Sunday, 20 December 2015

MGANGA MKUU UINGEREZA AONYA SIHA YA AKINA MAMA INAVYOTUATHIRI SOTE





Mganga mkuu Uingereza, Profesa Sally Davies, (pichani juu ) ,  amesisitiza umuhimu wa afya ya akina mama kwa taifa zima. Katika waraka aliouchapisha siku chache zilizopita-  kubadili kabisa mustakabal wa wanawake -Profesa Sally Davies alitaja mambo sita kisera na kiserikali. Mganga huyu aliye kati ya wanawake wachache wenye nguvu sana Uingereza ( kufuatana na kura ya Radio BBC 4, mwaka juzi), kitaaluma hushughulika na  maradhi ya damu, yaani “haematology”... 
Mfano mzuri wa jinsi damu inavyoathiri maumbile na afya yetu ni kama UKIMWI au saratani ya damu (“leukemia”) iliyomuua mwasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere, 1999.
Mapendekezo aliyoandika  yanayotegemewa kutekelezwa mwakani yalipandisha unene, utosini. Alisisitiza “unene wa wanawake” ni jambo hatari kama ugaidi, vita, mafuriko ya maji na “maradhi tsunami” mathalan,  Ebola na UKIMWI.
Akitoa takwimu alisema nusu ya wanawake wa Uingereza wenye miaka 34 hadi 44 na theluthi mbili ya walioshapitisha 45 ni wanene au wamezidi uzito unaotakiwa.  “Hiki ni kiasi kikubwa kuliko nchi zote za Ulaya,” alikaririwa.
Akihimiza suala la unene wa mwanamke ulivyo muhimu alitaja kipindi cha mimba kinavyoathiri  afya ya mtoto. Profesa  Sally Davies: “, Wazo lililoenea  kuwa mja mzito ale msosi kwa ajili ya watu wawili, sio sahihi.”
Kwanini hoja hii ni muhimu?
Mganga Sally Davies,  (mwenye umri wa miaka 66 na watoto wawili wakubwa),  alifafanua kuwa afya ya mwanamke akiwa mja mzito huathiri siha ya wanawe, wajukuu na vizazi vya baadaye.
“Badala ya kufuata ushauri wa jadi kula kwa wawili (mama na mtoto), wanawake wenye mimba wanatakiwa waambiwe kufuata masharti ya chakula bora na maisha ya afya. Masharti haya ni kula matunda na mboga zaidi. Wafanye pia mazoezi na kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe.”
Maneno haya yanatazamiwa kuwa ndani ya mlolongo wa mapendekezo mengine (tutakayoyaona chini) kwa Wizara mbalimbali  mwezi ujao.
Hebu tuvute hatua nyuma kidogo.
Je, yanatuhusuje , Afrika?
Matunda na mboga kwa wingi Afrika. Picha ya soko mojawapo Unguja na F Macha 2011

La kwanza kuzingatia hapa ni sayansi. Sayansi haina kabila, mazingira au taifa. Sayansi ni elimu inayoangalia suala lililofanyiwa utafiti na kufikiwa uamuzi wa hakika. Si lelemama au uzushi. Zamani wanadamu waliamini dunia ni kama meza. Ukienda mbele ya upeo wa macho utaangukia gizani. Miaka 100 iliyopita hatukuwa na simu. Leo hatuna tu simu za mezani bali tunazo mifukoni na viganjani. Wengi leo hatuwezi kabisa kuishi bila chombo hicho. Mawasiliano ni mepesi na haraka sana.
Miaka 100 iliyopita waganga walishindwa kutibu kifua kikuu. Miaka 30 nyuma, UKIMWI ulikuwa sifuri, tufani na kitendawili. Leo UKIMWI unatibika.
Karne moja  iliyokwenda, wanawake, hawakusikilizwa. Kazi yao ilikuwa kupika na kuzaa tu, basi. Leo tunao wanawake marais , mawaziri, mawakili, mamilionea na wanasayansi. Kauli yake Dokta Sally Davies imesimama katika mtazamo wa kwamba kitendo anachokifanya mwanamke, tupende tusipende kinaathiri kila mmoja wetu. Mwanamke asipokuwa na afya nzuri atazaa kiumbe mwenye hali mbaya.  Ndiyo maana kwetu Afrika ni muhimu kuzingatia (na kujifunza) hilo.


