Moja ya nyumba zilizoporwa wakati wa ghasia mjini London majuma mawili yaliyopita ni ya mwanamuziki maarufu wa Kiingereza , Amy Winehouse aliyefariki mwezi Julai.
Ingawa uchunguzi wa nini hasa kilichomuua ungali ukiendelea hadi Oktoba, Amy Winehouse alifahamika kuwa mchapa pombe kali na dawa za kulevya wakati wa maisha yake mafupi ya miaka 27.
Mwanamuziki huyu Myahudi alikuja juu 2003 kutokana na kipaji chake cha sauti nzito ya kupendeza juu ya utenzi wa maneno aliyoyaandika kwa ustadi sana.
Akiwa shuleni alifukuzwa sababu ya tabia ya bashasha, kutosikiliza aliloambiwa, kutoboa pua. Aliimba kila mara darasani akawakera waalimu. Ingawa hakuwa bado mlevi ufundi wake wa muziki (alipiga pia gitaa) ulimpatia nafasi ndani ya vyuo mbalimbali vya sanaa ikiwepo Sylvia Young Theatre School.
Amy akiwa na babake Mitch Winehouse. Picha Shaun Curry wa Getty Images.
<--more--!>