Mara baada ya uchunguzi kutangazwa mkuu wa maadili Shirikisho la Waganga Uingereza, Profesa Vivienne Nathanson alihojiwa na runinga ya Sky akafafanua kwamba wasichana wenye miaka kumi kuendelea hulazimishwa kukatwa na ndugu zao wa kike.
Mwaka 2001 shirika la Afya
Duniani (WHO) lilikisia wanawake milioni138
duniani wamekeketwa. Desturi hii iliyojizatiti Afrika, Asia na Mashariki ya Kati inazagaa leo nchi
zilizoendelea kutokana na wahamiaji wanaokimbia vita na adha nyingine za karne ya 21.
Alice Walker mmoja wa waandishi weusi mashuhuri aliyeanza kukekemea ukeketaji toka miaka ya 1980...
Awali wataalam na waandishi wachache (kama
Mmarekani mweusi Alice Walker) tu ndiyo waliopiga kelele- ila kutokana na
wanawake wengi kufurika mahospitalini- serikali na vyombo
vyake vimeanza kuchachamaa.
Hapa Uingereza sheria kuzuia
ukeketaji ilipitishwa rasmi 2003. Sheria
inasisitiza ni uhalifu kukata sehemu
zozote za siri za msichana( ila kwa
sababu za kiafya) -hukumu yake jela miaka 14. Vyombo vya habari vinalalamika
toka sheria ilipopitishwa hakuna yeyote aliyeshtakiwa.
Sababu kuu ni kwamba familia
na ndugu za wasichana wanaokeketwa huchukuliwa kimya kimya kwao wakapasuliwa na
kurudishwa bila mkono wa sheria kufahamu.
Profesa Vivienne Nathanson anasisitiza kuwa serikali husika Afrika na Asia
zinabidi kusaidia kufuatilia mbali kero hii.
Lakini wahusika wenyewe
wanasemaje?
Mmoja wa kina mama wa Kisomali
aliyekeketwa akiwa na miaka mitano tu- Waris Dirie- anayefahamika sana duniani
baada ya miaka mingi kama mtangazaji wa mavazi na uzuri (“model”) kawa mstari wa
mbele kuupinga. Toka 1997 Waris ni balozi wa Umoja wa Mataifa akiongoza kampeni
hii.
Waris (juu na kitabu chake kinachoelezea mada hii) aliiambia Sunday Times: “Kama msichana wa Kizungu
akiumizwa – polisi mara moja huuvunja
mlango. Lakini msichana Mweusi akikeketwa hakuna anayejali. Huu ni ubaguzi wa
rangi.”
Je ukeketaji ni nini hasa?
Unapoongea na baadhi ya
wananchi hapa na nyumbani wanaelewa ukeketaji kama tohara ambayo wanaume pia hufanyiwa. Mwanaume
anapotahiriwa haumii wala kuugua baadaye-
ilhali mwanamke huteseka maisha yake yote.
Watetezi wa ukeketaji
wanasema jadi imekuwepo maelfu ya miaka kabla ya dini za Kiislamu na Kikristo.
Wataalamu wamegawanya ukeketaji
au FGM (“female genital mutilation”)
sehemu nne. Mosi ni kukiondoa kinembe ili kufifisha hisia za mwanamke. Wanabailojia wanatuambia kwa
wanawake kiungo hiki ni sawa na uume wa
mwanaume. Aina ya pili ni kuondoa kiungo hicho na mashavu au nyama
zinazouzunguka uke. Aina hii ya upasuaji ndiyo iliyoenea zaidi- na kama ile ya
kwanza ina lengo la kupunguza kabisa hisia za mhusika. Ya tatu huondoa midomo ya uke na kuishona. Baadaye hubakishwa
tundu dogo tu kupitisha mkojo na damu wakati wa hedhi. Tatizo hufika wakati
mwanamke akiwa katika siku zake au wakati wa mimba na uzazi. Wasichana ambao
bado hawajawahi kuzaa hupata shida zaidi maana damu ya hedhi haitoki sawasawa
na huziba. Aina ya mwisho ya ukeketaji
(tunaelezwa na waganga waliowatibu kina mama waliohudhuria hospitali za
Uingereza ) inahusu kuondoa nyama nzima ya uke na “kuingiza vidude mbalimbali
vinavyosababisha maumivu makali.”
