Baada ya kuandika kuhusu maradhi ya moyo na kichomi yanavyodhalilisha vijana leo, mwezi Novemba, Watanzania wengi waliniandikia kutaka ufafanuzi kuhusu mazoezi na uinuaji vyuma. Mazoezi na uinuaji vyuma ni mada muhimu sana.
Suala la kwanza ambalo pia limeenea barani Afrika ni kwamba kazi ngumu (sulubu) ni sawa na mazoezi. Eti kama mtu anatembea kwenda kazini au anayo maisha ya taabu yanayoutoa mwili jasho kila siku basi hilo ni zoezi tosha.
Kwa miaka mingi nimeandika jinsi ambavyo mazoezi ya mwili na kazi ngumu za sulubu vilivyo vitu viwili tofauti. Watu wengi wanadhani ili mradi unatoka jasho au unataabika basi mwili wako unachongeka kiafya.
Pana ukweli kwamba mtu anayefanya kazi za sulubu na yule anayefanya kazi za kukaa, akienda kwa gari lenye kiyoyozi,maua na muziki wanapishana, kiafya. Lakini je, kwanini kitakwimu, wafanya kazi za sulubu, makuli, hohehahe wanayo maisha mafupi kuliko maofisa wanaoishi maisha ya burudani?
Hata lugha ya Kiingereza imewagawa wafanyakazi hawa kati ya “blue collar” (wanaovaa magwanda machafu) na “white collar” (mashati meupe na tai). Kitakwimu dunia yetu imeendelezwa na kuongozwa kifikra na watu wa tabaka la kati wenye muda wa kufikiri, wanaokula vizuri na kuvuta hewa safi ya bustani na chemchem nje ya miji mikubwa mikubwa. Kazi ngumu ya kusafisha, kujenga na kustahimili dunia yetu hii kimazingira hufanywa kwa mikono ya wavuja jasho, ambao maisha yao huwa magumu na mafupi, kitakwimu.
Tuulizane. Je, mazoezi yatamsaidiaje mvuja jasho?
Na mazoezi ya viungo ni nini?
Kutokwa jasho kunasaidia kuchuja mafuta lakini si mazoezi. Mazoezi maana yake ni kitendo kinachoukimbiza moyo, kinachomfanya mtu aheme na kinachonyoosha, kusafisha na kurekebisha viungo, mifupa, ngozi na musuli. Zingatia neno kurekebisha. Ingekuwa kazi za sulubu ni mazoezi maskini wasingekuwa wanaumwa migongo, mabega, vichwa na kusakamwa na mishipa ya ngiri. Maumivu au maradhi haya ni matokeo ya kazi hizo na huwasonga wananchi wengi kadri wanavyozeeka.
Yanachokifanya, mazoezi ni kuleta ahueni katika mwili uliochoka; kuujenga na kuukarabati. Unapofanya mazoezi ubongo hutoa dawa ya furaha na ahueni katika viungo vyote kama ambavyo mbolea inavyostawisha mboga na matunda. Jina lake la kitaalamu ni Dopamine.
Tunapokosa Dopamine tunaambulia kunywa pombe au kuvuta bangi na sigara; tukiipata tunajiendeleza ki-Bruce Lee na Ki Obama Obama.
Kufanya kazi ngumu bila mazoezi si vizuri hata kidogo. Ila kama unafanya kazi ngumu unatakiwa ujue ni mazoezi gani yanayokufaa. Kama kazi yako ni ya kuhema, kutembea (mathalan kwenda kazini kwa baiskeli ama kusukuma mkokoteni) huna haja ya kufanya tena mazoezi ya nguvu. Yapo mazoezi unayotakiwa kusawazisha nguvu zilizopotea na kurejesha mpya. Nitafafanua baadaye chini.
Tuje swali la pili. Baadhi ya wasomaji walioniandikia wamesema hukimbia na kuinua vyuma kila siku. Wanataka kujua ubaya wake maana niliandika awali si vizuri.
