Sunday, 24 March 2013

USONGO WANGU NA KISWANGLISHI : WATANZANIA HATUJAKOMAA KILUGHA- 1


Karibuni, Baraza la Waganga Uingereza lilipitisha sera ya kutomruhusu daktari wa kigeni kufanya kazi bila kufuzu mtihani wa Kiingereza fasaha. Ina maana ili kutibu wagonjwa lazima uimanye lugha ya wenyeji vizuri. Wenyeji wanathamini sana lugha yao mama- bila kuichanganya nganya na kuibandika  bandika viraka.
Mwandishi maarufu wa Kiswahili fasaha, Adam Shafi akiwa Uingereza mwaka 2007. 
Picha na F. Macha

Msemaji wa Baraza hilo alipohojiwa na runinga ya “Sky” alijitoa mwenyewe kama mfano:
“Nilisoma Kifaransa nikiwa sekondari. Ninaweza kuongea Kifaransa cha kuombea maji. Ila nilipofanya kazi kwao  kama mganga nlikua na matatizo maana sikuyajua maneno au misemo ya taaluma ya uganga ipasavyo. Ikabidi niende kozi. Ni hatari sana kutibu watu kama unaboronga lugha.”
Akiwa na maana kujua lugha juu juu au sawasawa ni mambo mawili tofauti. Wenzetu waliondelea wanathamini sana kufahamu lugha sawasawa badala ya kubabaisha.
Nimetathmini sera hiyo ya Waingereza ili kuongelea suala la Ki-Swanglish ambacho kinaendelea kuzaa chawa Tanzania. Miezi michache iliyopita nilikua kwenye kikao na kundi la Wabongo wenzangu hapa Ulaya, mzalendo mmoja akauliza: “ Bwana Macha hapendi sana kuchanganya changanya maneno ya Kiingereza na Kiswahili.”
Kitabu kipya cha Adam Shafi- kinachoendeleza Kiswahili Fasaha. Picha toka Blog la KiSwahili Afrika Mashariki


Yakaanza malumbano makali ambayo ningependa kuyarudia kwa niaba yako msomaji. Nilianza kwa kusisitiza misingi ya Kiswahili- kwamba ni lugha iliyokua kutokana na kuiba na kumeza maneno na misemo ya lugha mbalimbali. Ingawa tumbo na mzizi wa Kiswahili ni Kibantu- imenyofoa msamiati toka Kiarabu, Kihindi, Kiingereza, Kireno, Kiajemi nk.
 Ndani ya mseto huu, Kiarabu kinaongoza kwa takriban asilimia 30.  Zingatia maneno yanayoishia na “a”, “i” na “u”  yametokana na Kiarabu : “Basi,” “ Yaani,” “Salamu”, “Mustakabal”, “Maktaba”, “Mhariri”, “Rais”, nk. Au maneno ya dini za Kikristo na Kiislamu yaliyochangia misemo kama “Amina”, “Mtume!”,”Toba!”,  “Yarabi! Yarabi”, “Wallahi Laadhim”, “Inshallah”, “Ubarikiwe!”,  nk.  Yapo pia maneno yaliyobatilishwa; mathalan “Tajiri”, Kiarabu ni Mfanya Biashara, “Rijali” (  “Rajul” ni mwanaume), “Khata” Kiswahili ni kukanusha , Kiarabu ni “Kosa”, ”Dhana” Kiarabu ni “Kufikiria”, “Timamu”- kutimia, Kiarabu ni “Vizuri” nk.
Usomaji vitabu vya Kiswahili na Kiingereza ni muhimu kuboresha lugha. Picha na O. Macha, Arusha, 2011.

