“Mafanikio maishani yahitaji mawili; kutojua na kujiamini,” aliandika mtunzi maarufu wa riwaya, Mark Twain. Zamani shuleni tulisoma vitabu vya Mark Twain vinavyofundishia Kiingereza ulimwengu mzima. Kati ya riwaya ya sifa na sambusa ni The Adventures of Huckleberry Finn. Mashuhuri sana. Kisa chenye kejeli na utani kuhusu ubaguzi wa rangi. Nukuu, elimu na hekima za Mmarekani huyu aliyezaliwa mwaka 1835 akafariki 1910, (akatajirika kutokana na fasihi) hunyofolewa sana na wengi. Wanadamu tunapenda kujifunza kwa wenzetu waliofanikiwa kitaaluma na kimasilahi.
Mtunzi wa riwaya Mark Twain, mwaka 1871. Kitabu chake , Huckleberry Finn, hutumiwa mashuleni kujifunza Kiingereza ulimwengu mzima. Picha ya Wikipedia
Hebu tuikague nukuu hii kusaidia maongezi ya leo. Kutojua
kwaweza kuwa ujinga na Mwalimu Nyerere aliwahi kufafanua ifuatavyo...
Nahau ya Mark Twain iliongezea neno “kujiamini.”
Kwa vipi?
Viongozi wa zamani wa TANU walitueleza maadui mahsusi
barani ni ujinga, umaskini na maradhi. Kutokana na maadui hawa, (kama tulivyotathmini
safu ya wiki jana), asilimia 43 ya watoto Afrika hawasomi. Ukosefu wa elimu ni kitanda cha shida zote za mwanadamu. Chukulia theluthi mbili ya Waafrika ni vijana chini ya
miaka 30; ina maana mazingira yetu yanatawaliwa na ujinga. Na si tu elimu ya vitabuni. Kuna ulimbukeni,
unaotokana na TAABU za kijamii.
Mwalimu akiwa kijana. Hii picha ya jalada la kitabu cha maisha yake kabla hajatumbukia siasani. Kimeandikwa na Thomas Molony karibuni.
Mathalan tunaaambiwa
karibuni, mbwa ni kitoweo mahsusi cha jirani zetu Kongo, “kwa sababu, nyama ya
mbwa ni bei nafuu na rahisi zaidi kupatikana kuliko ya ng’ombe.”
Taabu zinatutwanga mithili ya mchi unaoitandika nafaka
katika kinu. Taabu, umaskini na maradhi vimekuwa utamaduni. Hata mtu anapopata wadhifa mkubwa akawa
kiongozi wa nchi atang’ang’ania hadi awe mzee wa miaka 90, ili mradi anatumia
nafasi aliyopewa na wananchi kujinufaisha yeye na ndugu zake. Anawapa kazi
rafiki zake akila na kuhakikisha
akiondoka damu yake inaendeleza jahazi. Mtu anakaa madarakani hadi anaanguka
ovyo na kuwafukuza kazi walinzi wake eti hawakutabiri alivyojikwaa? Tuliache
hilo. Tujiulize.
Wangapi wanashangazwa namna vijana wanavyogeuza kila kitu
siasa , siku hizi, maana “wanajua” ni ajira? Badala ya siasa kuwa mwongozo wa
kuendeleza uchumi- jamii; siasa imekuwa nahau na nukta ya ubadhilifu. Kila
msimu Rais wetu anatifua udongo wa baraza la mawaziri. Kasheshe, jama.
Siasa sio? Mradi ujue kusema, kudanganya na kuugeuza huo
uongo kuwa ahadi na matumaini. Tutaona uchaguzi utakavyotifua moto, Oktoba.
Penye taabu, kila mtu mjanja. Lakini hatuko
peke yetu. Dunia mviringo. Dunia ya leo
yataka taaluma na mtaji ili kuendelea.
Kuendelea vipi? Mwanadamu anahitaji makazi, mavazi na chakula aishi. Akivikosa
huhangaika na kuchanganyikiwa.
Siyo mastaajabu basi kutuona wengi tukibabaisha na kutafuta riziki popote
inaponukia. Huanza na mtazamo finyu unaoasa kuwa kila unalolitaka hutokana na
kusaidiwa na wageni.
Hapo ni “kutojiamini.”
Ukitafakari historia yetu wanadamu kila jipya
linalovumbuliwa huanzia kwa mtu binafsi.
Mara chache sana ikatokea serikali au kundi likagundua jambo zito.
