Sunday, 20 February 2011

OMBA OMBA NA WALEVI WA KIKE MITAANI LONDON...

Niko dukani nimepanga foleni. Hakuna kitu kinathaminiwa nchi hii ya Waingereza kama foleni. Mara nyingi huwaona wageni waliofika jijini London toka nchi zisizozoea kujipanga. Utamkuta mtu wa aina hiyo akivuka mstari, kabla hata hajaingiza mkono kutoa pesa alipie wenyeji watampigia kelele.
“There is a queue!” (Ipo foleni).
Basi nimo.
Mbele yangu kuna mama mmoja kibonge, tinginya, umbo la gunia. Kibonge nakwambia; mweusi, mchangamfu, sauti kubwa; ana lafidhi ya Kiingereza cha Kijamaika kinachoitwa Patois (tamka Patwaa).
Mwanamke huyu mcheshi ananikumbusha kina mama wanaouza bidhaa sokoni mjini Mbeya. Wakubwa wakubwa, waliojaa bidii, wachapa kazi.
Kabeba vyakula mbalimbali na vinywaji kama wiski na bia ya tangawizi wanayopenda Wakaribian. Wakaribian ni watu weusi toka visiwa kama Jamaika, Trinidad, Grenada, Haiti, Cuba, Montserrat, Barbados, nk. Wamejazana Uingereza. Zamu yake sasa; anapayuka:
“Duu! Nimesahau pesa nyumbani.”
Mwenye duka ni Mhindi toka Sri Lanka.
“ Paundi 25!”
(Kama shilingi elfu sitini).
Mama Gunia, gubeli, bado anafukua pochi.
Anasonya. “ Ah, hizi hapa! “
Anatoa pesa akicheka.
“Nna pesa ! Nna pesa! Unadhani sikuwa na pesa bwa’ mdogo? He! He! he!”
Shere nyingi; analipa, hatimaye. Wapo wanaotabasamu; wapo wanaoudhiwa na vigimbi vyake. Jiji hili huwa na kila aina ya mijeledi. Ni saa tano asubuhi walakin mama keshauchapa. Kinyume na walevi wengine kabeba viazi vikuu, magimbi, ndizi mbivu za manjano kubwa ambazo baadaye atazikaanga (Wakaribian huziita “Plantain”). Sasa n’naongozana naye maana anakaa mtaa mmoja nami. Kachangamka, bado anabonga, utadhani redio.
“Nimeshakaa nchi hii miaka 50! Nilikuja hapa mwaka 1960! Wakati huo weusi tulifananishwa na majibwa. Kuna sehemu ukipita Wazungu wanakupiga kama mwizi. Ilikuwa nisome miaka miwili kisha nirudi kwetu; nikasomea uuguzi, nilipomaliza sikurudi tena.”
Kwanini?
“Ah, nlikutana na brazameni ulimi wa sukari akaniloanisha mapenzi.(Anacheka kwa nguvu) Baadaye wakazaliwa watoto. Sasa wote washakuwa watu wazima, wamezaa, miye nakula maisha tu.”
Tunakumbana na yule dada niliyewaeleza juma lililopita; mnamkumbuka, Vivian? Bado yuko pale pale tulipomwacha; bado anaomba hela, nje ya benki ya Barclays.
Kavalia ile ile suruali yake ya Jeans iliyoshapauka yenye matundu na mabaka mabaka meusi kama masizi. Bado kavalia viatu vyake vile vile vya raba ya Tennis nyekundu vilivyofungwa kwa kamba chafu nyeusi; awali zilikuwa nyeupe sasa hazieleweki. Tena bado anajikuna kuna mapele makubwa mekundu usoni. Ananyoosha mikono yenye kucha ndefu chafu akimpungia Mama Kibonge.
“Queeeen Mary!”
Kibonge anamchekea.
“Yes, Vivian.”
Wanatazamana. Omba omba kakaa pale chini kajikunyata, akipigwa baridi ya Ulaya, Queen Mary (Malkia Maria) anapekua begi lake. Anatoa mkebe mmoja wa bia; anamkabidhi Vivian.
Utadhani Vivian kajengewa nyumba mpya maana tabasamu anayoitoa anapokiona kile kikopo cha bia, maalum! Ajabu pamoja na kuvuta fegi, kulala nje na kuogelea katika ulevi bado meno yake masafi meupe. Ama kweli! Mungu hupambana na shetani; hachafui vyote.
Tunaendelea na safari.
Malkia Maria bado analonga na kutoa mastori, kila baada ya hatua haachi kumsalimia mtu, kumpungia yule kule, akicheka kwa nguvu; juu yake ongezea ile tabia yake ya uchangamfu na nishai ya adhuhuri; basi nadhani wasomaji mnamwona.
