Ingawa muda umepita tulioko Ughaibuni tunawapa pole waliofiwa Karatu. Tumeangalia
picha zilizosambazwa kwa uchungu, maastajabu na majonzi. Kama mzazi picha moja
iliniuma sana. Watoto wa Lucky Vincent wamesimama wakijitayarisha kuondoka safari yao ya
mwisho. Wamevalia mavazi ya shule: furaha
ya mtoto. Masomo, maisha, matumaini.
Ila picha inayostahili
kujadiliwa zaidi ni ya wanaume kadhaa wakikwea basi , wakijaribu
kunyofoa maiti zilizojibana bana. Hapa
ndipo kilipo kilinge na janga letu Waafrika leo.
Kuna jamaa nilikuwa nazungumza naye, mzawa wa Trinidad. Alipoona picha akamaka kwa hasira:
“ Karne zilizopita
tumeona Warumi wakitawala, kisha Waingereza , Wamarekani , na hatimaye itakuwa
Waafrika. Lakini kipindi hicho mali zetu zote zitakuwa zimeporwa...bara
halitakuwa tena na madini wala mimea. Tutakuwa juu lakini maskini kirasilmali.”
Akiwa na maana gani?
Utajiri wetu hausemeki. Ila bado maskini. Tunaibiwa neema zetu, ama
kwa kuuza bei nafuu au kwa wageni kuzipora kwa mwendo mkali. Na hizi safari za
mabasi ya umma zinazidi kuwa za utata na huzuni. Si kwamba Wazungu au wenzetu
wengine hawapatwi ajali. Wanapata, tena sana. Ila hujifunza.
Hapa Uingereza
mathalani miaka 40 iliyopita ajali za mabasi zilizidi. Baada ya uchunguzi na
utafiiti ikapitishwa sera kuwa mabasi hayaruhusiwi kukimbia zaidi ya kilometa
30 kwa saa. Mabasi ya shule , vyuo na wagonjwa hayakubaliwi mwendo wa zaidi ya
kilometa 20. Unapopanda basi la kadamnasi hutegemei dereva kukimbia. Mabasi
yana mikanda na hiyo ndiyo huzuia wasafiri kubingirika na kupasuka vichwa
yanapobwagika.
Au tudadavue ndege ya Lufthansa iliyoanguka milimani
Alps, Ufaransa, Machi 2015. Abiria 144
wengi wao wanafunzi wa shule walifariki. Ndege za Lufthansa huwa hazidondoki
ovyo. Baada ya uchunguzi kufanywa iligundika kuwa rubani wake, Andrea Lubitz,
alipindua ndege makusudi, ili kujiua mwenyewe shauri alikuwa na matatizo yake.
Bw Lubitz alivizia rubani mwenzake alipokwenda msalani akafunga mlango kwa kitasa.
Baada ya angamio uchunguzi mkali ulifanywa na sasa
imepitishwa sheria kuwa marubani hawaruhusiwi kukaa peke yao chumba cha
kuendesha. Juu ya hapo vipimo kamili vya kiafya vinatakiwa kufanywa kwa
marubani kabla ya kuendesha ndege.
Jingine lililowatokea wafiwa ni malipo ya fidia ya Euro
50,000 kwa kila familia. Baada ya majadiliano fedha ziliongezwa. Ingawa fedha
hazirudishi marehemu hii inaonesha thamani ya makampuni haya makubwa kwa
wasafiri wake.
Mbali na masaibu, mafunzo yamepatikana na sheria (na utaratibu)
rasmi kupitishwa.
Je sisi tutafanyaje kuzuia majonzi kama ya Karatu
hayatufiki tena?
Ilichapwa Mwananchi Jumapili 14 Mei 2017
No comments:
Post a Comment