Baadhi ya wananchi karibuni wamelalamikia suala
jipya la vitambulisho. Wanadai linakera; eti watu wameuawa. Kuna upendeleo. Ugumu, nk.
Kabla ya kusafiri ughaibuni miaka thelathini
iliyopita wakati wanamgambo walipokuwa
wakisimamisha simamisha wazalendo mimi vile vile nililiona suala la vitambulisho ni unyanyasaji wa serikali. Ila baada ya
kutembea na kuishi nchi nyingi duniani nimegundua vitambulisho ni jambo la kawaida. Tofauti ipo
namna vinavyoulizwa au vipi sera hii inavyotekelezwa na vyombo husika.
Tunavyojua suala la vitambulisho liliasisiwa
Tanzania mwaka 1968 kwa sababu za kiusalama baina ya nchi jirani marafiki-
Afrika Mashariki na Kati. Baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika
(kutokana na sababu mbalimbali mojawapo kufariki Rais Jomo Kenyatta wa Kenya,
1978 na serikali dhalili ya Jemadari Idi Amin wa Uganda iliyoangushwa 1979), sera
ilifyata. Hadi leo suala hili limekuwa
likifufuka fufuka na kutoweka, bila kujikita na kukaa kitako muda mrefu kama ilivyo
mataifa mengine. Ndiyo maana leo ni jambo
geni na kero kwa raia, hasa vijana.
Idi Amin na Jomo Kenyatta - miaka ya Sabini. Picha ya Kwekudee Blog
Mamlaka ya vitambulisho Tanzania(NIDA)-
imeorodhesha vipengele kumi na moja vinavyoelezea faida zake kuu. Ndani ya
orodha – kipengele cha saba kinaahidi
vitambulisho “vitafanikisha kuhakikisha kuwa mtu anapata stahili zake za jamii.
Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za pensheni, haki za matibabu, haki
za kujiunga na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia Tanzania
anastahili.”
Kimtazamo ni ahadi nzuri na muhimu. Naomba
nichangie namna mambo yanavyokuwa huku Ughaibuni.