Yapo mazoezi ya aina mbili. Mazoezi yanayokufanya uheme na kutumia nguvu mfano kukimbia, kuogelea, kuinua vyuma, baiskeli, mpira, ngumi; ambayo huitwa Cardio. Hiki ni kifupi cha neno, Cardiovascular, ambalo maana yake ni mahusiano ya damu na moyo. Mazoezi haya huupa mwili nguvu na kuufanya usichoke (stamina). Wanajeshi na polisi mathalan wanapoanza mafunzo hubidi kufanya sana Cardio kusudi wasitaabike vitani au doriani.
Mtindo wa pili wa mazoezi si lazima ukufanye uheme lakini huupa mwili, kheri. Ni wa kujinyoosha nyoosha ambao unataka upole, pumzi ndefu na utaratibu. Haujulikani kwa wengi. Mara nyingi mtindo huu wa mazoezi hutumiwa katika mazingira au nyakati maalum. Mathalan mtu akiwa mgonjwa wa moyo, anatakiwa atembee kila mara taratibu katika bustani au kupunga upepo. Pengine alivunjika au kuteguka sehemu nyingine ya mwili sasa budi afanye mazoezi na kusingwa na mganga wa musuli na mishipa (Physio-therapist) kurejesha kiungo katika hali yake.
Mfumo wa mazoezi haya una taratibu mbalimbali kama Yoga, Pilates na Tai Chi Chuan. Yoga asilia yake ni India na huongozwa na uvutaji pumzi. Kwa mfano kama unanyoosha mikono juu unavuta pumzi ndani; ukishusha unatoa pumzi nje. Kitendo hiki cha kuzingatia uvutaji pumzi sahihi hutumiwa na akina mama wanapojifungua.
Mazoezi ya Yoga yana mpangilio ulioundwa miaka elfu nyingi sana kunukuu mienendo ya maumbile (miti na mimea) wanyama (mbwa, paka, nyoka) na husaidia viungo ndani ya mwili.
Pilates haipishani na Yoga ila ni mtindo uliovumbuliwa karibuni na Wazungu kutumia vifaa. Kazi yake kuu ni kujinyoosha vizuri vile vile. Tai Chi Chuan toka China si tofauti kimsingi na Yoga ila ni pia mapigano ya taratibu kama uchezaji densi.Huujenga uwiano wa mwili, damu na akili mwilini. Nchini China, Tai Chi inapendwa sana na watu wa makamo na wazee. Tai Chi hufanywa nje na hupendeza sana kutazama.
Mtindo huu wa pili wa mazoezi unaitwa Neuro Vascular na umelala katika kujinyoosha( stretching). Tunaweza kuelewa maana yake vizuri tukimwangalia paka. Paka ni mnyama mwenye maisha marefu na mazuri kutokana na kujinyoosha nyosha kila mara. Kinyume na yale ya haraka haraka juu (Cardio) Neuro Vascular huhusisha mishipa na viungo vya ndani yaani figo, moyo, ubongo, tumbo, mishipa ya fahamu, uti wa mgongo, hata ngozi na nywele.
Ni vizuri kufanya mazoezi haya kila siku; ikiwezekana mara mbili maana yanatuliza. Ili kujenga mwili wa afya ni vyema kufanya mazoezi haya baada ya kumaliza yale ya haraka na nguvu. Ama kama wewe mtu wa kazi za sulubu zinazohemesha vyema kuyafanya baada ya kuoga; kama dakika kumi kumi na tano kila siku. Unaweza pia kuyafanya ukiamka kabla ya kutafstahi na jioni kabla ya kula au kulala.
Wafanya mazoezi wanapaswa kwanza kabisa kuzingatia kwamba ufanyaji wa mazoezi ya nguvu (Cardio) hautakiwi kila siku. Ni vyema kufanya mara tatu kwa juma; yaani leo tizi kesho kupumzika na kadhalika. Jilinganishe na shamba. Ukiweka maji mengi katika mimea kila siku utaiozesha. Juma lijalo tuangalie kwa undani utaratibu wa mazoezi ya viungo kwa wasio na muda; ulaji kwa wasio na uwezo na ufafanuzi zaidi kwa wainua vyuma.
-London, 20 Desemba, 2010.
Makala hii ilitoka Mwananchi, Jumapili 26 Desemba:
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/38-johari/7749-mazoezi-kuinua-vyuma-kwa-wabongo
No comments:
Post a Comment