Kihindi na Kiingereza hivyo hivyo. Mfano mzuri ni vyakula na mavazi. Maneno na vyakula tuliyozoea kama “Chapati” , “Biriani”, “Binzari”, “Pilau” yamefanywa yetu toka kwa Wahindi. Si ajabu unapomuuliza mwananchi yeyote kwamba chakula cha Kitanzania nini hatakosa kutaja misosi hiyo- maana imeshamezwa na joka ambalo ndilo lugha yetu mahsusi.  Kiingereza nacho kimechotwa sana tunavyojua mathalan, kimavazi: “Gauni”, “Sketi”, “Sweta”,  “Suti”, “Koti”, “Shati”,  “Soksi”, nk. Au vyombo vya starehe ; “Tarumbeta”, “Wiski”, “Redio,”nk
Sasa mseto huonekana dhahiri hivi: “Jamaa alivaa shati nadhifu rangi nyeupe akakaa mezani tayari kula”, Hapo chambua: Uhindini (“Rang”), Uingereza (“Shirt”), Uarabuni (“Nadhiif”), Ureno (“Mesa”) nk, yamechanganywa kuunda Kiswahili ambacho historia yake ni kutafuna na kumeza maneno ya lugha nyingine.
Ila lijapo suala la Kiswanglish tunakabiliana na lugha inayopachika sentensi nzima za Kiingereza katika Kiswahili. Ilikua zaidi pale Mswahili (hasa aliyesoma) alipodai hapati neno linaloelezea anachokitaka. Huu ni uvivu tu kwani lugha ya Kiswahili inajitosheleza kimsamiati na haihitaji kukopa, kuiba.
Tabia ilianzia pale  kukua kwa mitandao na mawasiliano ya mtandao wa Kiingereza kulipotudanganya kuwa iko haja ya kujifaragua kwa kujifanya eti wajuaji kwa vile tumeweka neno moja au mawili ya Kimombo. Kwanini sisi tu ndiyo tunaotaka kujionyesha kwa kubandika maneno ya Kiingereza katika lugha ya Kiswahili inayothaminiwa sana ulimwenguni? Tunasahau kwamba Kiswahili ni kati ya lugha muhimu zinazokua upesi ulimwenguni kwa miaka kumi sasa? Siri ya ulimbukeni wetu nini? Tunajidunisha kiasi gani hadi tudhani kuvaa shati la mwenzako ni maendeleo?
 Sasa tutazame kauli ya pili.
 Sio sisi tu tunaochanganya lugha. Yapo mataifa ya Kiafrika yenye tabia ya kupamba lugha zao na za Kizungu- Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Afrika Kusini.
Wakenya ndiyo walioanza mchezo huu wakaunda “Shenge” iliyostawi sana jiji la Nairobi, miaka ishirini iliyopita. Shenge ni mseto wa “Swahili na English”- kama lilivyo neno Swanglish. Miseto ya aina hii ipo pia kwa Waspanyola wa Marekani wanaoongea “Spanglish.”
Hapa kuna muhimu la kukumbusha.
Kidesturi majirani zetu hawa wanaongea Kiingereza fasaha kabisa. Hata Mkenya ambaye hakumaliza sekondari hana matatizo ya lugha hiyo sababu wao wamekua karibu na Wazungu na shule zao zimeendeshwa Kizungu toka enzi za mkoloni. Ukisikiliza hotuba au mahojiano wakati wa uchaguzi  Kenya mwezi jana, ukisoma blogu, maandishi na fasihi, utaona Wakenya wanakimanya Kimombo vyema. Na ndiyo moja ya sababu wanazitwaa kazi za ajira hapa Bongo.  Tatizo la wengi – ukiondoa wananchi wa Mombasa na pwani- huja pale wanapoongea Kiswahili. Huanza kuazima azima maneno ya Kiingereza-kwa mintaarafu ya kujazia msamiati. Kwa hiyo tatizo lao ni msamiati-kuliko lugha – na tatizo hili ndilo lililozusha lugha ya  “Shenge” kufidia.
 Hapo hapo licha ya kutukuza Kishenge, kitaaluma, Wakenya wamekua mstari wa mbele kujenga lugha ya Kiswahili. Kila unaposoma majarida mbalimbali ya Kiswahili utawakuta maprofesa na waalimu wa Kiswahili, Kenya wakipeperusha mambo muhimu. Mmoja wa wataalamu hawa ni Sheikh Ahmed Nabany,  bingwa wa kuunda maneno.
Moja  alilounda miaka ya Tisini ni “runinga” –mseto wa “rununu” (sauti kutoka mbali) na “maninga”(macho yaonayo mbali).
Bango au tangazo la kutetea wanyama pori- lililoandikwa kwa Kiswahili fasaha miezi michache iliyopita. Picha na Kidon Ngoille...

 Mwingine ni Profesa Ken Walibora mwanafasihi makini anayepigania sana uandishi na fasihi ya Kiswahili (alihariri mkusanyiko wa hadithi fupi za waandishi Waafrika wa Kiswahili na Kiingereza uliotafsiriwa Kiswahili- “Damu Nyeusi” akishirikiana na Mtanzania  Profesa Said A. Mohammed, 2007) na karibuni kafanya uhakiki   wa kitabu kipya cha Adam Shafi –“Mbali na Nyumbani” kilichochapwa Nairobi na “Sasa Sema” (Longhorn Publishers).
Kwa miaka mingi sana Kenya wamechapa vitabu vya Kiswahili. Waandishi wakubwa wakubwa wa Kitanzania- Adam Shafi, Mohamed S. Mohamed na Said A. Mohammed wote wamechapa na wanaendelea kuchapisha vitabu Kenya.
Kenya wamezalisha nyimbo za Kiswahili- “Malaika”, “Jambo Jambo” (Hakuna Matata), “Sina Makosa”(Simba wa Nyika bendi ya Watanzania wakazi Kenya), “Mambo Bado” (Makassy)nk zilizowika duniani na kutuletea sifa Waswahili. Hapo hapo waandishi wakubwa wa Kiingereza bara Afrika wanatoka Kenya-  Ngugi wa Thiong’o, Meja Mwangi, David Mailu na Binyavanga Wainaina- waandishi wenye sifa za kimataifa. Hivyo tunaposema wanachanganya lugha si tu wanatambua umuhimu wa lugha zote mbili, wanazijua fika.
Tumalizie mada juma lijalo.

Ilichapishwa Mwananchi Jumapili...24 Machi, 2013.

No comments:

Post a Comment