“Ungegombea ubunge, Queen Mary,” namkoga.
Anabanja ghafla.
“Bwa’ mdogo. Wakiniona wanadhani mi mlevi; jimama jizee linene, kwisha kazi. Hawan’jui. Siku hizi watu humu mijini hawaangalii watu wakoje; wanaangalia tu walivyovaa wanavyotembea, wakawasema wako hivi na hivi. Ukitaka kujua kitabu kizuri usiridhike na jalada. Kifungue ukisome.”
Anacheka na kubanja tena.
“Nishapitia kila kibaya na kizuri. Nilipohama kwetu nilisemwa, mtoto wa kike nakimbiliaje Ulaya? Nikawaambia wazee msijali, n’najua ninachokifanya. Nilipofika hapa sikuwasahau nyumbani. Baada ya kuhitimu masomo ya unesi nikawa natuma pesa nyumbani. Ilikuwa nirudi lakini bahati mbaya nikakutana na yule mshikaji tuliyependana. Tuliishi pamoja miaka kumi; nikamzalia watoto watatu. Watu wazima sasa hivi. Nina wajukuu saba na kitukuu kimoja.”
Namuuliza kama baba watoto yuko hai.
“Mungu keshamchukua. Alikuwa freshi sana. Ila alifanya kosa moja. Hali kabla ya kunywa; na akinywa hafanyi kazi. Mi bado nachapa kazi za kujitolea hospitali za wazee ingawa nimeshastahafu. Mwezi ujao natimiza miaka 70. “
Anacheka.
Kwanini hakurudi kwao visiwani, Jamaika?
“Mi si Mjamaika. Unaona mlivyo mabwege? Mkimwona mtu mweusi mnasema anatoka Nigeria au Jamaika. Kwetu ni Montserrat. Unapajua?”
Ni kule mlima ulipotoa volcano mwaka 1997?
“Huko huko. Nilitaka nirudi Montserrat lakini kwa kuwa mambo ya volcano yameanza tena; nitafia hapa hapa Uingereza.”
Anacheka.
Tumefika kwake.
Namuuliza vipi akakatiwa jina la Malkia Maria?
“Yule binti ananjua...Namfahamu toka akizaliwa. Wazee wake matajiri lakini babake alikuwa fisi. Alikuwa akiwapiga wote, mama na watoto. Watoto wote wa yule mzee wameharibika. Yeye mwenyewe kahamia Hispania. Aliwaachia nyumba na utajiri lakini kutokana na hali ngumu aliyowafanya wakiwa wadogo akili zao hazikuwa nzuri; wakapoteza hela katika dawa za kulevya.”
Kesho yake ninapompitia Vivian namwangalia kwa macho mengine.
Nchi hii tajiri lakini ina kila aina ya mambo.
Kwetu Afrika umaskini hutokana na wachache kuwa na mali na kutowapa wengi. Hutokana na viongozi wasiojali watu wao na kujilimbikizia mali kama ilivyokuwa Misri. Mbabe yule katawala toka mwaka 1981 bila kukubali uchaguzi; akiwafunga waliodai haki yao, akiwapendelea wenzake na ndugu zake; akijaza mabilioni ya pesa nje ya Misri aliyodai anaipenda. Hicho ndicho kinachotudidimiza Afrika; kujenga umaskini ndani ya bara hili tajiri kushinda yote duniani.
Sasa linganisha na ufukura ulioko nchi zilizoendelea.
Omba omba na maskini wapo.
Mna hohehahe lakini si wote wanatoka familia maskini za matabaka ya chini. Ufukara, huzuni au ukiwa wao husababishwa na mambo ya kila aina.
Vivian alizaliwa mwaka 1986. Babake alikuwa mfanya biashara mkubwa. Kutokana na hali yake ile alipenda sana kazi kuliko watoto. Kwa kuwa akiwa nao watoto anakuwa amechoka huonyesha mapenzi yake kwa kuwapa zawadi na pesa. Na siku moja moja mkewe akimkorofisha anamnyuka. Watoto wakilia anawatandika vile vile. Hatimaye mkewe akatoroka na mwanaume mwingine. Akamwachia watoto wale; wawili wa kike, mmoja mwanaume. Baba mtu alivyokuwa punguani akawa anawaharibu, analala nao. Ndivyo alikoanzia hadi leo binti kageuka omba omba, kaharibikiwa.

-London, Jumatatu, 14 Februari, 2011
-Ilitoka Mwananchi, 20 Feb, 2010

No comments:

Post a Comment