Mti alionyongewa Mangi Meli Makindara wa Old Moshi mwaka 1892. Wakoloni wa Kijerumani waliua viongozi wengi. Mfano mzuri wa kumbukumbu toka Blog la Xanadu.
Kwa mfano rejea siku magaidi wa ISIS walipoharibu haribu na kuvunja vunja makumbusho ya kale ya Iraq wiki kadhaa zilizopita. Makambusho haya ni sanaa na sanamu zilizojengwa na wananchi wa zamani kabla hata dini za Kikristo na Kiislamu kubuniwa. Tukio limepingwa vikali na Umoja wa Mataifa. Hifadhi za kijadi ni sawa na makaburi na tambiko za ndugu na mababu zetu. Sasa tukio “limefutwa machozi” na Waingereza waliotangaza kuwa wanazo baadhi ya hifadhi hizo katika majumba yao ya makumbusho.
Sanaa
hizi zilizoporwa kipindi cha ukoloni ndiyo kumbukumbu pekee za mila na ustaarabu wa
Waarabu. Kwanini Mwingereza apende kuhifadhi vidude hivi? Kwanini kichwa cha shujaa
wetu Mtemi Mkwawa wa Wahehe (aliyepigana dhidi ya Wakoloni wa Kijerumani)
kikarejeshwa na kuhifadhiwa kijiji cha Kalenga? Kati ya mafuvu mengine ni lile
la Mangi Meli Ringi Makindara aliyenyongwa mbele ya watu wake Old Moshi, mwaka
1892. Jitihada za kudai fuvu hilo lirejeshwe Kilimanjaro, sijui zimeishia
wapi. Mara ya mwisho (2005), Ubalozi wa
Ujerumani ulisema kichwa hakikupatikana.
Hifadhi ni kumbukumbu.
Kumbukumbu ni historia. Historia ni muhuri wa maisha ya mwanadamu.
Ukiona wengine wanakuiga jua
unalo zuri.
Na zuri huwa haliji kwa
kukopa, kuiga, kujifanya, kutamani, kuomba, kudai. Huja kwa kuunda. Uvumbuzi
hutokana na undani wa mtu mwenyewe. Watanzania lazima tujikumbushe tunakotoka. Watoto na vijana wanaokua leo
shurti tujichunguze sisi nani. Kwamba kabla ya kuja hawa wageni tulikuwa na ngoma,
ibada, imani, mila na desturi. Leo tambiko na imani zetu zimepambwa na kufuja
utamaduni wa Kizungu na Mashariki ya Kati kuliko makabila na asili zetu. Leo
mtu mweusi yuko tayari kupigana (hata kuua) kutetea desturi hizi za kigeni.Yabidi
tujirudi na kujipenda.Lakini si rahisi.
Bado tunakabiliwa na ukosefu wa elimu (ujinga), umaskini na maradhi.
Adha hizi zimetugeuza omba omba. Na sio tu wananchi wa kawaida.
Viongozi wetu bado wanategemea misaada na kudra ya wageni. Serikali
zinaendeshwa kwa misaada. Mwaka 2010 Benki kuu ya dunia ilieleza kuwa deni la nchi zinazoendelea lilipanda kutoka
Dola trilioni 4.4 hadi trilioni 4.9 miezi kumi na miwili baadaye. Ongezeko hili
la Dola bilioni 464 laweza kuwasomesha watoto wote wa Tanzania kwa kuwalipia
ada ya dola 150 kila mwaka kwa kipindi kirefu sana.
Kama tulivyoona katika
uchambuzi wa makala mbili zilizopita fedha na vifaa vya fadhila havitolewi kwa
kila mtu. Hata hivyo wapo wafadhili wanaosaidia shida mbalimbali.
Lakini utawajuaje?
Tovuti la Forbes limetaja mashirika 50 makubwa ya fadhila Marekani. Picha ya Forbes
La kwanza kabisa jifunze
kuwa mtafiti mzuri. Lazima ujifunze
kusoma na kuelewa unachokitafuta. Fedha haipo tu kuchota. Je unajua kutafuta
habari katika mitandao? Je unaifahamu Google au Bing?