Idadi ya wanawake hospitali za Uingereza iliongozeka toka 109 mwaka 2003 hadi wagonjwa 317 mwaka 2007. Kati ya matatizo ya
msingi yanayowafika wanawake hawa ni haja ndogo kuchukua wastani wa dakika 20
msalani kutokana na njia au shimo la mkojo kuziba. Pili, badala ya hedhi
kuchukua siku saba wahusika huendelea siku
28 kutokana na mfereji mdogo uliosababishwa na ukeketaji.
Alipohojiwa dada mmoja wa Sierra
Leone alidai ukeketaji humfanya mwanamke “awe msafi na mwenye afya.”
Miaka ya karibuni,
Heartlands, zahanati maalum iliyoundwa na mkunga wa Kiingereza Alison Byrne, kusaidia wanawake
wanaoteseka mjini Birmingham huhudumia
wanawake kwa kuwapasua, kuwashona upya, kuwapunguzia maumivu.
Tatizo haliko Uingereza tu.
Niliongea na mwanamke mmoja
wa Sudan aliyekimbilia nchi za Scandinavia. Mumewe alikuwa mfanyabiashara aliyesafiri
Uarabuni. “Kila akiondoka ilibidi nizibwe nisilale na mwanaume mwingine.
Akirudi nyuzi ziliondolewa. Nikishapona naanza kufanya naye tena mapenzi.
Nikiwa mja mzito na nikishajifungua- nazibwa tena. Mtoto akikua nikitaka tena
kujifungua mwingine nazibuliwa tena. Mume akisafiri nashonwa tena.”
http://www.youtube.com/watch?v=pPJEl-gyQOo
http://www.youtube.com/watch?v=pPJEl-gyQOo
Matokeo leo kukaa au kulala
shida- licha ya haja ndogo au shughuli nyingine za kibinadamu. Ilimbidi atorokee
Majuu ambapo anatibiwana mumewe kaapa
akimkamata atamuua.
Ukeketaji unapigwa vita Majuu. Mitandao kadhaa
imefunguliwa kusaidia mathalan- “Digital Spy Forum” uliochapa barua hii Jumapili ya tarehe 22:
“Ukeketaji wa wasichana ni sawa namna jadi ilivyotumika kufunga miguu
ya vigoli zamani China kusudi wasitembee- ikasababisha maumivu yasiyosemekana,
vifo vya mara kwa mara na vilema vya kudumu.”
Mwingine- Emily 222 akauliza:
“Lengo la mila hii ni
kuwataka wasichana wawe safi kabla ya kuolewa sio? Je ina maana Mungu alikosea
kuwaumba wachafu walipozaliwa? Je, Mungu alikosea kuwapa wanawake viungo sawa
na vya wanaume kusudi wasifurahie ngono? Kinachoudhi zaidi ni namna mama zao
hawa wasichana wanavyoendeleza mila hii. Huu ni udhalimu kwa watoto.”
Mwalimu Nyerere akiwa na Rais Barre wa Somalia miaka ya Sabini...Nyerere alikuwa kiongozi wa Afrika aliyepinga mila hii...
Hapa Bongo mikoa 19
inaendeleza ukeketaji uliopingwa zamani
na marehemu Mwalimu Nyerere. Wapo wanawake wanaotetea na pia wanaume wanaosema
ni jadi muhimu. Wanaume ambao wamewahi kuwa na wanawake au wapenzi waliokeketwa
hawana maoni mazuri. Mmoja aliniandikia:
“Niliwahi kuwa na Msomali,
Mburundi na Mswahili ambao wote wamekeketwa. Ilibidi niachane nao maana wakati
wa kufanya mapenzi ni dhiki tupu- hawasikii lolote. Baadaye nikagundua hata kwa
wanaume wa Kisomali kijadi kufanya mapenzi ya kimwili si muhimu. Hufanya tu
mara moja kwa msimu – kupoteza tu siku kwa kutafuna mirungi badala ya kufikiria
kama sisi wengine ambao ukiwa na mwanamke kukutana kimwili ni mojawapo ya
mapenzi ya kila siku. Nilishindwa.”
Jadi hii inayotukuza mateso
kama “utamaduni” wetu inaweza kufananishwa na
mauaji ya Albino kutumia miili yao kama suala la bahati, ushirikina au
mali. Si tu dhambi bali hudhalilisha wanawake wetu walio sehemu mahsusi ya
uzalishaji mali na wanadamu (uzazi).
Ilichapwa Mwananchi Tanzania Jumapili 6 Mei, 2012.
No comments:
Post a Comment