza nimwite Marianne, jina lake la kuzaliwa. Wazungu hawana shikamoo; wala hawawaiti wazee kwa majina ya wanao, kama sisi. Jones ambaye ni rika langu keshalewa. Anajaribu kuimba na wanawe vijana. Wimbo maarufu sasa hivi Ulaya, “Dynamite” (baruti) wa mwanamuziki,Taio Cruz:
“You wanna put your hands in the air sometime!
Gotta let go!”
(Nyoosha mikono angani uimbe!
Jiachie!)
Wageni washalainika, pombe imewaingia, Mama Jones yule kule anajimwaga na wajukuu na vitukuu. Kawaida Majuu wanawake ndiyo wacheza densi. Wanaume hasa vijana huona kucheza densi jambo la kike; ama la kifirauni.
Hapa nilipokaa naisikiliza soga la mama mmoja mwalimu wa Kijamaika:
“Basi jana Freddy niliona jambo la ajabu mjini London.”
Kwa vipi? Nataka kujua.
“Natoka kituo cha basi kuelekea nyumbani. Nimepinda uchochoroni, kiza kimeshaingia nikamwona mwanamke kakaa chini. Nikadhani kaanguka au anajaribu kurekebisha viatu vyake. Kumbe sio.”
Kakamata glasi ya mvinyo; anaweka fundo moja, anakaza macho tena, anajifuta midomo.
“Alikuwa akikojoa.”
Namuuliza kama huyo mkojoaji, alimwona.
“Aliniona ndiyo, lakini hakujali. Nadhani alikuwa kalewa; aliendelea tu na shughul.”
Si kawaida mji huu wenye zaidi ya wakazi milioni kumi, kusikia mwanamke kajisetiri barabarani. Kwanza kabisa lazima ieleweke kisheria ukishikwa unajisaidia ovyo njiani unatozwa faini na kupewa onyo kali. Ukishikwa tena ni jela.
Niliisikia sheria hii mara ya kwanza nilipotembelea Nairobi, zamani. Miaka hiyo ya Sabini ilikuwa hatia kukojoa nje, Kenya, ilhali kwetu Tanzania hakukuwa na utaratibu aina hiyo, kisheria.
Kisa anachokisema mwalimu huyu wa Kijamaika kinamgutua dada mwingine kando yangu mzawa wa Pakistani. Tumwite Sharmilla. Sharmilla anasisitiza jinsi wanawake walivyo na taabu kujisaidia hadharani.
“Nyinyi wanaume mnaweza tu kujibanza pembe ya ukuta au mti mkajiachia...”
Bwana Jones, anakohoa: “ Mbona miye sijawahi?”
Kila mtu anacheka. Sharmila anachachamaa.
“Ngoja niwapashe. Siku moja nimetoka kazini; mvua bab kubwa inanyesha. Halafu ilikuwa imetokea ajali hivyo foleni za magari haikuwa masihara. Kila nikitaka kutoka dereva wa basi hataki kusimamisha chombo...”
Sharmilla anasisitiza moja ya sheria ambayo haiwaruhusu madereva kusimamisha ovyo mabasi sehemu zisizo vituo. Sheria hii ilipitishwa kutokana na abiria kushtaki makampuni kulipia fidia wakiumia. Kawaida nchi zilizoendelea suala la bima ya maisha ni suala zito sana. Ukiumia kazini, safarini au barabarani, kwa ajali unadai fidia.
Sharmila : “Basi mkojo umenibana. Nangoja weee, nangoja weee... kibofu karibu kinipasuke. Hatimaye basi limesogea kidogo ingawa hatujafika nyumbani, nimeona baa nikashuka upesi upesi. Mi Mwislamu, sinywi pombe lakini ikanibidi niingie kwenye ile baa; nikataka nielekee moja kwa moja msalani. Pale nimesimamishwa na mmoja wa wahudumizi. Kasema vyoo vya baa haviruhusiwi kutumiwa kama wee si mteja na hujanunua kinywaji. Nikasema ntanunua kinywaji nikishamaliza kujisaidia. Nikaambiwa hapana. Watu wengi huja pale wakatumia choo cha baa ovyo. Mkojo bado unanitesa. Nikaagiza juisi kisha nikakimbilia msalani. Kufika kule nimekuta milango miwili. Kumbuka vyoo vya wanawake si kama vyenu wanaume. Hakuna sehemu ya kusimama (urinals). Milango hiyo miwili imefungwa maana kuna wake wenza wanajisaidia. Sasa najiuliza nikojoe wapi. Nikatoka kuelekea choo cha wanaume. Kufika kule nimekuta navyo vina watu. Huyo nikatoka mbio mbio. Wala juisi niliyonunua sikuinywa. Nakimbia kama mwenda wazimu. “
Kila mtu shereheni anamtazama Mdosi. Tunacheka naye.
“Mnacheka, na mimi nacheka sasa hivi, lakini siku hiyo haikuwa vichekesho. Basi baada ya dakika kumi nimefika nyumbani. Nimefungua mlango haraka. Huyooo... nimo ndani. Nimepanda ngazi upesi upesi maana choo kiko ghorofa ya kwanza. Kufika pale nimekuta mlango umebanwa. Binti yangu katoka shule anajisaidia. Kisa? Hataki kutumia vyoo vya shule maana anasema vinamtia kinyaa. Nakwambia! Ilikuwa siku ya kisirani. Mpaka binti amalize ingekuwa kazi. Pale pale niliposimama nikajiachia. Nimeshindwa kuvumilia. Si nguo nafua mimi ? Potelea mbali wanangu wakiniona ati mama yao kikojozi.”
Kisa cha kusisimua; ila karamu la Mama Jones halisimami. Umewadia wakati wa kuimba:
“Happy Birthday!”
Mishumaa themanini inaletwa; Mama Jones anajitayarisha kuipuliza kama ilivyo desturi Uzunguni. Lilian, kitukuu cha miaka tisa kinaiwasha mishumaa. Nyanya mtu anapuliza. Tunashangilia.

Imetoka Mwananchi, Jumapili 6 Januari, 2011
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/9048-wanawake-kwenda-haja-ndogo-nje-si-rahisi

No comments:

Post a Comment