Sunday, 14 January 2018

WATANZANIA TUWE WABUNIFU WA KADI NA SALAMU MITANDAONI...



Sikukuu kubwa mbili zimepita : Krismasi na Mwaka Mpya.
 Nyakati hizi , hushuhudia salaam kem kem mitandaoni, kupitia simu.  Ila, al kheri  zinavyotumwa ni tofauti sana kati yetu Waafrika na wenzetu Weupe.

 Chukua mfano wa kadi za Krismasi. Uzunguni msimu huwa wa barafu na mavazi mazito kuzuia kibaridi kikali kinachofukuta fukuta mifupa na ngozi. Wenyeji hucheza nje. Watoto hupigwa picha wakibingirishana juu ya barafu na mbwa au vidude vingine vya Kizungu. Wenzetu wanapotumiana salamu za sikukuu huwasilisha picha za pale walipo kama “wajihi wa kumbukumbu.”
Ila sisi?
 Wavivu sana.
Msimu sikukuu huwa kero tupu kutokana na kadi zilizochomolewa mitaandano kwa maneno ya Kiingereza, au viji-video vilivyopokonywa ugenini. Kati ya wimbo maarufu unaosambazwa miaka mitatu, minne sasa ni ule wa Kispanyola  : “Feliz Navidade, Feliz Navidade...”
(Krismasi ya Furaha, au Kheri za Krismasi).
Bahari ya Nungwi- Picha na F Macha, 2011. Mfano wa mandhari zinazoweza kutumiwa katika kadi zetu badala ya kukopi kopi tu mitandaoni.

Wanaotandaza video zaidi ni sisi Waafrika. Nadra sana utumiwe salamu za mtu akikuimbia kwa Kiswahili ( au hata hicho Kiswanglish kinachosujudiwa siku hizi). Picha zinazopeperushwa si za mazingira ya pale mtumaji aliko bali kadi iliyonyofolewa mitandaoni, Uzunguni.
Mbali ya picha za namna hii (ingawa za bure,  huwatajirisha waliobunia) huwa maneno yaliyonukuliwa vile vile yalivyotumwa  ( “copy and paste”...) - mtindo huu wa kutapika kila unachorushiwa huchusha zaidi  pale mtumaji anapodai: “Kama kweli unanithamini wasambazie wenzako wengine 10...”
Niliwahi kupokea moja iliyonitaka niwasogezee wengine 50 la sivyo itakuwa balaa.
Barua hizi za minyororo au foleni (“chain letters”) zinakumbusha enzi za kabla ya huu mtandao kuwepo.  Iligharimu sana kununua bahasha na stempu. Leo haigharimu; ila hutafuna muda na nafasi katika simu zetu (“data”).
Ni upuuzi uliobuniwa kughasiana.
Na tunaopatikana zaidi ni sisi Waafrika. Kwetu  teknolojia bado  “kipya kinyemi.” Wenzetu waliogundua- hawayafanyi tena.
Jingine ni usambazaji video bila maelezo (“caption”).
 Mpokeaji ukifungua unakutana na mambo.
Ipo moja mathalan  kuhusu jamaa fulani mwenye lafudhi ya KiNigeria....( haina jina wala maelezo). Jamaa anasema keshasafiri sana bara Asia. Kule  wenzetu hawasubiri kuomba omba kwa Wazungu kama sisi. Wanachapa kazi.
 Anatoa mfano wa Cambodia na Vietnam.
Itakumbukwa jinsi Vietnam ilivyotwangwa mabomu na Wamarekani - 1965 hadi 1975. Ukatili haukuwa tu kuua wananchi wasio na hatia vijijini, bali kuharibu mimea, mifugo na ardhi. Bomu lililoitwa “napalm” lilitumiwa. Napalm iligunduliwa na mwanasayansi Louis Fieser (1942). Ni  kama maji yanayochemka kwa joto la mara 8-12 zaidi. Moja likidondoshwa husambaa kiasi cha mita 2,000. Zaidi ya viwanja kumi vya mpira.  
Sasa Vietnam, Korea na Cambodia anasema jamaa katika video, (licha ya maangamizi)  hazina umaskini kama wetu.  Bara Asia linakimbia kimaendeleo.  Tumejitawala zaidi ya miaka 60 sasa baada ya Uhuru lakini bado hatuna ubunifu.
 Udhaifu huu unajionyesha katika jambo dogo kama hili la salamu za sikukuu. Badala ya kupiga picha za mandhari zetu, familia au kuandika maneno yanayotuhusu tunatapika tu yaliyoshabuniwa na wenzetu mitandaoni na kusambaza kikasuku.
Zamani ilikuwepo sera iliyoitwa Ujamaa na Kujitegemea. Kati ya nguzo zake kuu ndizo hiyo. Ubunifu na Ugunduzi.

-Chapishwa Mwananchi Jumapili , 7 Januari, 2018


No comments:

Post a Comment