Mshairi na mwanamuziki maarufu wa Kimarekani Bob Dylan. Picha ya Wikipedia
Mfano. Wasanii. Mwanamuziki na mshairi maarufu wa Kimarekani, Bob Dylan
anaeleza katika kitabu cha maisha yake (Chronicles, 2004) alipoanza utotoni
aliamua “ataandika nyimbo kubwa zaidi ya maisha atakayoishi.”
Na kweli ametimiza
azma hiyo. Ujumbe ulioko ndani ya nyimbo za Bob Dylan si wa kawaida. Historia
itamkumbuka Bw Dylan, kwa kachangia kubadili namna wanamuziki wanavyotunga
nyimbo. Awali mwanamuziki alikariri tu nyimbo za wenzake (covers).
Mwanamuziki na
mtunzi maarufu wa Kijamaika, marehemu Bob Marley, alipoulizwa alianza lini
kuimba alijibu “nilianza nikilia” akimaanisha alipotoka tumbo la mamake, akavuta pumzi,
uimbaji ulifungua dimba. Mzizi.
Mpiga gitaa na
mtunzi wa kusifika wa Kimarekani, Nile Rodgers aliyebuni vibao vilivyoshaimbwa
na Madona (Like a Virgin), Diana Ross( Upside Down), Sister Sledge (We are
Family), Chic (Le Freak), Get Lucky (Pharrell Williams), nk; alikulia shida za
umalaya, dawa za kulevya na ujambazi. Ila alipoiona maiti ya baba yake mlevi na
fukara kando ya mtaro, akiwa bado mtoto aliamua lazima afaulu maishani.
Profesa Tim Berners- Lee, Mwingereza aliyevumbua tovuti, bpepe na mtandao tunaotumia leo. Picha ya One Life Success.
Je, wanasayansi? Mvumbuzi wa mtandao (inteneti) tunayoitumia
leo, kila nyanja, ni Mwingereza Profesa Tim Berners-Lee, mzawa wa hapa London
familia iliyofanya biashara ya kompyuta.
Bwana Berners Lee alikichezea chombo hiki na mwaka 1989 akavumbua HTTP, kiini cha mtandao na tovuti. Akihojiwa mwaka
2010, alisisitiza hakugundua mtandao, bali alichofanya “ni kuyaoanisha mawasiliano haya yafanye kazi pamoja na hapo
pakatokea jipya, yaani WWW.” Kitendo kama hiki chahitaji ujue tayari jambo
unalolifanya. Kwa kuwa alishazoea kuchezea chezea tarakilishi tangu mtoto ilikuwa rahisi kuendeleza chombo hicho
ambacho kimeleta mapinduzi ya mawasiliano duniani. Profesa Berners Lee ni mfano mzuri wa mtu KUTHAMINI jambo ulilozaliwa
au kukua nalo.
Yeye na tuliowataja juu waliamua utotoni kufanya
walichokitaka bila kutetereka.
NI ushauri mzuri sana kwetu Tanzania.
Kujua unachokiweza na unachotaka kukifanya ndiyo siri ya
mafanikio yako. Wengi wetu hutaka kujibu swali HIKI KITANIFAIDIA NINI badala ya
kulenga JE MIMI NINAPENDA NINI AU ‘NAWEZA KUFANYA NINI? Mtazamo wa kuanza fikra
na azma ya kufaidi (au kujua matokeo ya)
kitendo hutughafilisha pale mafanikio yasipoonekana. Matokeo tunajidanganya
hatuna bahati, tuna mikosi; tuelekee tu kwa wachawi kuwapa vipande vya miili ya
Albino.
Mchukue mtu aliyekulia
mazingira ya ukuli, sulubu na kubeba mkokoteni.
Ikiwa ataithamini kazi ya mikokoteni na
kuijua anaweza hatimaye kuunda kiwanda kidogo, kampuni au kituo cha kuendeleza
mikokoteni. Badala yake mlalamikia Mungu. Kutamani (mosi) magari na majumba ya
fahari. Kumbe fahari ni ujuzi wako. Hili liko pia kwa mtu aliyezaliwa mazingira
magumu kijijini. Anajua kilimo. Au mifugo. Badala ya kujaribu kujiendeleza na
kile anachokimanya atavitupa. Atakimbilia mjini. Huko atakutana na wajuaji.
Atafanya asiyoyazoea. Ataitwa bwege kwa vile hajui kuendesha gari, Kiingereza
au kuvaa kinamna fulani. Ujuzi wa vijijini
utaishia mtaroni. Mifano hii
michache inaweza kupanuliwa kwa kuangalia taaluma au fani nyingine zozote kama
michezo, ususi, upishi, nk. Tumalizie mada juma lijalo.
-Ilitoka Mwananchi Jumapili, Machi 1, 2015
No comments:
Post a Comment