Mengine Profesa Sally Davies aliyolenga yalihusu mambo tusiyoyajua sawasawa au tukiambiwa tunaziba macho na masikio na kujifanya hayapo. Matano makuu.
Baada ya unene ni kuvunjika kwa hedhi, yaani pale mwanamke anapofunga kizazi. Wastani wa kipindi hicho ni miaka 45 hadi 55. Lugha ya kitaalamu ni “menopause”... 
 Mwanamama hubadilika kama enzi alizokuwa balehe. Ingawa si wote huwa na ishara zinazofanana, ila tukio kuu huwa  kukatika kabisa hedhi. Pili, baadhi ya ishara nyingine kuu ni kuona mwangaza na joto la ghafla (“hot flashes”) usoni, kooni na kifuani. Kuchuruzika jasho sana usiku, moyo kwenda kasi, maumivu ya kichwa, uchovu usio na msingi na kutokulala sawasawa. Kutokulala sawasawa huathiri zaidi wanawake kuliko wanaume. Matokeo ni mabadiliko ya ghafla ghafla ya tabia kama hasira za karibu na kutokuwa na simile.
 Tatizo hili ni kubwa sana kwa wanawake wa makamo.
 Dk Sally Davies alichopendekeza ni  jamii ( kupitia taasisi na uongozi wa  kazi) kuwa tayari kutambua wanawake wanachokipitia.
 “Sitaki wanawake waumie kimya kimya. Itakuwa vyema mameneja makazini wawe tayari kuwaruhusu kujisikia huru kujadili suala hili la “menopause” kama yalivyo matatizo mengine kazini.”
Pendekezo la sera, aghalabu, ni kuwaruhusu wanawake kupewa likizo fupi au mapumziko pale jambo hilo linapokuwa baya zaidi kazini.
 Afrika mambo haya bila shaka yapo ila kutokana na mila na desturi hayazungumziwi na hata kuyaandika hubanwa. Wanahabari wangapi wako tayari kuchambua mada kama hii? Wanawake wangapi wa ngazi za juu Tanzania bara na visiwani wako tayari kutathmini tatizo hili hadharani? Je jamii yetu inalionaje suala ?
Mengine aliyopendekeza  Profesa tunayemwongelea, ni waganga na wauguzi kujua au kutambua pale mwanamke akiwa  na majeruhi aliyoyapata katika unyumba wake. Mara nyingi mwanamke huwa kapigwa na anapokwenda hospitali huongopa. Atasema jeraha lilitokana na kuanguka au kuumia tu kiholela.
 Alichosisitiza Mganga huyu Mkuu Uingereza ni wahusika mahospitalini kujua namna ya kutambua pale majeraha ya mwanamke yanapotokana na unyanyasaji. 


La nne, ni ukeketaji na kubakwa. Takwimu zilizotolewa na mganga mhusika wa tiba ya ukeketaji, marehemu Dokta Efua Dokernoo, OBE, pichani juu (aliyefariki mwaka jana) London, zilisema kiasi cha wasichana na wanawake  waliokeketwa  (wenye  miaka 15-49) toka jamii za Afrika na Mashariki ya Kati na bara Asia wanaishi sasa, Uingereza.
Idadi yao iliongezeka kutoka 66,000 (mwaka 2001) hadi 103,000 mwaka 2001. Hii inaonesha, alisema, hayati Dk Efua Dokernoo kuwa wanawake waliokeketwa (au wanaoendeleza mila hii) Uingereza inazidi kuongezeka. Hatujazungumzia huko walikotoka.
Ndiyo sababu karibuni serikali ya Uingereza imezidisha ukali kuhusu jadi hii kale inayotesa mamilioni ya wanawake. Hadi sasa kilichozuiwa si tu sheria bali pia waganga na wanaserikali kutojua namna ya kupambanua au kutambua tatizo.
Mengine ni saratani ya kizazi na kuzuia mimba hasa kwa wasichana wanaosoma bado.
Si kila  wenzetu Wazungu wanalofanya, la kuigwa. Ila kwa yaliyochunguzwa na kutathiminiwa na wanasayansi, hayana ubishi. Tuyatafakari.



 Ilitoka Mwananchi Jumapili 20 Desemba, 2015

(zingatia  kuwa  maneno machache mwishoni yalikatwwa na kutohaririwa sawasawa)

No comments:

Post a Comment