Amanda Rodgers akimbusu mbwa aliyefunga naye ndoa. Picha ya Medavia
Majuma mawili yaliyopita
habari za mwanamke wa London aliyeoana na mbwa wake aitwaye Sheba zilitangazwa na gazeti la Metro. Metro hutolewa bure, kila siku, kwa wasafiri miji mbalimbali ya
Uingereza. Baadaye Bi. Amanda Rodgers alipohojiwa na ITV mjini London alidai : “Nafahamu ndoa yangu
na Sheba haitambuliki kisheria. Lakini ilikuwa njia nzuri ya kuonyesha
ninavyomthamini Sheba. Sheba amekuwa nami miaka mingi, hunichekesha na
kunifariji ninaposononeka. Sikuweza
kumpata mwenzi mwingine wa maisha kama huyu.”
Huyo ni Mbwa anayeongelewa, babu eh.
Mwenzenu alishachoka, aisee.
Baada ya kuishi na wanaume wawili, kuyeyushwa na mahusiano na kero akaamua. Aaakheri
mbwa. Tena tunakosea hapa tunapomwita mwenzie, mbwa. Mila ya wafuga mbwa wa ndani(
kinyume na walinda nyumba, wanaosaidiana
na polisi nk) ni kuwa nao kama sehemu ya familia, kuwatunza na kuwapa majina
mithili ya ndugu yeyote wa damu. Hivyo Sheba (ambaye ni mbwa jike) alitimiza
kanuni za mapenzi ambazo mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 47 alizihitaji.
Kwani siri ya mapenzi ni nini,
huuliza wanasaikolojia?
Niambie msomaji. Siri ya
fenesi la moyo nini?
Wimbo mmoja wa Taarabu
uliwahi kushauri zamani : “Ukipenda Pendeka...”
Amanda Rodgers keshaishi miaka
47, ndiyo.
Miaka arobaini na kitu kwa
mwanadamu huitwa “umri wa makamo” kwa Kiswahili. Bado uzee kushtadi hakika, bali kukomaa kimaisha; kupitia mengi hata
ikibidi kujaaliwa kajukuu. Lakini si
wote tunaojaaliwa haya...
Hapa Uzunguni ndoa zimefikia
kilele cha ugumu siku hizi. (Ugumu kiasi ambacho ndoa za jinsia moja zinapigiwa
madebe kukidhi haja...!)
Kihistoria, miaka 50
sasa Uhuru na Ukombozi wa akina mama
umeleta maendeleo katika uchaguzi wa kazi na taaluma, mahusino na wanaume, malezi ya wanao,
kujiamini na kujituma, nk. Hapo hapo maendeleo haya yameporomoka kiuwiano.
Wanawake wamekuwa wahitaji na wakali zaidi, na matokeo ndoa hazidumu. Wanaume
wanakimbia majumbani. Habari za baadhi ya
midume kuzaa kisha kuua watoto, mke na wao
wenyewe zinazidi kuenea. Wanaoumia ni watoto.
Katika hali hii “ngumu” unawakuta wachache wanaoamua bora kuoana na viumbe
wengine kuliko wana-Adam.
Kuna habari za waliooana na
nyoka, samaki, hata waliofunga ndoa na “vitu”
walivyovihusudu mathalan, madaraja, viwanja vya kuchezea nk. Yanachekesha,
yanastaajabisha, yanakondesha, yanasikitisha.
Ila mahusiano mazuri kati ya
mtu na mbwa ndiyo mbingu.
Mbwa ni kiumbe anayethaminiwa
sana Uzunguni. Nakumbuka mara yangu ya kwanza kuzozana na utamaduni huu nilikuwa
naishi Ujerumani mwaka 1985. Mmoja wa
jirani zangu alikuwa na mbwa mwenye tabia mbili zilizoudhi sana. Kwanza hubweka
usiku na mchana kutokana na kufungiwa ndani na kuhasiwa. Wazungu huwahasi wanyama
kuzuia kuzaa zaa ovyo. Hii ni kutokana na
uhaba wa nafasi majumbani, ukosefu wa muda wa kuwahudumia(shughuli na kazi
nyingi) na gharama. Huku Uzunguni huwezi
kumrushia mbwa wa jirani kipande cha mfupa au masazo ya chakula ovyo ovyo.
Hairuhusiwi. Vile vile mwenye mnyama
hatokubali. Vyakula maalum vya wanyama
huuzwa madukani na masupamaketi.