Yakubidi uelewe maneno ya
Kiingereza kama “charities”, “aid trust”, “foundation”, nk.
Ukibofya neno “charities for
Africa” (Fadhila kwa Waafrika) ,mathalan, utaukuta msururu wa mashirika
mbalimbali yanayotoa misaada barani. Wazungu wengi wanaojiunga na mashirika
haya hufanya kazi kwa kujitolea au mshahara mdogo sana.
Dhamira kuu ni kuondoa umaskini na maradhi kupitia miradi jumla.
Mara chache sana utakumbana na shirika la fadhila (“charity organisation”)
likijitangazia kumsaidia mtu binafsi. Mfano mzuri ni tajiri Bill Gates ...mwasisi wa Microsoft.
Bill Gates alipostaafu aliamua mwisho wa maisha yake utakuwa kuendeleza wasiojiweza.
Ukisoma na kuchunguza
mashirika yake ya fadhila utagundua anazungumzia
matatizo ya watoto yatima, wasichana au kina mama wanaonyanyaswa, maradhi kama
Malaria na umaskini uliozidi kiasi. Mfano mzuri wa ya misaada anayoitoa pamoja
na mkewe (“Bill and Melinda Gates Foundation”) ni mtaji kuanzisha duka la pamoja. Unaweza
kumwandikia. Lakini itakubidi ujue masharti ya shirika lake. Mashirika ya fadhila hutakiwa kisheria
kuendeleza makundi au watu waliojisajili kuendeleza jamii. Hayatoi fedha za mtaji
wa biashara ya binafsi. Lengo lake si
biashara.
Tathmini msaada wa kutokomeza Malaria unaotolewa na
tajiri Bill Gates. Ukibofya ukurasa wake
utaona akisukuma msaada wa waganga wakujitolea kupunguza adha ya malaria; ama
kusafirisha nyavu za mbu . Au kuwahudumia wafanyakazi wa kujitolea
kuendeleza miradi ya shirika, yaani kupigana na maudhi ya mbu.
Sasa utajiuliza je, Bill Gates atanisaidiaje nimalize kusoma?
Je nitamwanzaje? La kwanza kabisa yabidi usome vizuri na kujua yeye nani na
mashirika yake yana utaratibu gani? Huenda ukimwandikia atakujibu. Lakini
lazima ujue namna ya kuiandika hiyo barua. Zingatia masharti kuwa yeye hasaidii
mtu kutajirika. Hairuhusiwi.
Prince Charles. Picha ya Wikipedia
Mfano mwingine ni wa mtoto wa Malkia Elisabeth
wa Uingereza. “Prince Charles Trust” wenye misaada kadhaa ikiwemo elimu na
mafunzo kwa vijana wasiojiweza Ila wanaopewa
msaada huu ni raia wa Uingereza tu.
Sasa unapoanza kutafuta watu kama hawa lazima usome
sawasawa masharti. Nimejaribu kuandika
neno “International Grant for education” katika Google. Neno “International”
lina uzito maana ni la dunia nzima. Nimekuta shirika la “Trickle
Up.” Shirika hili hutoa mitaji kwa watu
wenye kipato kidogo, chini ya dola moja kwa siku kiwastani,
shilingi elfu moja. Hawa hupewa mtaji wa Dola 100 hadi 250 kuanzishaa
biashara au mradi mdogo.
Kwa hiyo yapo mashirika
yanayosaidia watu binafsi.
Je nimefikaje hapo? Nimesoma
maelezo. Je wewe ni msomaji mzuri au “unaotea” tu bahati?
Makala hizi tatu zimejaribu
kutomasa tomasa dhamira ya fadhila. Nimeamua kutazama mada baada ya kupata
barua na maombi lukuki ya wananchi wanaotafuta wafadhili ughaibuni. Natumaini
angalau nimechokoza utafiti wako msomaji. Na kukuelewesha wapi pa kuanzia.
-Ilitoka Mwananchi gazeti Jumapili 29 Machi, 2015.
No comments:
Post a Comment