Tatizo la pili ni hulka. Kiasilia, wanyama huishi
maporini. Maisha ya mijini yenye kelele za magari, lami, uchafu wa moshi na viwanda, nk si makini kwao. Ongeza sasa hizo nafasi ndogo za
kufungiwa ndani, mbwa hukosa jaha. Wanaojiweza huajiri “watembeza mbwa”(dog-walkers) wanaotoza fedha kwa waliokwenda kazini (kwa
kukosa nafasi) kuwatembeza na kuwafanyisha mazoezi.
Hilo, moja.
La pili, mbwa huyo wa jirani
aliacha kinyesi chake pale mlangoni kwangu. Kila nilipolalamika n’lionekana eti nimejaza tu chuki. Ilitokea hata siku moja mgeni wangu akakanyaga
kinyesi cha uharo. Zingatia harufu
iliyokithiri na matusi yaliyotutoka.
Nilipogomba nikaambiwa : “Ah
nyinyi Waafrika mnachukia wanyama, mnatesa wanyama, hamna utamaduni wa elimu
viumbe!”
Baada ya malalamiko ya majuma
kadhaa, kutosikilizwa na kupuuzwa, nikaamua sasa kumvizia yule jibwa. Asubuhi
moja wakati akijisetiri mlangoni nikamvizia na tofali dogo (maana mawe hayapatikani
ovyo miji ya Ulaya) nikambabua vizuri. Kilio alichokitoa kilizagaa mithili ya
kinyamchela eneo lote lile. Magari yalisimama. Wapita njia wakaduwaa. Utadhani
nimeua. Pamoja na yale mavi kuwa
ushahidi nikaandamwa. Simu ikapigwa polisi. Dakika kumi hazikupita, king’ora
hicho. Askari watatu wakaja; pingu mkononi, vigongo. Nikazolewa mkuku hadi
kituoni.
“Akili zako ziko sawasawa?”
Nikaelezea hali mbaya ya
kinyesi na kadhalika.
“Kwanini hukuja kituoni
kushtaki?”
Nikasema sikujua kama
unatakiwa kumshtaki mbwa kwa kwenda haja
kubwa.
“Unatakiwa ndiyo. Huo ni
uchafu wa mazingira.”
Yote yalikuwa mapya kwangu. N’lizoea
mengine, Afrika.
“Umefanya kosa la jinai.
Umemdhuru kiumbe na mali ya mtu.”
Maneno yalikuwa mengi. Lakini
pamoja na ukali wao, sheria za nchi hizi
zina haki. Ukishtakiwa unapewa pia wakili. Wakili akatetea sijaishi sana nchini.
Nimezoea mazingira na utaratibu mwingine bara Afrika. Sifahamu utaratibu, nk
Nikaonywa. Lakini ilibidi kuhama; kila nilipopita
nilinyoshewa vidole kitongojini. Kampiga mbwa. Mtesa wanyama, nk.
Mbwa, paka na wanyama,
kijumla huheshimiwa sana. Na si ajabu kwamba huyu Bi Amanda Rodgers akaamua
kufunga nao pingu za kheri. Ukitazama video au sinema zinazoonyeshwa katika
mtandao wa “You Tube” utathibisha mahusiano haya. Taswira za wanaume kwa
wanawake wakipigana mabusu (midomoni) na mbwa ni nyingi sana.
Kijana wa miaka 19 , Wayne
Bryson, alifikishwa mahakamani mapema mwezi huu kwa kufanya ngono na mbwa wa
mke wake. Mke anasema asingefahamu
kilichokuwa kikiendelea kama si jamaa kujipiga picha ya video katika simu yake.
Kisa kilichojulikana zaidi
duniani ni cha dada wa Kimarekani, Alyssa
Rosales aliyefanya ngono na mbwa kwa takriban
dakika moja halafu akasambaza video Facebook na You Tube. Baada ya malalamishi iliondolewa.
Leo Alyssa katajirika kutokana na tendo hili. Ukitaka kuitazama filamu pana
malipo.
Lakini si Wazungu tu.
Video za Wakongo, Wakorea na
Wachina wakichinja mbwa, kuwauza au kuwala kama kuku zimejazana You Tube.
Yote haya yanatueleza nini
kuhusu maisha yetu ?
Je, mapya?
Sidhani. Toka zamani wanadamu tulikuwa na tabia ya “kufanya
vitendo” na wanyama. Leo vyaonekana zaidi kutokana na uwazi na usambazaji haraka wa habari. Vile vile siku
hizi wanadamu hatuoni aibu kuelezea mambo yetu ya undani, hadharani. Ni sura
halisi ya maendeleo tuliyoyafikia.
-Ilichapishwa Machi 23, 2014- Mwananchi Jumapili
No comments:
Post a Comment